Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fahamu mambo 10 ya kutokomeza ukatili wa kijinsia

Zekia Musa ni mwanaharakati kijana ambaye ana ulemavu wa macho .Yeye ana umri wa miaka 29 na pamoja na kufanya kazi na Wizara ya Elimu Sudan Kusini, anasaidia kujengea uwezo watoto wasioona.
Maura Ajak
Zekia Musa ni mwanaharakati kijana ambaye ana ulemavu wa macho .Yeye ana umri wa miaka 29 na pamoja na kufanya kazi na Wizara ya Elimu Sudan Kusini, anasaidia kujengea uwezo watoto wasioona.

Fahamu mambo 10 ya kutokomeza ukatili wa kijinsia

Wanawake

Ukatili dhidi ya wanawake na wasichan unasalia kuwa kitendo cha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu duniani kote, ukiathiri zaidi ya wanawake milioni 1.3, takwimu ambayo hata hivyo haijabadilika kwa zaidi ya muongo mmoja.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women kupitia wavuti wake linasema dharura duniani, majanga, mizozo, na vita vinazidi kuongeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichan na kuchochea visababishi na hatari zaidi.

Mabadiliko ya tabianchi yanachochea aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na wasichana na tayari kuna mwenendo ulio dhahiri ambao pasi shaka unazidi kupanuka kadri janga la tabianchi nchi linavyozidi kuwa baya. Kasi ya meandeleo ya teknolojia nayo yanaongeza ukatili wa wanawake na wasichana kupitia mtandaoni na kuibua vitisho vipya dhidi ya haki za makundi hayo.

Na wakati huo huo kumekuweko na ongezeko la harakati dhidi ya makundi yanayotetea haki pamoja na yale yanayosimamia masuala ya wanawake, na hivyo kurejesha nyuma sheria ambazo tayari zilishasongesha maendeleo ya utetezi wa haki za wanawake, halikadhalika kutishia mustakabali wa watetezi wa haki za wanawake,

Mfuko wa kusaidia manusura wa ukatili na unyanyasaji wa kingono umesaidia wanawake huko DR Congo kujifunza kilimo cha uyoga (Oktoba 2018)
MONUSCO/Michael Ali
Mfuko wa kusaidia manusura wa ukatili na unyanyasaji wa kingono umesaidia wanawake huko DR Congo kujifunza kilimo cha uyoga (Oktoba 2018)

Katika muktadha huu, kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake kunaweza kuonekana kama hakuwezi kufanikiwa, la hasha. Kupungua kwa kiasi kikubwa kwa ukatili dhidi ya wanawake kunaweza kufanikiwa kupitia vuguvugu la utetezi wa masuala ya wanawake na uchechemuzi unaounganishwa na kuratibiwa kimtambuka kupitia haki, afya, fedha na sekta nyingine nyingi.

Ushahidi wa hivi karibuni unadokeza kuwa harakati thabiti na huru za utetezi wa masuala ya wanawake ni muhimu katika kuchochcea mabadiliko.

Kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake ni jukumu la kila mtu. Ndio maana katika siku hizi 16, “onesha mshikamano wako na harakati za utetezi wa haki za wanawake na uchechemuzi duniani kote. Iwe ni mwanaharakati wa msimu au ndio kwanza unaanza, kuna njia 10 ambazo kwazo unaweza kuchangia katika kutokomeza vitendo hivyo,” inasema UN Women.

Njia 10 za kushiriki kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana

1. Paza sauti; Zungumza

Ukatili dhidi ya wanawake umetapakaa, lakini si kwamba hauwezi kuepukika, labda tunyamaze. Katika zama hizi za kuongezeka kwa harakati na vuguvugu za makundi ya utetezi wa haki za wanawake, ni muhimu kuliko wakati wowote ule kupaza sauti na kuzungumza.

Mila potofu zinazozingira ukatili wa kijinsia hupatia watendaji fursa ya kukwepa mkono wa sheria na kuzuia wanawake na wasichana kupata msaada wanaohitaji: Takwimu zinaonesha kuwa wanawake wanaosaka msaada baada ya kukumbwa na ukatili wa kijinsia ni chini ya asilimia 40 tu

Hebu waoneshe manusura na wanaharakati kuwa uko nao. Paza sauti na simulizi zao. Fungua fursa ya mazungumzo iwe ya uso kwa uso au mtandaoni.

2. Fahamu tatizo pamoja na dalili

Ukatili dhidi ya wanawake hujitokeza katika njia tofauti tofauti. Inaweza kuwa kimwili, kingono au kifikra. Inaweza kufanyika mbele za watu, faraghani au mtandaoni na kutekelezwa na mpenzi au mtu mwingine yoyote. Bila kujali unafanyika vipi, wapi na umetekelezwa nani au ni kwa sababu gani? Ukatili dhidi ya wanawake una madhara makubwa ya muda mfupi au muda mrefu kwa wasichana na wanawake na huzuia ushiriki wao kikamilifu kwenye jamii zao.

