Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada kutoka FAO waleta matumaini kwa wakazi wa Hirshabelle nchini Somalia

Fadumo Ibrahim, mkulima huyu akipalilia shamba lake la mahindi huko Marka, Somalia mwezi tarehe 22 Novemba mwaka 2021.
©FAO/Arete/Abdulkadir Zubeyr.
Fadumo Ibrahim, mkulima huyu akipalilia shamba lake la mahindi huko Marka, Somalia mwezi tarehe 22 Novemba mwaka 2021.

Msaada kutoka FAO waleta matumaini kwa wakazi wa Hirshabelle nchini Somalia

Tabianchi na mazingira

Ukame wa zaidi ya miongo minne na mafuriko vimekuwa ‘mwiba’ kwa wananchi wa Somalia na hivyo kutishia uhakika wa kupata chakula halikadhalika mbinu za kujipatia kipato. Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO kwa msaada kutoka serikali ya Sweden imewezesha mradi wa kusaidia wakulima wadogo kwa kuwapatia pembejeo na msaada wa fedha na sasa kuna nafuu hasa kwenye jimbo la Hirshabelle nchini humo. 

Kabla ya mradi hali ilikuwa mbaya 

Mradi huo uko kwenye maeneo ya Johwar na Beledweyne na manufaa yameanza kuonekana huku wakulima wakilinganisha kabla na baada ya kupata usaidizi.  

Miongoni mwa wanufaika ni Farhiya Ali Diriye, mkulima huyu katika jimbo la Hirshabelle ambaye katika video ya FAO anasema, “maisha yetu yanategemea kilimo, sisi ni wakulima na tunalima mashambani!  

Akiwa kwenye shamba lake la mahindi, kwa kiasi fulani kuna mahindi yamestawi na mengine yamenyauka na Farhiya anasema“kuna wakati tunapata mavuno, tunashukuru Mungu na kuna wakati tunaambulia patupu.” 

Taswira kutoka juu katika video hii ya shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO inatufikisha kwenye makazi yake, nyumba zikiwa ni za makuti! Ingawa wakulima wadogo, ndio tegemeo la uhakika wa chakula Somalia, wakulima wa hapa Johwar, jimboni Hirshabelle wanakabiliwa na majanga lukuki, yakiwemo ukame na mafuriko. 

Lakini msaada wa kifedha kutoka serikali ya Sweden, umewezesha FAO kushirikiana na serikali kuu Somalia na zile za majimbo kuimarisha uhakika wa upatikanaji wa chakula pamoja na lishe kwa zaidi ya wakulima wadogo 7,500 na familia zao kupitia mradi maalum.  

Wanaushirika wanapatiwa fedha taslimu bila masharti 

Mradi huo unahusisha upelekaji wa fedha kupitia vyama 24 vya ushirika wa wakulima jimboni Hirshabelle ambako wakulima wanapatiwa fedha taslimu bila masharti yoyote, pembejeo za kilimo kama vile majembe, mbegu za mazao  yanayostahimili ukame pamoja nafaka na zaidi ya yote mafunzo ya jinsi ya kukabiliana na ukame. 

Yusuf Mayow Ali ni mdau wa FAO kupitia shirika la STS International na anasema “wamepatiwa mafunzo mengi kuhusu masoko, kuhifadhi mazao na kuzuia mazao kushambuliwa na wadudu waharibifu.” 

Sasa Farhiya anaonekana akiangalia mbuzi wake wapatao 12, na anasema, “ni fursa nzuri sana kwa jamii yetu. Sasa tumejikomboa kutoka kupoteza nafaka. FAO imetupatia mafunzo mengi yaliyotunufaisha. Zamani tulipanda tu mazao, lakini sasa kuna mengi tumejifunza kutoka kwenye mafunzo. Mfano jinsi ya kuhudumia na kupanda mahindi. Tumenufaika sana kutoka FAO.” 

Sasa ni tabasamu kutoka kwa wakulima 

Kwenye video hii ya FAO, wana ushirika wanaonekana na tabasamu linalotia moyo wakiwa na pembeejo zao walizopatiwa kupitia vyama vya ushirika. Pembejeo kama vile majembe, mbegu na mbolea. 

FAO inasema pembejeo hizo pamoja na mafunzo vinaongeza uwezo wa wakulima wadogo kuzalisha mazao. 

Na zaidi ya yote, uwekezaji wa kutosha kwenye kilimo kupitia vyama vya ushirika utasaidia kuimarisha uhakika wa upatikanaji wa chakula kwenye taifa hilo la pembe ya Afrika lililoshuhudia misimu mitano mfululizo ya kukosa mvua na hivyo basi kuongeza mnepo kwenye madhara dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. 

Video ya FAO inatamatikia maeneo ya mjini ikionesha harakati za watu za kujipatia kipato huku ikieleza uwekezaji wa kina kwenye kuinua vipato vya wakazi wa vijijini utapunguza hama hama ya watu wanaolazimika kukimbia makwao kutokana na ukame na kwenda kuishi katika kambi za wakimbizi wa ndani.