Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna mwanafunzi anayestahili kuzikwa na sare za shule:UNICEF

Nidhamu, walimu na miundombinu bora ni muhimu katika kumhakikishia mwanafunzi elimu bora.
© UNHCR/Diana Diaz
Nidhamu, walimu na miundombinu bora ni muhimu katika kumhakikishia mwanafunzi elimu bora.

Hakuna mwanafunzi anayestahili kuzikwa na sare za shule:UNICEF

Amani na Usalama

Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF nchini Sudan Abdullah Fadil amesema amesikitishwa na kughadhibishwa na tukio la ufyatuaji risasi lililosababisha vifo vya angalau wanafunzi watano wa shule ya sekondari na kujeruhi wengine wengi katika eneo la El Obeid jimbo la North Kordofan nchini humo.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo kwa niaba ya UNICEF Fadil amesema “tunatuma salamu zetu za rambirambi kwa familia, wanafunzi wa shule hiyo na jamii nzima kwa ujumla kufuatia mkasa huu.”

Ameongeza kuwa watoto hao waliopoteza maisha “Ni wa umri wa kati ya miaka 15-17 na walikuwa wakiandamana kupinga muanza kwa muhula wa masomo wakati huu ambapo sintofahamu ya kisiasa inaighubika Sudan”.

Duru za Habari zinasema maandamano hayo yamefanyika ikiwa ni siku moja tu kabla ya mkutano ulioopangwa kufanyika kesho jumanne baina ya viongozi wa maandamano na majenerali wanaoongoza nchi kwa sasa kujadili serikali ya mseto ikiwa ni pamoja na jinsi gani madaraka yahamishwe kutoka mikoni mwa jeshi na kuingia kwenye serikali ya ushirika wa kijeshi na kiraia ambayo hatimaye itakabidhi madaraka hayo kwenye utawala wa kiraia.

Mwakilishi wa UNICEF Sudan amesisitiza kuwa “Hakuna mwanafunzi anayestahili kuzikwa na sare za shule , UNICEF inazitaka pande zote katika maandamano hayo yaliyoghubikwa na machafuko kuwalinda Watoto wakati wote na kuwanusuru na maafa kwa kuzingatia wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu na misingi ya haki za binadamu.”

UNICEF pia imetoa wito kwa pande zote kuheshimu mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto na sheria ya Watoto ya Sudan yam waka 2010, na hivyo kujizuia na vitendo vyovyote vya ukiukwaji wa haki za Watoto ikiwemo kuwaingiza jeshini na kuwatumia katika vikosi vya kijeshi au makundi yenye silaha.

Shirika hilo la watoto limeitaka serikali ya Sudan kuchunguza na kuwawajibisha watekelezaji wa ukatili huo dhidi ya watoto.

UNICEF imeahidi kuendelea kufanyakazi kwa karibu na wadau wa kitaifa na jumuiya ya kimataifa ili kulinda na kutekeleza haki za mtoto nchini Sudan.