Bofya hapa kufahamu aina mbalimbali za ukatili.

Na kufahamu jinsi ya kumsaidia anayekumbwa na ukatili bofya hapa

3. Kemea unyanyasaji wa kijinsia

Kwa wanawake wengi, unyanyasaji wa kijinsia ni uzoefu wa kila siku. Iwe mtandaoni, mtaani, pahala pa kazi, kupuuzia tabia isiyo sahihi huendelea kukomaza au kushamirisha unyanyasaji wa kijinsia na kuonekana kuwa jambo la kawaida.

Manyanyaso yaliyozoeleka kama vile uonevu mtandaoni, mazungumzo ya kingono, kupiga mluzi, vituko au vichekesho vya kingono hufanya wanawake na wasichana wajione hawakaribishwi au hawajisikii kuweko kwenye maeneo fulani au wajione hawako salama. Vitendo hivyo vinasaidia kuimarisha vitengo ya ubaguzi wa kijinsia na huchochea kuimarika kwa utamaduni wa ukwepaji sheria ambao hatimaye madhara yake huathiri wanawake,

Weka mazingira salama mtandaoni na nje ya mtandao kwa kila mtu na hoji wana rika wenzako juu ya tabia zao na kemea yeyote yule anayevuka mipaka kwenye mazungumzo au saka usaidizi pindi unapohisi hauko salama.

4. Hoji mfumo dume

Mfume dume wenye sumu na uhachochea ukatili dhidi ya wanawake

Ushahidi unaonesha kuwa wanawake walio kwenye uhusiano na wanaume ambao tabia na imani zao zinabeba na kushinikiza ubabe wa kiume na ukosefu wa usawa wa kijinsia wako hatarini zaidi kukumbwa na ghasia kutoka kwa mpenzi.

Fikra za kitamaduni kuhusu ubabe wa kiume huchochea mienendo kama uonevu na udhibiti huku vikipuuza hisia za mtu, upendo, huruma na mambo mengine ambayo kitamaduni yanaambatana na masuala ya wanawake.

Tunaposhindwa kuhoji na kukemea imani na fikra hizi potofu, kila mtu anapata hasara. Hebu tafakari mawazo yako kuhusu mfumo dume na msimamo wako kuhusu wanawake na bonga bongo kuhusu taswira ya jinsia kwenye vyombo vya habari na tamaduni mbalimbali. Shikamana na wanaume na wavulana kwenye maisha yako kusongesha kujali na kuelezea mienendo mingine isiyopatia kipaumbele mfumo dume hatarishi.

UN
Wanafunzi wa shule ya ukunga huko El Fasher jimboni Darfur kaskazini nchini Sudan wakiandamana kupinga ukatili wa kijinsia
UN

5. Fadhili mashirika ya wanawake

Kuwekeza katika harakati za kusongesha wanawake kuna umuhimu mkubwa.

Ushahidi unaonesha kuwa harakati huru na thabiti kuhusu wanawake ni muhimu katika kuchochea mabadiliko ya kisera kuhusu ukatili wa kijinsia. Lakini kadri siku zinavyosonga mashirika ya wanawake ambayo ni muhimu katika kuleta mabadiliko yanazidi  kukosa ufadhili, yakienguliwa na kunyamazishwa kwenye mchakato wa kutoa maamuzi.

Kuongeza ufadhili wa muda mrefu kwa mashirika hay ani jawabu la msingi la kuzuia na kuchukua hatua kukabili ukatili dhidi ya wanawake.

Changia mashirika ya eneo lako yanayojengea uwezo wanawake, saidia manusura na songesha hatua na sera zinazolenga kuzuia ukatili wa kijinsia.

UN Women kwa upande wake hushirikiana na mashirika ya wanawake duniani kote kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na kusaka haki sawa kwa wanawake na wasichana. Unaweza kuchangia hapa.

6. Paza sauti kwa hatua na huduma bora

Huduma kwa wanawake na wasichana wanaokumbwa na ukatili zinaweza kuleta tofauti kubwa kati ya uhai na kifo.

Hii ina maana maeneo ya hifadhi, namba za simu za kutoa taarifa wakati wowote, ushauri nasaha na aina zozote za usaidizi ambao manusura wa ukatili wa kijinsia wanahitaji hata wakati wa majanga na dharura.

Kila mwaka, kampeni ya siku 16 ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake husaka hatua za pamoja za kimataifa kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.

Ungana nasi kaitka kutoa wito kwa serikali kuziba pengo la ufadhili na kushughulikia ukatili dhidi ya wanawake na wasichana na kuhakikisha huduma zinapatikana na zinkuweko wakati wowote.

