Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfumuko wa bei watia dosari ukuaji wa uchumi duniani uliokuwa unashamiri: UNCTAD

Mizigo ikiwasili nchini Marekani.
UN News/Daniel Dickinson
Mizigo ikiwasili nchini Marekani.

Mfumuko wa bei watia dosari ukuaji wa uchumi duniani uliokuwa unashamiri: UNCTAD

Ukuaji wa Kiuchumi

Kamati ya  Umoja wa Mataifa ya Maendeleo ya Biashara duniani, UNCTAD hii leo imetoa ripoti yake kuhusu ukuaji wa biashara duniani inayoonesha kuwa licha ya biashara duniani kukadiriwa kufikia thamani ya dola trilioni 32 mwaka huu, mfumuko wa bei umerudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana nusu ya kwanza ya mwaka huu. 

Wachambuzi katika ripoti hiyo iliyotolewa leo huko mjini Geneva, nchini Uswisi wanasema ukuaji wa uchumi duniani uliporomoka na kufikia hasi katika nusu ya pili yam waka 2022. 

UNCTAD inasema biashara ya bidhaa na huduma inatarajiwa kufikia dola trilioni 25 na dola trilioni 7 mtawalia, ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. 

Kuporomoka kwa ukuaji wa uchumi kulianza robo ya tatu ya mwaka huu ambapo biashara ya bidhaa ilikuwa pungufu kwa asilimia moja ikilinganishwa na robo ya pili ambayo ni mwezi Machi hadi mwezi Mei. 

Thamani zaporomoka 

Katika ripoti yake hiyo kuhusu biashara, UNCTAD inasema ijapokuwa biashara ya huduma iliongezeka kwa asilimia 1.3 katika robo ya tatu ambayo ni mwezi Juni hadi Agosti, kwa ujumla thamani ya bidhaa na huduma zinatarajiwa kupungua kuelekea mwishoni mwa mwaka. 

Mahitaji ya bidhaa za kigeni yaliendelea mwaka 2022, ambapo kiwango cha biashara ya bidhaa hizo kiliongezeka kwa asilimia 3. 

Halikadhalika kiwango cha biashara kwa nchi za mashariki mwa Asia nacho kilihimili changamoto na kuendelea ilhali kiwango cha biashara kati ya nchi za kusini kiliporomoroka katika kipindi hicho cha robo ya tatu yam waka. 

Kwa ujumla, “mvutano wa kijiografia, mfumuko wa bei na kuporomoka kwa mahitaji duniani vinatarajiwa kuwa na madhara kwa biashara duniani mwaka 2023,” imedokeza ripoti hiyo. 

Meli ikipita Panama Canal huko Amerika ya Kati.
UN News/Daniel Dickinson
Meli ikipita Panama Canal huko Amerika ya Kati.

Vigezo viletavyo madhara 

Miongoni mwa vigezo vinavyoleta changamoto ni makadirio ya ukuaji mdogo wa uchumi mwaka 2023 kutokana na bei ya juu ya nishati, viwango vya juu vya riba, mfumuko wa bei unaoendelea katika nchi nyingi na athari za vita nchini Ukraine. 

Bei za bidhaa za vifaa na vyakula zinatarajiwa kupunguza mahitaji ya uagizaji wa bidhaa kutoka nje na hivyo kuchochea kupungua kwa kiwango cha biashara ya kimataifa. 

Viwango vya juu vya deni la kimataifa na ongezeko la viwango vya riba vinaleta hofu kubwa ya uendelevu wa deni, na kuongeza shinikizo kwa serikali zenye madeni halikadhalika madhara ya deni kwa taifa kuwa kubwa zaidi. 

Makadirio ya UNCTAD ya ukuaji wa biashara kwa mujibu wa takwimu za kitaifa
UNCTAD
Makadirio ya UNCTAD ya ukuaji wa biashara kwa mujibu wa takwimu za kitaifa

Vigezo vya kutia moyo 

Kando mwa changamoto, kuna nuru, bandari na kampuni za meli zimerekebisha mfumo wao wa usambazaji uliotikiswah na COVID-19, ambapo sasa hivi usafirishaji majini na mlundikano wa meli kwenye bandari umepatiwa utatuzi. 

Makubaliano ya hivi karibuni kama vile ubia wa kina wa kiuchumi kwenye ukanda wa Asia na Pasifiki, (RCEP) na eneo la biashara huru barani Afrika, (AfCFTA), “yanapaswa kuwa suluhu na fursa ya kuongeza kasi kwenye mfumo wa kimataifa,” imesema ripoti hiyo. 

Hata hivyo ukosefu wa uhakika na hatari zinatabiriwa kuendelea kuwa tisho kwenye mnyororo wa usambazaji wa huduma na bidhaa, lakini juhudi kuelekea uchumi usioharibu mazingira zinatarajiwa kuchochea ongezeko la mahitaji ya bidhaa endelevu kwa mazingira imesema UNCTAD huku ikipunguza mahitaji ya bihdaa zenye kiwango kikubwa cha  hewa ya ukaa na nishati ya mafuta kisukuku.