Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yaendelea na doria wakati mapigano yakianza tena kati ya M23 na FARDC, Kivu Kaskazini

Askari ya kijeshi wa MONUSCO wakijificha kwenye kilima cha Munigi wakati wa shambulio la FARDC dhidi ya maeneo ya M23 huko Kanyaruchinya karibu na Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Photo: MONUSCO/Sylvain Liechti
Askari ya kijeshi wa MONUSCO wakijificha kwenye kilima cha Munigi wakati wa shambulio la FARDC dhidi ya maeneo ya M23 huko Kanyaruchinya karibu na Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

MONUSCO yaendelea na doria wakati mapigano yakianza tena kati ya M23 na FARDC, Kivu Kaskazini

Amani na Usalama

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC mapigano kati ya jeshi la serikali FARDC na waasi wa kundi la M23 yalianza tena jana Jumapili kwenye eneo la Kibumba jimboni Kivu Kaskazini mashariki mwa taifa hilo. 

Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq, akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya

Umoja huo jijini New York, Marekani hii leo amesema “tuna taarifa mpya kutoka DRC ambako ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO unasema mapigano kati ya FARDC na M23 yameanza tena jana.” 

 Amesema kwa upande wa kaskazini, M23 wamesonga na kufikia eneo la Katwiguru, kilometa 11 kutoka mji wa Nyamilima. 

Amesema MONUSCO inaendelea kuendesha doria za pamoja na jeshi la serikali, FARDC kwenye barabara ya kitaifa namba 2 kutoka Sake hadi Kibati, huku wakiwa wanaungwa mkono kwa uthabiti na wakazi wa jimbo la kivu Kaskazini. 

Bwana Haq amesisitiza kuwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaendelea kushirikiana kwa karibu na jamii za wenyeji ili kuelewa vema hali ya usalama na kuchukua hatua kwa haraka kukidhi mahitaji ya usalama wa jamii hizo kwa mujibu wa mamlaka ambayo MONUSCO imepatiwa ya kulinda raia.