Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko AU kwa kuridhia eneo la biashara huru- UN

Eneo huru la biashara litaimarisha pia biashara baina ya nchi Afrika
Jonathan Ernst/World Bank
Eneo huru la biashara litaimarisha pia biashara baina ya nchi Afrika

Heko AU kwa kuridhia eneo la biashara huru- UN

Ukuaji wa Kiuchumi

Ajenda 2030 ya  UN na Ajenda 2063 ya AU zote zinalenga kuboresha maisha na ustawi hivyo eneo la soko huru Afrika linachagiza mafanikio ya ajenda hizo.

Umoja wa Mataifa umepongeza viongozi wa Afrika kwa hatua yao ya kihistoria ya kutia saini makubaliano ya kuanzisha eneo la biashara huru barani humo, AfCFTA.

Katibu Mkuu Antonio Guterres amesema hatua hiyo ya kuanzisha eneo la biashara kwa nchi zaidi ya 50 ni ya kihistoria.

Nawapongeza Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais Mahamadou Issoufou wa Niger na Mwenyekiti wa kamisheni ya Muungano wa Afrika, AU Moussa Faki ambao waliongoza mchakato huo,” amesema Bwana Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake.

Katibu Mkuu amesema hatua hiyo iliyofikiwa huko Kigali, Rwanda ni muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs pamoja na ajenda ya Afrika ya amani na ustawi.

Amesema kwa kuwa kuna makubaliano ya pamoja ya AU na UN ya kutekeleza ajenda 2063 ya Muungano wa Afrika na ajenda 2030 ya UN, Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia bara la Afrika linapoelekea kuanza kutekeleza makubaliano hayo ya eneo la biashara huru katika miezi ijayo.