Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaongeza msaada kwa wakimbizi na familia zilizotawanywa Kaskazini mwa Ethiopia

Wanawake huko Afar nchini Ethipia wakipokea msaada wa chakula cha dharura
© WFP/Claire Nevill
Wanawake huko Afar nchini Ethipia wakipokea msaada wa chakula cha dharura

UNHCR yaongeza msaada kwa wakimbizi na familia zilizotawanywa Kaskazini mwa Ethiopia

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifan la kuhudumia wakimbizi UNHCR, linaongeza msaada kwa raia walioathirika na machafuko kwenye majimbo ya Kaskazini mwa Ethiopia ya Tigray, Afar na Amhara. 

Mwakilishi wa UNHCR nchini Ethiopia Mamadou Dian Balde leo amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva Uswis kwamba “Tangu kutiwa saini kwa makubaliano ya amani , tumeshuhudia mabadiliko makubwa katika fursa ya kufikisha misaada ya kibinadamu na uwezo wetu wa kusafirisha huduma muhimu kuingia Tigray. Kuanzia wiki hii UNHCR imeweza kutuma malori 61 kuingia Tigray yakiwa yamebeba tani 2400 za msaada muhimu unaohitajika haraka zikiwemo dawa, vifaa vya malazi, mablanketi na vifaa vya nyumbani, na lori la mafuta lilibeba lita 20,000 za petroli ili kutusaidia kufikisha msaada kwa wale wanaouhitaji zaidi.” 

Ameongeza kuwa wakati timu za UNHCR imesalia Tigray wakati wote wakiendesha shughuli zao kutokea Mekelle and Shire, UNHCR hivi sasa imeanza tena operesheni zake katika maeneo mengine kama Maichew, Adigrat, na Abi Adi. 

Ameendelea kusema kwamba “Kwa kushirikiana na idara ya serikali ya Ethiopia ya huduma kwa wakimbizi na wanaorejea nyumbani RRS na wadau wengine tumeweza kuwasaidia zaidi ya wakimbizi wa Eritrea 7,000 ambao walikuwa wamekwama kwenye makambi ya Mai Aini na Adi Harush magharibi mwa Tigray. Na sasa wamehamishiw katika makazi mapya yliyoanzishwa ya Alemwach kwenye jimbo la Amhara ambako zaidi ya waomba hifadhi na wakimbizi 22,000 kutoka Eritrea sasa wanaishi. Katika makazi ya Alemwach, watu hao wanapatiwa msaada mbalimbali na huduma muhimu.” 

Wakimbizi wa Eritrea katika mkoa wa Afar nchini Ethiopia wakipokea msaada wa dharura.
© UNHCR/Laurence Bron
Wakimbizi wa Eritrea katika mkoa wa Afar nchini Ethiopia wakipokea msaada wa dharura.

Msaada kwa wakimbizi unabadili maisha 

Kwa mujibu wa Balde msaada huo ni muhimu sana kwa wakimbizi na waomba hifadhi na unabadili kabisa maisha yao akitolea mfano mmoja wa wakimbizi aliyekutana naye Alemwach wiki iliyopita ambaye alimweleza kuwa amefurahi sana na sasa ana matumaini kwamba Watoto wake hatimaye wanaweza Kwenda shuleni tena baada ya miaka zaidi ya miwili. 

 Amesema hali kama hiyo pia inaendelea kwenye jimbo la Afar, ambako anasema “Tumesaidia kuwahamisha kwa hiyari zaidi ya wakimbizi 900 wa Eritrea kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo Semera na kuwarejesha kwenye kambi ya Barahle ambayo iliathirika na mapigano mwezi Januari mwaka huu. Na tunatumai kuanza hivi karibuni tena kutoa huduma kamili kwa kushirikiana na RRS na wadau wetu.” 

Kwa mujibu wwa UNHCR kuishi katika mazingira salama na yenye utu ni hatua moja ya suluhu kwa wakimbizi hao  ambao wamekubwa na mziunguko wa kutawanywa kila wakati. 

Hali ya wakimbizi wa Eritrea wanaoishi thiopia imekuwa mbaya wakati wote wa machafuko ya Tigray limesema shirika hilo la wakimbizi. 

“Wanachokitaka na kustahili hivi sasa ni msaada ulioratibiwa na unaoendelea kutoka kwetu sote ili waweze kujenga upya maisha yao na kuweza kujitegemea  wakisubiri suluhu ya kudumu .” 

Ushirikiano na mamlaka ya Ethiopia 

UNHCR piaimesema inafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu n amalaka za serikali Kaskazini mwa Ethiopia ili kuwasaidia raia wa Ethiopia waliotawanywa na machafuko. 

“Kati ya Januari na Oktoba mwaka huu tumewasaidia zaidi ya wakimbizi wa ndani milioni 2.1 kwa kuwapa huduma mbalimbali za ulinzi, malazi, na vifaa vya nyumbani ili warejee makwao. Pia tunmetoa ushauri nasaha na msaada mwingione kwa walio hatarini zaidi ikiwemo Watoto waliotenganishwa na familia zao, walio na mahitaji maalum na manusura wa ukatili wa kijinsia.” 

Kwa mujibu wa UNHCR hadi sasa wakimbizi wa ndani zaidi ya 50,000 wamesaidiwa kurejea nyumbani kwa hiyari Tigray, Afar na Amhara.