Shiriki kwa kujitolea kwenye maeneo ya hifadhi ya manusura wanawake, changia nguo au vifaa, au pata mafunzo uwe mshauri nasaha kwenye makazi ya hifadhi ya wanawake manusura.

7. Saka takwimu zaidi

Harakati thabiti za kukabili ukatili wa kijinsia ni kutambua tatizo lenyewe. Takwimu sahihi ni muhimu katika kufanikisha hilo hasa katika kuzuia na kupatia manusura msaada sahihi.

Hata hivyo kupata takwimu sahihi zilizonyumbuliwa kijjinsia bado ni changamoto na pia hakupatiwi kipaumbele na serikali.

Ukatili wa kijinsia unavyoshamiri kutokana na janga la coronavirus">COVID-19, mabadiliko ya tabianchi na majanga mengine, pengo la takwimu zenye mnyumbuliko wa kijinsia limekuwa dhahiri zaidi kuliko wakati wowote.

Toa wito kwa serikali ziwewekeze kwenye ukusanyaji wa takwimu kuhusu ukatili wa kijinsia.

Wanawake wakihudhuria masomo ya kujifunza kusoma na kuandika huko Umm al Khairat nchiin Sudan
PBF Secretariat in Sudan
Wanawake wakihudhuria masomo ya kujifunza kusoma na kuandika huko Umm al Khairat nchiin Sudan

8. Chechemua ili kuweko na sheria thabiti

Ni miaka 21 sasa tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Kimataifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake duniani, CEDAW.

Dunia inahitaji mifumo thabiti zaidi ya ulinzi na kutokomeza ukatili, unyanyasaji, na vitisho na ubaguzi dhidi ya wanawake watetezi wa haki za binadamu na wachechemuzi na wanaharakati wa masuala ya wanawake.

Fahamu zaidi kuhusu sheria katika nchi yako kwa kubofya hapa.  Na wakati huo huo toa wito kwa serikali yako iimarisha mifumo ya kisheria, na saidia kupaza sauti na uelewa kuhusu mapengo ya kisheria yaliyoko.

Anzisha au unga mkono maandamano, saidia vikundi vya uchechemuzi, na jielimishe mwenyewe kuhusu misimamo ya wagombea wa kisiasa au wawakilishi kuhusu masuala ya wanawake.

9. Unga mkono uongozi wa wanawake

Wakatiwa janga la COVID-19, wanawake walienguliwa kwa kiasi kikubwa kwenye vikosi kazi vya kujikwamua baada ya janga la Corona. Pengo hilo linadhihirika katika hatua za serikali kwenye masuala ya kijinsia kama vile kuongezeka kwa ghasia majumbani.

Suala hilo ni vivyo hivyo kwenye hatua kwa tabianchi, ujenzi wa amani na mengine mengi ambako sauti zao hazisikiki.

Hali hii inasababisha vyombo vya maamuzi kusahau mapengo muhimu yaliyoko kwenye utungaji wa sera na ufadhili.

Uwakilishi wa wanawake kwenye vyombo vya kupitisha maamuzi ni muhimu sana na husaidia kuhakikisha mahitaji ya wanawake na wasichana yanakuwa kitovu cha hatua zozote wakati wa dharura au majanga, mikataba ya amani  na utungaji wa sera zozote.

Na wakati huo huo, viongozi wanawake wanakabiliwa na hatari ya ghasia; katika mabara Matano, asilimia 82 ya wanawake wabunge wameripoti kukumbwa na aina ya ghasia za kisaikolojia wakati wa awamu zao za ubunge.

Kwa sasa wito unazidi kutolewa kwa uwakilishi zaidi wa wanawake kwenye nafasi za uongozi. Saidia au unga mkono wagombea wanawake na mashirika au kampuni za wanawake. Au chukua jukumu wewe mwenyewe kwa kuwa kiongozi mwanamke unayependa kuona duniani,

10. Shikamana na harakati nyingine za kuinua wanawake

Umoja ni nguvu na mshikamano ni udhaifu.

Ukatili dhidi ya wanawake na wasichana una uhusiano na aina nyingine za vitendo vibaya na ukosefu wa haki, ikiwemo ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni, chuki dhidi ya wapenzi wa jinsia moja, umaskini na mabadiliko ya tabianchi,

Imarisha vita dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa kushirikiana na makundi mengine ya harakati za kijamii na kisiasa ili pia kujumuisha wanaharakati kwenye makundi hayo katika kundi lako.

Kwa pamoja, tunaweza kuzuia kurejeshwa nyuma kwa haki za wanawake na hatimaye kupaza sauti na matakwa ya harakati za utetezi wa masuala ya wanawake duniani kote na kisha ajenda ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ifanikiwe.