Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF imeshtushwa na vifo vya watu 8 wakiwemo watoto 6 kwa mlipuko wa bomu Somalia

Mwonekano wa Barawe, makaazi ya zamani ya Al-Shabaab katika eneo la Shabelle nchini Somalia. (maktaba)
UN Photo/Ilyas Ahmed
Mwonekano wa Barawe, makaazi ya zamani ya Al-Shabaab katika eneo la Shabelle nchini Somalia. (maktaba)

UNICEF imeshtushwa na vifo vya watu 8 wakiwemo watoto 6 kwa mlipuko wa bomu Somalia

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudmia watoto UNICEF limesema limesikitishwa sana na ripoti kwamba watoto sita ni miongoni mwa wahanga katika mlipuko wa bomu la kutegwa ardhini lililoua watu 8 siku ya Jumapili, karibu na mji wa Bulaburde, katika jimbo la Hirshabelle nchini Somalia. 

Katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Moghadishu Wafaa Saeed mwakilishi wa UNICEF nchini Somalia alesema “Watoto hao walikuwa sehemu ya familia mbili zilizokuwa zikisafiri kwa pikipiki ya miguu mitatu maarufu kama tuk-tuk ilipogonga bomu hilo la kutegwa ardhini na kulipuka. Kufiwa na wapendwa wao katika hali hiyo mbaya ni jambo la kuhuzunisha sana. Tunatoa pole kwa familia na tunawatakia majeruhi ahueni ya haraka.”

Bi. Saeed ameongeza kuwa "Tukio hili la kusikitisha linakuja takribani mwezi mmoja baada ya watoto 22 kuuawa na bomu ambalo haikulipuka katika eneo la Lower Shabelle nchini Somalia, kwa mara nyingine tena likithibitisha hatari ambazo watoto nchini Somalia wanakabiliana nazo wanapoendelea na maisha yao ya kila siku.” 

Hatari inayowakabili watoto Somalia

Baada ya miongo kadhaa ya vita, Somalia imekuwa mojawapo ya maeneo hatari zaidi duniani kwa watoto, kulingana na Ripoti ya hivi karibuni ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu “Watoto na Migogoro ya Kivita”. 

Mwaka 2022, zaidi ya visa 3,000 vya ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto vilithibitishwa, na watoto 200 waliuawa na wengine karibu 600 kulemazwa.

Mwakilishi huyo wa UNICEF amesisitiza kuwa "Pande zote katika mzozo nchini Somalia zina wajibu wa kushughulikia sheria kwa uangalifu, ili kuepuka kuchafua maeneo yenye watu wengi na ya kupita na mabaki yasilaha za vita, kusafisha mabomu yaliyopo na vifaa ambavyo havikulipuka, na kuongeza elimu ya hatari ya mabomu miongoni mwa watoto na jamii.”

Ameongeza kuwa "Usalama wa watoto lazima uwe jambo la msingi katika hali zote na hakuna juhudi zinazopaswa kuepukwa katika kudumisha haki zao za mazingira salama na yenye ulinzi.”

Amehitimisha tarifa yake kwa kusema kwamba UNICEF inafanya kazi na serikali na washirika wengine kutoa huduma na msaada kwa watoto waathiriwa wa mabomu ya kutegwa ardhini nchini Somalia na watendaji wa mashirika ya kiraia kutoa elimu ya hatari na ufahamu kuhusu milipuko kwa watoto na walezi wao ili kujilinda vyema.