Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa uwiano kwenye sekta ya afya wahatarisha uhai wa watu wenye ulemavu- WHO

Thomas Dieme, ana umri wa miaka 60. Aliweza kutembea hadi mwaka 1964 alipougua polio na kuwa na ulemavu.
UNICEF Senegal
Thomas Dieme, ana umri wa miaka 60. Aliweza kutembea hadi mwaka 1964 alipougua polio na kuwa na ulemavu.

Ukosefu wa uwiano kwenye sekta ya afya wahatarisha uhai wa watu wenye ulemavu- WHO

Afya

Ushahidi mpya umedhihirisha kuwa watu wenye ulemavu wako hatarini zaidi kukumbwa na vifo vya mapema au magonjwa mengine kuliko watu wasio na ulemavu, imesema ripoti mpya iliyozinduliwa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, kuelekea siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu kesho Desemba 3.

Taarifa iliyotolewa leo na WHO huko Geneva, Uswisi inanukuu ripoti hiyo iliyopatiwa jina Ripoti ya kimataifa kuhusu uwiano wa afya kwa watu wenye ulemavu, ikisema kutokana na mifumo iliyodumu ya ukosefu wa uwiano kwenye afya, watu wengi wenye ulemavu wanakabiliwa na hatari ya kufa mapema, hata miaka 20 kabla ya wakati wao kuliko watu wasio na ulemavu.

Idadi ya watu wenye ulemavu duniani yaongezeka, huduma zawaengua

Watu hao wenye ulemavu wana hatari  maradufu zaidi ya kupata magonjwa sugu kama vile pumu, msongo wa mawazo, utipwatipwa, magonjwa ya kinywa na kiharusi.

“Tofauti nyingi za hali ya kiafya haziwezi kuelezwa kwa magonjwa yanayomsibu au ulemavu, lakini kwa vigezo visivyo sawa na haki,” imesema ripoti hiyo.

Idadi ya watu wenye ulemavu duniani imeongezeka na kufikia watu bilioni 1.3, sawa na mtu mlemavu 1 katika kila watu 6, idadi ambayo kwa mujibu wa ripoti hiyo, “inatoa msisitizo wa umuhimu wa kufanikisha ujumuishi na ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika masuala yote ya kijamii ikiwemo afya bila ubaguzi wowote.”

Vigezo visivyo vya haki: Sababu kuu ya tofauti kwenye afya

Ripoti inasisitiza kuwa kuna umuhimu wa kuchukua hatua kuondoa pengo la ukosefu wa usawa na uwiano kwenye mifumo ya afya, pengo ambalo linatofautisha matokeo ya kiafya kwa watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu.

Mathalani, watoa huduma ya afya kuwa na mtazamo hasi au unyanyapaa kwa wagonjwa wenye ulemavu, taarifa za afya ambazo hazieleweki kwa watu wenye ulemavu, au watu wenye ulemavu kushindwa kufikia huduma za afya kutokana na miundombinu isiyo rafiki, bila kusahau ukosefu wa usafiri na fedha.

Waichana walio na ulemavu wakicheza mpira wa vikapu nchini DRC.
© UNOCHA/Maxime Nama
Waichana walio na ulemavu wakicheza mpira wa vikapu nchini DRC.

“Mifumo ya afya lazima iboreshwe ili kuondoa changamoto zinazokabili watu wenye ulemavu badala ya mifumo hiyo kuwa kikwazo kwa watu hao,” amesema Dkt. Tedros Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO.

Amesisitiza kuwa ripoti hii inaangazia ukosefu wa uwiano kwenye huduma za afya ambao watu wenye ulemavu wanakumbana nao wanapojaribu kupata huduma za afya wanazohitaji.

“WHO imejizatiti kusaidia nchi kwa kupatia miongozo inayohitaji kuhakikisha watu wote wenye ulemavu wanapata huduma bora za afya,” amesema Dkt. Tedros.

Kujumuisha watu wenye ulemavu kwenye afya kutainua uchumi wa nchi

Kwa kutambua kuwa kila mtu ana haki sawa ya kupata kiwango cha juu cha huduma ya afya, ripoti inatoa uchambuzi muhimu wa kiuchumi wa kupitisha mfumo jukmuishi kwenye afya. “Inaonesha kuwa kuwekeza kwenye mfumo jumuishi wa kiafya ni njia bora na nafuaa kigharama.”

Serikali zinaweza kupata dola 10 kwa kila dola 1 inayowekeza kwenye mfumo jumuishi wa afya kwa watu wenye ulemavu katika tiba na kinga dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Halikadhalika huduma za mpango wa uzazi na chanjo zina ufanisi kigharama iwapo zitatekelezwa kupitia mpango unaojumuisha pia watu wenye ulemavu.