Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vyanzo vya maji zamani havikukauka kama sasa, jua ni Kali mno- Mfugaji 

Mabinti wakiwa wametoka kuteka maji
© UNICEF/Scott Moncrieff
Mabinti wakiwa wametoka kuteka maji

Vyanzo vya maji zamani havikukauka kama sasa, jua ni Kali mno- Mfugaji 

Tabianchi na mazingira

Umoja wa Mataifa ukiendelea kutaka hatua zaidi kwa ajili ya tabianchi kama njia mojawapo ya kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi nchini Tanzania madhara hayo yako dhahiri kwa wafugaji wa wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha ambao kupitia taarifa hii iliyoandaliwa na Mathias Tooko wa Radio washirika Loliondo FM wanaeleza hali ilivyokuwa zamani na sasa. 

Wilayani ngorongoro baadhi ya wafugaji wameonekana kupata adha ya maji safi kwa matumizi ya nyumbani na mifugo kama anavyotueleza Loltudula Rakatia ambaye ni Mwenyekiti wa kijiji cha Lopolun tarafa ya Loliondo. 

“Unaona watu wanavyohangaika kupata maji, binadamu, mifugo na wanyamapori sote tunategemea haya maji. Ili mifugo wapate kunywa maji tunachota kwa kutumia madumu. Hivyo tunaona mabadiliko makubwa ya tabianchi, misimu imebadilika,mvua imepungua na vyanzo vya maji vimekauka.” 

Jamii katika kukabiliana na hali  kundi la wakina mama limeonekana kuuumia zaidi na janga hili, kwa kufuata maji na majani ya ngombe wanaoshidwa kutoka nyumbani kufuata maji na majani umbali mrefu.Nooseuri Lupa ni shuhuda. 

“Sisi ndio tunaumia zaidi, majukumu yetu ni mengi nyumbani, kulea familia, kuteka maji, kuhudumia mifugo pamoja na kuokota kuni. Tunapata adha kubwa ya maji na tunapitia mazingira magumu katika kutimiza majukumu haya. Miaka ya nyuma maji haikuwa tatizo kama hivi sasa. Vyanzo vya maji vilikuwa karibu na havikuwahi kukauka tofauti na sasa kwa sababu hakuna mvua, jua limezidi kuwa Kali na majira yamebadilika.” 

Maafisa wa mazingira na mifugo wilayani hapa licha ya kushauri jamii kupunguza mifugo pia wameasa jamii kuwa makini na kuacha kukata miti kwa ajili ya kulisha mifugo kipindi hiki, kwani huchangia kusababisha hali kuzidi kuwa mbaya miaka ijayo.