Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taarifa za awali zadokeza uhalifu wa kivita na ukiukwaji wa haki za binadamu Ukraine- Kamisheni 

Mji wa Bucha umeharibiwa vibaya kufuatia mashambulio Kyiv, mji mkuu wa Ukraine.
© WFP/Marco Frattini
Mji wa Bucha umeharibiwa vibaya kufuatia mashambulio Kyiv, mji mkuu wa Ukraine.

Taarifa za awali zadokeza uhalifu wa kivita na ukiukwaji wa haki za binadamu Ukraine- Kamisheni 

Amani na Usalama

Kamisheni iliyoundwa na Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu kuchunguza madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu nchini Ukraine imetoa ripoti ya ziara yake ya kwanza nchini Ukraine na kusema ingawa haiko katika nafasi ya kuwa na vigezo vya kisheria au matokeo kamilifu, taarifa za awali zinadokeza kuweko kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za kimataifa za kiutu. 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, Erik Møse ambaye ni Mwenyekiti wa kamisheni hiyo inayoundwa na watu watatu ikwemo Bi.Jasminka Džumhur na Pablo de Greiff Bwana Møse amesema, “ingawa tumefanya ziara tukiwa na watendaji wachache, katika hatua ya sasa kwa kutegemea pia uthibitisho wa siku za usoni, na taarifa tulizopokea na maeneo yaliyoharibiwa ambayo tumezuru, vinaunga mkono madai ya ukiukwaji wa sheria ya haki za binadamu, sheria ya kimataifa ya kiutu na labda uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.” 

Kilichobainika Ukraine 

Ametaja maeneo ya Bucha na Irpin ambako wamepata taarifa za mauaji ya kiholela dhidi ya raia, uharibifu na uporaji wa mali, pamoja na mashambulizi dhidi ya miundombinu ya kiraia zikiwemo shule. 

“Huko mikoa ya Kharkiv na Sumy, Kamisheni imeshuhudia uharibifu maeneo ya mijini, ikidaiwa kuwa ni matokeo ya mashambulizi ya mabomu kutoka angani, makombora au mashambulizi yaliyolenga moja kwa moja raia,” amesema Bwana Møse. 

Jasminka Džumhur ambaye ni mjumbe wa Kamisheni hiyo amesema walipata pia fursa ya kuzungumza na wakimbizi wa ndani wakiwemo waliotoka MAshariki mwa Ukraine. 

“Shuhuda zao zinajumuisha simulizi za uharibifu wa mali za raia, uporaji, kufungiwa ndani, manyanyaso na kutoweshwa kwa raia. Kuna ripoti pia za ubakaji na aina nyingine za ukatili wa kingono,” amesema Bi. Džumhur huku akisema kuwa madai hayo yote yatachunguzwa kwa kina siku za usoni. 

Watoto wamebadilishwa uraia kinguvu na hata kuasiliwa

Amesema shaka na shuku ya Kamisheni hiyo ni madhara ya vita kwa watoto, “na Kamisheni inafikiria ni vema kuchunguza zaidi rioti kuhusu watoto kudaiwa kuhamishiwa kwenda katika  maeneo ambayo yalishikiliwa kwa muda mfupi na Urusi na taarifa ya kasi ya kubadilisha uraia wa watoto na kuwaasili.” 

Watoto wengi wakimbizi wa ndani nchini Ukraine wametengana na familia zao, huku uharibifu wa shule au matumizi yake kama malazi kwa wakimbizi wa ndani  vinatia hofu kuhusu mustakabali wao wa kupata elimu. 

Mama na binti yake wakikimbia ghasia kwenye eneo la Bucha jimboni Kyiv nchini Ukraine
© UNDP/Oleksandr Ratush
Mama na binti yake wakikimbia ghasia kwenye eneo la Bucha jimboni Kyiv nchini Ukraine

Tutazingatia mustakabali wa manusura na waathirika 

Mjumbe huyo amesisitiza kuwa Kamisheni hiyo katika kuendesha kazi yake itazingatia mfumo wa kuweka manusura na waathirika kama kitovu cha kazi yao, hali ambayo itatoa fursa pia ya wahusika wa uhalifu wanawajibishwa na zaidi ya yote manusura wanapatiwa fursa ya kujenga upya Maisha yao. 

Amesema serikali ya Ukraine kwa upande wake inajitahidi kukidhi mahitaji ya manusura ingawa kuna changamoto wakati huu ambapo bado mashambulizi kutoka Urusi yanaendelea. 

Kitakachofuata baadaye

Akizungumzia kitakachofuata baada ya ziara hii ya kwanza, Pablo de Greiff ambaye pia ni mjumbe amesema, “ziara zitakazofuatia zitafikisha wajumbe kwenye maeneo mengine ya Ukraine kabla ya kuwasilisha ripoti kamili mbele ya Baraza la Umoja wa Mataifa la haki za binadamu mwezi Septemba mwaka huu. 

“Tutaendelea na mchakato wa kukusanya Ushahidi ambao unaweza kutumika katika hatua za uwajibishaji wahusika,” amesema Bwana de Greiff. 

Wakiwa kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, wajumbe walikutana na wawakilishi wa serikali, Bunge, Wizara na Mwendesha Mashtaka Mkuu. Halikadhalika walikutana na wawakilishi wa mashirika ya kiraia. 

Tarehe 4 mwezi Machi mwaka huu wa 2022 Baraza la Haki za Binadamu lilipitisha azimio la kuanzisha Kamisheni Huru ya uchunguzi dhidi ya ukiukwaji wa haki kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na kuchagua wajumbe watatu.