Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza atembelea waathirika wa ukame Ethiopia atoa ahadi ya kuendelea ushirikiano na UN

Maelfu ya familia wamehama makazi yao kutokana na ukame wa hivi karibuni nchini Ethiopia
© UNHCR/Eugene Sibomana
Maelfu ya familia wamehama makazi yao kutokana na ukame wa hivi karibuni nchini Ethiopia

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza atembelea waathirika wa ukame Ethiopia atoa ahadi ya kuendelea ushirikiano na UN

Tabianchi na mazingira

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, James Cleverly akiambatana na Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF Ethiopia, Gianfranco Rotigliano wametembelea eneo la Afar, nchini Ethiopia kujionea athari za ukame kwa watoto na familia na kutathimini hatua za dharura zizazochukuliwa na UNICEF ambapo Uingereza ni mdau muhimu kama mwanachama wa Umoja wa Mataifa na muhisani.

Jamii katika maeneo ya kusini na kaskazini mashariki mwa Ethiopia bado wanateseka na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka arobaini na kuwasukuma watoto zaidi na familia zao ukingoni mwa maisha yao. Kwa ujumla, zaidi ya watu milioni 24.1 wakiwemo watoto milioni 12.6 wanakadiriwa kuathiriwa na ukame huu. 

Kutokana na changamoto za ukame, mafuriko, na migogoro, kumekuwa na ongezeko la mahitaji ya kibinadamu na kuzorota kwa mafanikio ya maendeleo. Mathalani, katika eneo moja tu la Afar, inakadiriwa kuwa watu milioni 1.7 wanahitaji msaada wa kibinadamu.  

Baadhi ya wanaotoa usaidizi mbalimbali ni ili kuunga mkono misaada ya kibinadamu ni Shirika la misaada la Uingereza, UK Aid, linalofadhiliwa na Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO) ya serikali ya Uingereza. Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza James Cleverly anasema, "jambo muhimu zaidi ambalo tunaweza kufanya ni kuunga mkono mchakato wa amani ambao unafanyika kwa sasa. Amani ni jiwe la msingi ambalo kila kitu tunachofanya kinajengwa juu yake. Lakini pia tunachohitaji kufanya ni kuhakikisha kuwa tunaendelea kuunga mkono kazi ambayo inafanywa na wadau wetu mashinani ikiwa ni pamoja na UNICEF.” 

Akishukuru hatua kama hizo zinazochukuliwa wahisani kama Uingereza kupitia UKAid, Mwakilishi wa UNICEF nchini Ethiopia, Gianfranco Rotigliano, anasema, "Ushirikiano na UK Aid/FCDO ni jambo la msingi. Imekuwa miaka mingi ambapo tunashirikiana na UK Aid/FCDO katika dharura na katika maendeleo. Kwa Ethiopia, tumepata mchango mkubwa kwa ajili ya dharura na maendeleo, kwa lishe, kwa elimu, na katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro na ukame kama hapa Afar tulipo sasa.