Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu wa UN na Rais wa Uturuki wajadili matarajio ya amani ya Ukraine 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekutana na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan mjini Ankara.
UN/Stéphane Dujarric
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekutana na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan mjini Ankara.

Katibu Mkuu wa UN na Rais wa Uturuki wajadili matarajio ya amani ya Ukraine 

Masuala ya UM

 Leo 25 Aprili, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekutana na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan mjini Ankara. 

Viongozi hao wawili wamejadili uwezekano wa kusitisha vita nchini Ukraine na kupunguza madhila kwa raia wa nchi hiyo. 

"Antonio Guterres ameonyesha kuunga mkono juhudi za kidiplomasia za Uturuki zinazohusiana na vita vya Ukraine," msemaji wa Umoja wa Mataifa alisema katika taarifa iliyotolewa leo.  

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa na rais wa Uturuki wamesisitiza nia yao ya pamoja ya kufikia amani ya mapema kwa taifa la Ukraine, na pia "kuunda mazingira ambayo yatakomesha mateso kwa mamilioni ya raia."  

Viongozi hao pia wamesisitiza haja ya kuweka njia za kibinadamu kwa ajili ya kuwahamisha raia na kuwasilisha misaada inayohitajika katika maeneo yaliyoathirika. 

Guterres na Erdogan wamekubaliana kudumisha mawasiliano ili kujadili mipango ya amani.  

Pia wamejadili athari za vita vya Ukraine kwa kanda hiyo na dunia kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na kupanda kwa bei za nishati, chakula na huduma za kifedha. 

Kutoka Ankara, Katibu Mkuu António Guterres anasafiri hadi Moscow, ambapo kesho Jumanne atafanya mkutano wa kikazi na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Sergei Lavrov, na pia atapokelewa na Rais wa Urusi Vladimir Putin. 

Na hapo Aprili 28, mkuu wa Umoja wa Mataifa anapanga kuelekea mjini Kyiv, Ukraine ambako atafanya mkutano wa kikazi na waziri wa nmambo ya nje Dmitry Kuleba na atapokelewa na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.