Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sekta ya huduma isisahaulike katika kusongesha biashara huru Afrika

Hifadhi ya taifa ya Tarangire nchini Tanzania ni mojawapo ya vivutio vya watalii
Lameck Kiula/GLF Nairobi 2018
Hifadhi ya taifa ya Tarangire nchini Tanzania ni mojawapo ya vivutio vya watalii

Sekta ya huduma isisahaulike katika kusongesha biashara huru Afrika

Ukuaji wa Kiuchumi

Eneo huru la biashara barani Afrika, AfCFTA, kwa sasa linalenga kuondoa vikwazo kwa biashara ya bidhaa katika nchi zote barani Afrika, lakini bado sekta ya huduma imeachwa nyuma. 
 

Hiyo ni kwa mujibu wa utafiti wa Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika, ECA, ukisema kuwa hali hiyo inatokea licha ya kwamba sekta ya huduma inachangia kwa takriban nusu ya pato la taifa katika nchi za bara hilo.

Takwimu zinaonyesha kuwa Afrika Mashariki, biashara katika sekta ya huduma inaendelea kuongezeka, kutoka dola za kimarekani bilioni 6 mwaka 2005 hadi bilioni 17 mwaka 2016, na kusaidia baadhi ya nchi za ukanda huo kupunguza nakisi ya biashara, kwa mfano Kenya na Tanzania. 

Sekta zilizochangia zaidi katika ongezeko hilo ni teknolojia na habari na mwasiliano, benki na utalii. 

Hata hivyo bado kuna changamoto zinazozuia ukuaji wa biashara ya sekta ya huduma kama anavyoelezea Geoffrey Manyara, mchumi na mtalaam wa masuala ya utalii ECA. 

“ Kwanza, vikwazo dhidi ya uuzaji wa huduma nje ya nchi bado ni vingi. Pili, gharama za huduma ni kubwa sana. Halafu, hatuna utaalam wa kutosha katika rasilimali watu.”

Kuhusu sekta ya utalii, ECA imeisaidia jumuiya ya Afrika Mashariki kuunda mkakati wa kukuza soko la utalii katika ukanda huo. 

“Tunachotarajia ni kuongeza idadi ya watalii wanaotembea Afrika Mashariki, kutoka milioni 5 mwaka 2017 hadi milioni 35 mwaka 2024. Tunataka kuona raia wa Afrika Mashariki, hasa walio kwenye tabaka la kati ama middle class, wanatalii katika nchi jirani. Ni fursa kubwa ambayo haijaangaziwa. ”