Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan hakikisheni haki ya kuandamana na kujieleza-OHCHR

Ravina Shamdasani, msemaji wa ofisi ya haki za binadamu.
Photo UN Multimedia
Ravina Shamdasani, msemaji wa ofisi ya haki za binadamu.

Sudan hakikisheni haki ya kuandamana na kujieleza-OHCHR

Amani na Usalama

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR imesema imepokea taarifa kuhusu matumizi ya vitoa machozi na risasi za moto na vikosi vya usalama nchini Sudan.

Hayo ni kwa mujibu wa msemaji wa OHCHR, mjini Geneva, Uswisi, Ravina Shmdasani kufuatia swali kutoka kwa mwandishi habari ambapo amesema licha ya kwamba vikosi vya usalama, jeshi na vikosi vinavy unga mkono serikali vinashiriki vitendo hivyo lakini, serikali ina wajibu wa kulinda waandamanaji.

Bi. Shamdasani akimnukuu Kamishna Mkuu wa haki za binadamu amesema, Michelle Bachelet, amesema kuwa katika matukio mbali mbali ameelezea wasiwasi wake kuhusu matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji tangu kudorora kwa hali mwezi Disemba mwaka jana wa 2018.

Msemaji huyo wa OHCHR amesema, “ni vigumu kufahamu idadi kamili ya watu waliouawa katika mapigano hayo; huku baadhi ya makundi ya haki za binadamu yakikadiria kwamba watu 70 wamepoteza maisha wakati serikali ikitoa idadi ya waliopoteza maisha kwamba ni watu 46.  

OHCHR imetoa wito kwa serikali na vikosi vya usalama kuhakikisha haki ya kuandamana kwa amani na uhuru wa kujieleza vinaheshimiwa na kwamba majadiliano ya kweli yanafanyika kutatua hali tete inayoshuhudiwa kutokana na malalamiko ya umma kuhusu hali ya kiuchumi na kijamii.

Ripoti hii ya OHCHR imekuja baada ya taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres kwamba anafuatilia maandamno nchini Sudan kwa karibu na kutoa wito kwa pande husika kujizuia na kujizuia na vitendo vya ukatili wakati huo huo akitoa wito kuachiwa huru waandamanaji waliozuiliwa.