Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ethiopia yavunja rekodi ya India, yapanda miti milioni 350 ndani ya saa 12

Vitalu vya miti ambayo inasaidia kukabiliana na mabadilliko ya tabianchi
FAO
Vitalu vya miti ambayo inasaidia kukabiliana na mabadilliko ya tabianchi

Ethiopia yavunja rekodi ya India, yapanda miti milioni 350 ndani ya saa 12

Tabianchi na mazingira

Ethiopia imevunja rekodi ya upandaji miti kwa siku moja ambapo katika uzinduzi wa kampeni  ya  upandaji miti, imepanda zaidi ya miti milioni 350 kwenye bustai ya Gulele katika mji mkuu Addis Ababa.

Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UN Environment limesema kampeni hiyo ya kipekee inalenga kukabiliana na uharibifu wa misitu na mabadiliko ya tabianchi.

Ikiwa ni sehemu ya mpango ulioanzishwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed wa kupanda miti, kampeni hiyo inataka kuona kila siku miti milioni 200 inapandwa katika maeneo 1000 nchini kote.

Akizungumza kwenye tukio hilo Bwana Ahmed amepongeza taifa lake kwa siyo tu kukidhi mpango huo lakini pia kwa kuvuka lengo.

Miti hiyo milioni 350  ilipandwa ndani  ya saa 12 na kuvunja rekodi ambayo iliwekwa na India mwaka 2016 ya kupanda miti mingi zaidi kwa siku moja ambayo wakati huo ilikuwa miti milioni 50.

Wawakilishi kutoka Umoja wa Mataifa walishuhudia tukio hilo la aina yake ambapo Mkurugenzi wa UN Environment ofisi ya Afrika Juliette Biao amesema, “Afrika ina sifa na uwezo wa kusongesha kampeni ya upandaji miti duniani, na kwa kuzingatia kuwa imeathirika zaidi na iko hatarini zaidi, hatua za kukabili mabadiliko ya tabianchi lazima zipatiwe kipaumbele katika siku za usoni.”

Ameongeza kuwa, “sisi katika UN Environment tunaongoza katika kusaidia kujenga uwezo wa mataifa na watu wake kutekeleza wao wenyewe mikakati ya upandaji miti na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.”

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa wigo wa misitu Ethiopia umepungua na kufikia asilimia 4 kwenye miaka ya 2000 kutoka asilimia 35 mwanzoni mwa karne iliyopita ya 20.

Kwa rekodi hiyo mpya ya Ethiopia, shirika hilo la mazingira la Umoja wa Mataifa limetaka mataifa mengine ya Afrika yachukue hatua kwa kasi na kupatia changamoto suala la kukubali mambo kama yalivyo.

Wataalamu wanasema kuwa miti inasaidia bayonuai na mazingira kwa sababu kadri inavyokua, inavyonza hewa ya  ukaa ambayo ni hatari sana kwa ongezeko la joto duniani.

Kwa mujibu wa chapisho moja katika jarida la kisayansi, watafiti wanakadiria kuwa upandaji miti kote duniani unaweza kuondoa theluthi mbili ya hewa chafuzi inayoingia angani kutokana na shughuli za binadamu.