Chonde chonde Sudan jizuieni na machafuko:Guterres

8 Aprili 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa pande zote katika vurugu zinazoendelea sasa nchini Sudan kujizuia na matumizi ya nguvu na kuepuka machafuko.

Kufuatia tarifa iliyotolewa na msemaji wake hii leo mjini New York Marekani Guterres amesema anafuatilia kwa karibu maandamano yaliyoingia siku ya pili na kuzitaka pande zote kuheshimu haki za binadamu, ikiwemo uhuru wa kukusanyika, uhuru wa kujieleza na kuwaachilia waandamanaji wanaoshikiliwa rumande.

Pia ameitaka serikali ya Sudan kuweka mazingira mujarabu kwa ajili ya kusuluhisha hali inayoendelea hivi sasa na kuchagiza majadiliano jumuishi. Kwa mujibu wa duru za Habari maandamano hayo ni ya kutaka Rais Omar al-Bashir kung’atuka madarakani.

Maelfu ya waandamanaji wameelezewa kukita kambi nje ya makao makuu ya jeshi la nchi hiyo wakimtaka Bashir kujiuzulu ili kufungua serikali ya mpito. Hadi sasa Rais Bashir amekataa kuondoka madarakani kwa madai kwamba wapinzani wake wanapaswa kutafuta madaraka kwa kupitia mchakato wa uchaguzi.

Rais Bashir aliingia madarakani baada ya mapinzuzi mwaka Oktoba 1993 aliteuliwa na baraza la mapinduzi na kisha kuthibitishwa kidemokrasia baada  ya uchaguzi mkuu mwaka 1996 nafasi anayoishikilia hadi sasa.

Katibu Mkuu Guterres amesisitiza kwamba Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia juhudi zozote zitakazokubalika na Wasudan ili kutatua mgogoro wa sasa kwa njia ya amani.

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter