Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamishna wa Haki za Binadamu wa UN ziarani nchini Ukraine

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Volker Türk akiwa mji mkuu wa Ukraine Kyiv mwanzoni mwa ziara rasmi nchini humo
OHCHR
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Volker Türk akiwa mji mkuu wa Ukraine Kyiv mwanzoni mwa ziara rasmi nchini humo

Kamishna wa Haki za Binadamu wa UN ziarani nchini Ukraine

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Volker Türk ameanza ziara ya siku nne nchini Ukraine hapo jana Jumapili Desemba 4 kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo akiwa ameongozana na wafanyakazi wa ofisi yake wanaohusika na kufuatilia masuala ya haki za binadamu.

“Niko Ukraine kwa wakati huu kuonesha mshikamano na waathirika wa vita hii ya kutisha” … Ni maneno ya kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu Volker Türk akiwa nchini Ukraine ambapo ametembelea taifa hilo lililoanza kushambuliwa na nchi ya Urusi mwezi February mwaka huu.

Katika siku ya kwanza ya ziara yake alitembelea katika mji wa Kyiv na maeneo ya jirani, Bucha na Irpin.

Video ya Ofisi ya Kamishna huyo inamuonesha akizungumza katika eneo ambalo nyuma yake theluji imetanda kuonesha dhahiri ni msimu wa baridi Kali.

…. Anasema, “Unaweza kuona mazingira ya msimu wa baridi, lakini ni mazingira ya msimu wa baridi ambayo inamaanisha watu wengi wako katika mazingira magumu, shida nyingi kwa sababu wanaganda kutokana na umeme kukatika wakati mwingine, miundombinu ya umeme haifanyi kazi na wananchi hata hawajui jinsi ya kupita katika kipindi hiki cha baridi.”

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za binadamu imekuwa ikitelekeza shughuli zake nchini Ukraine tangu mwaka 2014 ambapo imekuwa ikifuatilia ukiukwaji wa haki za binadamu, na Kamishna Turk anasema ujumbe wake katika ziara hii ni kuwa

“Vita haina maana. Mauaji ya aina hii hayakubaliki kabisa na hayana maana. Ninaweza tu kutoa wito kwa wale ambao wamefanya hivi kwamba waache kufanya hivyo, na waheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu, haki za binadamu na haki”.

Ziara yake hiyo ya siku nne nchini Ukriane itamkutanisha na maafisa wakuu wa serikali ya kitaifa na serikali za mitaa, mashirika ya kiraia, pamoja na wawakilishi wa vikundi vya waathirika, pamoja na jamaa za raia waliopotea au waliotekwa na wafungwa wa vita.

Ziara ya Türk itakamilika tarehe 7 Desemba ambapo anatarajiwa kufanya mkutano wa wanahabari mjini Kyiv nchini humo Ukraine.