Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunalaani matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji Sudan: UNITAMS/AU/IGAD

Waandamanaji wameingia mitaani katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum tarehe 11 Aprili 2019,
UN Sudan/Ayman Suliman
Waandamanaji wameingia mitaani katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum tarehe 11 Aprili 2019,

Tunalaani matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji Sudan: UNITAMS/AU/IGAD

Amani na Usalama

Mchakato wa pande tatu nchini Sudan ambao ni mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNITAMS, Muungano wa Afrika AU na mamlaka za kitaifa kwa ajili ya maendeleo kwenye Pembe ya Afrika IGAD wamelaani vikali machafuko na matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji nchini Sudan.

Katika taarifa yao iliyotolewa leo mjini Khartoum wadau hao watatu wamesema matumizi hayo ya nguvu kupita kiasia yameshasababisha vifo vya watu wawili Alhamisi iliyopita kwenye mji wa Omdurman na kufanya idadi ya vifo hadi sasa kufikia 121 na mamia wamejeruhiwa tangu jeshi lilipofanya mapinduzi tarehe 25 Oktoba mwaka 2021. 

Wawakilishi wa AU, IGAD na UNITAMS pia wametuma salamu za rambirambi kwa familia za waathirika na kuwatakia ahuweni ya haraka majeruhi. 

Pia wamekumbusha kwamba “kila mtu ana haki ya kukusanyika kwa amani na uhuru wa kujieleza” 

Na wametoa wito kwa mamlaka ya Sudan kufanya uchunguzi wa  matukio hayo na kuhakikisha wahusika wanafikishwa kwenye mkono wa sheria. 

Muungano wa Afrika, IGAD na UNITAMS wamesema wanaebndelea kufanyakazi pamoja ili kurejesha kipindi cha mpito ambacho kitakuwa endelevu na kuruhusu kuundwa kwa serikali ya kiraia ambayo ni ya kuaminika, ya kidemokrasia na inayowajibika katikia kuleta amani na maendeleo kwa taifa hilo.