Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usiweke kwenye kapu moja mayai yote- Ushauri wa Irene

Kiswahili: Irene Pallangyo, (kulia) mjasiriamali wa kitanzania ambaye wakati wa janga la COVID-19 alilazimika kuanza biashara ya bidhaa mtandaoni kwa kuwa janga hilo liliathiri biashara ya kupeleka watalii kwenye mbuga za wanyama.
UN News
Kiswahili: Irene Pallangyo, (kulia) mjasiriamali wa kitanzania ambaye wakati wa janga la COVID-19 alilazimika kuanza biashara ya bidhaa mtandaoni kwa kuwa janga hilo liliathiri biashara ya kupeleka watalii kwenye mbuga za wanyama.

Usiweke kwenye kapu moja mayai yote- Ushauri wa Irene

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ugonjwa wa COVID-19 ulipotangazwa na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO kuwa ni janga la afya ya dunia mwezi Januari mwaka 2020, watu wengi hawakutarajia kile ambacho kingalifuatia baada ya hapo, kuanzia athari kiafya, kiuchumi na kijamii. 

Kama takwimu za Umoja wa Mataifa zinavyoonesha kuwa mamilioni ya watu walipoteza ajira zao na biashara kufungwa au kudorora, Irene Pallangyo, mjasiriamali kutoka mkoa wa Arusha nchini Tanzania alikuwa ni miongoni mwa waliomo kwenye takwimu hizo. 

Bi. Pillangyo akihojiwa na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa hivi karibu alipokuwa ziarani nchini Marekani kikazi anasema “baada ya kumaliza Chuo niliajiriwa na kwa miaka sita kwenye kampuni moja mkoani Arusha, kaskazini mwa Tanzania, lakini kwa kuwa sijatoka kwenye familia yenye uwezo, nilitamani kwamba nifanye kitu kingine cha kuniongezea kipato ili hatimaye nipandishe uchumi wangu na wa wale wanaonizunguka. Kwa hiyo ndipo wazo la kuanzisha kampuni ya utalii lilipokuja wakati bado niko kazini.” 

Alianzisha kampuni iitwayo Muraa African Safaris ya kupeleka watalii kwenye mbuga za wanyama akisema kuwa alipenda kuingia kwenye biashara hiyo kwa sababu alikuwa anaona vijana na wanawake wanafanya biashara hiyo “kwa nini na mimi nisifanye?” 

Irene Pallangyo, (kushoto) mjasiriamali wa kitanzania ambaye wakati wa janga la COVID-19 alilazimika kuanza biashara ya bidhaa mtandaoni kwa kuwa janga hilo liliathiri biashara ya kupeleka watalii kwenye mbuga za wanyama.
UN News
Irene Pallangyo, (kushoto) mjasiriamali wa kitanzania ambaye wakati wa janga la COVID-19 alilazimika kuanza biashara ya bidhaa mtandaoni kwa kuwa janga hilo liliathiri biashara ya kupeleka watalii kwenye mbuga za wanyama.

COVID-19 ilitikisa sasa nimejifunza umuhimu wa kujijengea mnepo 

Mkurugenzi huyu wa Muraa African Safaris anasema biashara ya kupeleka watalii ilishamiri kwa mwaka mmoja tu kisha COVID-19 ikabisha hodi. 

“Baada ya kuingia kwa COVID-19 hali ilikuwa ngumu kwa kweli,” anasema Bi. Pallangayo akiongeza kuwa wakati huo sasa alishaacha kazi ya kuajiriwa na alikuwa na familia na watoto wawili. “Lakini nilianza kuuza vitu vidogo vidogo kupitia mtandao wa WhatsApp. Nilinunua vitu Dar es salaam, mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania, na kisha kuwauzia watu jijini Arusha. Nilifanya hivyo kwa wakati huo na hata sasa ninaendelea sambamba na kazi yangu ya kupeleka watalii mbugani lakini si kwa kiasi kikubwa.” 

Akaulizwa ni jambo gani amejifunza ili kujijengea mnepo kwa siku za usoni na ndipo akasema, “nilichojifunza na kila mtu afanye ni kwamba usiweke mayai yote kwenye kikapu kimoja. Kama una biashara unafanya au una kazi umeajiriwa, jitahidi uwe una kazi pembeni. Mfano kama una sehemu unauza chakula, ikatokea mlipuko wa kipindupindu, angalau uwe na shamba unalima utapata kipato. Yaani mtu uwe na kitu unafanya kando ya ile kazi yako kuu.” 

Muraa African Safaris na utalii endelevu unaolinda mazingira 

Umoja wa Mataifa kupitia malengo ya maendeleo endelevu, SDGs unasisitiza umuhimu wa utalii endelevu na Muraa African Safaris inatekeleza ili kuhakikisha kuwa kinachofanyika sasa hakiharibu mazingira ya vizazi vijavyo. 

Bi. Pallangayo akafafanua wanavyotekeleza akisema, “utalii ambao sisi tunafanya ni endelevu ambao tunatamani kama tulivyoukuta uendelee kuwepo. Kwa hiyo tunajitahidi kadri tunavyoweza kutunza mazingira. Kwa hiyo wakati watalii wanapokuwa mbugani tunawahimiza mara kwa mara kutokutupa chupa, wala kutokufanya vitendo vyovyote vitakavyoathiri mazingira na wanyama walioko mbugani. Hata tunapowapokea uwanja wa ndege wanapofika tunawapatia maelezo ya mwanzo kama wakiwa mbugani ni kipi wafanye na kipi wasifanye, kama vile wasitupe chupa, mifuko ya plastiki au kulisha wanyama, na vyote hivi tunawaeleza kabla ya kwenda mbugani.”