Wakazi wa Belet Weyne Somalia waanza kupata msaada wa chakula

Mji wa Belet Weyne kwenye eneo la Hiraan likiwa limezama kwenye maji ya mafuriko ya mto Shabelelle katika picha hii ya tarehe 30 Aprili mwaka 2018. Mji wa Belet Weyne hivi sasa unakabiliwa na mafuriko mabaya zaidi na watu 150,000 wamepoteza makazi.
UN Photo/Ilyas Ahmed)
Mji wa Belet Weyne kwenye eneo la Hiraan likiwa limezama kwenye maji ya mafuriko ya mto Shabelelle katika picha hii ya tarehe 30 Aprili mwaka 2018. Mji wa Belet Weyne hivi sasa unakabiliwa na mafuriko mabaya zaidi na watu 150,000 wamepoteza makazi.

Wakazi wa Belet Weyne Somalia waanza kupata msaada wa chakula

Msaada wa Kibinadamu

Umoja wa Mataifa umeunga mkono juhudi za Somalia za kusambaza misaada ya dharura kwa makumi ya maelfu ya wananchi walioathiriwa na mafuriko hususan kwenye wilaya ya Belet Weyne jimboni Hirshabelle. Grace Kaneiya na ripoti kamili.

Mafuriko katika jimbo la Hirshabelle yameleta tafrani kubwa, nyumba zikitwama na wakazi kushindwa kujipatia huduma muhimu ikiwemo chakula.

Tayari shirika la mpango wa chakula duniani, WFP na wadau wengine kwa msaada wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa masuala ya kibinadamu, OCHA wamesafirisha shehena za vyakula kukidhi mahitaji ya haraka ya lishe kwa familia zilizoathirika sambamba na kuwapatia maji safi na salama na huduma za afya.

Mkurugenzi wa WFP Somalia, Caesar Arroyo amesema kuwa wanashirikiana na serikali ya Somalia kusambaza misaada hiyo ikiwemo tani 260 za chakula na biskuti zenye virutubisho.

Halikadhalika amesema kuwa, "chakula hiki hakihitaji maandalizi na kinaweza kusaidia watoto, akina mama na yeyote yule anayehitaji mlo wa haraka. Kwa sasa tunaleta msaada zaidi ili tuweze kusaidia angalau kwa miezi miwili eneo hili la Belet Weyne na viunga vyake ambako kuna mafuriko na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.”

Katika wilaya ya Belet Weyne watu zaidi ya 270,000 wameathirika,  mashamba yameharibiwa pamoja na miundombinu .

Halimo Osman Abdi ni mmoja wao waliokimbia makwao na angalau amepata msaada na anasema, "nimepokea msaada wa chakula ikiwemo unga na mchele. Nina mgao wang una nashukuru Mungu.”

WFP imepanga kuendelea kusambaza msaada wa chakula kwa kaya 4,000 sawa na watu 24,000.

Mvua kubwa za msimu zimesababisha mafuriko kwenye  mto Juba na Shabelle  kwenye majimbo ya Hirshabelle, Jubaland na Kusini Magharibi.

Wakati wa ziara yake huko Belet Weyne, Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed 'Farmaajo' ameelezea wasiwasi wake juu ya kiwango cha madhara yaliyosababishwa na mafuriko na kile kinachohitajika kukwamua maeneo husika.

Amesema kwamba wanafahamu mafuriko yam waka jana yalivunja rekodi lakini pengine haya ya mwaka huu yatakuwa na madhara makubwa zaidi.