Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pembe ya Afrika: UNFPA yazindua ombi la dola milioni 113 kwa wanawake na wasichana walioathiriwa na ukame

Amira, mwenye umri wa miaka 12 anafanya kazi za shule akiwa kwenye bweni la kituo cha kulinda watoto cha Garisa wasichana nchini Somalia
© UNICEF/UN0657272/Odhiambo
Amira, mwenye umri wa miaka 12 anafanya kazi za shule akiwa kwenye bweni la kituo cha kulinda watoto cha Garisa wasichana nchini Somalia

Pembe ya Afrika: UNFPA yazindua ombi la dola milioni 113 kwa wanawake na wasichana walioathiriwa na ukame

Afya

Ukame ambao haujawahi kutokea katika Pembe ya Afrika unaathiri jamii nzima, lakini ni wanawake na wasichana ambao wanalipa “gharama kubwa isiyokubalika,” limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani na masuala ya afya ya uzazi UNFPA hii leo wakati likizindua ombi la dola milioni 113.7 ili kukidhi mahitaji yao.

Ufadhili huo utatumika kuongeza huduma za afya ya uzazi na ulinzi zinazookoa maisha, ikiwa ni pamoja na kuanzisha kliniki zinazoweza kuhama kutoka eneo kwenda nytingine na maabara zitakazowekwa katika maeneo ya kambi za wakimbizi wa ndani.

Kwa ujumla, zaidi ya watu milioni 36 katika nchi za Ethiopia, Somalia na Kenya wanahitaji msaada wa kibinadamu kwa sababu ya ukame unaowakabili.

Kuzilinda huduma muhimu

Migogoro, mashambulizi ya nzige na athari zinazoendelea za janga la coronavirus">COVID-19 zinazidisha athari zake, na kusukuma mamilioni kwenye ukingo wa njaa.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dk. Natalia Kanem, anasema hali ya uhakika wa chakula ikiendelea kuzorota, wanawake na wasichana wanakabiliwa na njaa na vitisho vingine vikubwa kwa afya, haki na usalama wao, alisema

“Tunahitaji kuchukua hatua sasa kuokoa maelfu ya maisha na kuwapa wanawake na wasichana msaada muhimu wanaohitaji haraka na nafasi ya kujenga maisha bora ya baadaye,” alisema Dkt.Kanem.

Kulazimishwa kutafuta chakula

Mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na washirika wao walieleza kuwa ukame unaowakumba sasa wananchi wa pembe ya Afrika ndio mbaya zaidi katika eneo hilo katika miongo minne na unatazamiwa kuendelea hadi 2023.

Wilaya mbili nchini Somalia ziko katika hatari ya kukumbwa na baa la njaa.

Kwa mujibu wa UNFPA kuna takriban watu milioni 1.7 ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao kwenda kutafuta chakula, maji na huduma za msingi. Wengi wao ni akina mama, ambao mara nyingi huishia kutembea kwa siku au hata wiki.

Ukame mkali Pembe ya Afrika, Ethiopia, Somalia na Kenya unaathiri mamilioni ya watu
UNICEF/Raphael Pouget
Ukame mkali Pembe ya Afrika, Ethiopia, Somalia na Kenya unaathiri mamilioni ya watu

Anaishi hatarini

Safari hizi hatari kwa miguu huongeza uwezekano wa wanawake kudhulumiwa kingono, unyonyaji na unyanyasaji. UNFPA imeeleza tayari ripoti za unyanyasaji wa kijinsia zinaonekan kuongezeka.

Huku familia zikikabiliwa na maamuzi magumu ya kuishi, ripoti za wasichana kuacha shule, ukeketaji na ndoa za utotoni zimeenea zaidi.

Wasiwasi kwa wajawazito

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema upatikanaji wa huduma za kimsingi za afya, ikiwa ni pamoja na uzazi wa mpango na afya ya uzazi, umetatizwa kwakiasi kukubwa.

Matokeo yanaweza kuwa mabaya, ikiwa ni pamoja na zaidi ya wajawazito 892,000 ambao watajifungua katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.

Utapiamlo miongoni mwa wajawazito na wanaonyonyesha ni wa hali ya juu, na hivyo kuongeza hatari yao ya kupata matatizo makubwa ya ujauzito, kama si kufa, na kuna ripoti za kusikitisha za akina mama dhaifu sana ambao wanashindwa hata kulisha watoto wao.

Tofauti na maeneo mengine ya Afrika, wanawake ndio idadi kubwa ya wahamiaji kwenye Pembe ya Afrika
IOM/Amanda Nero
Tofauti na maeneo mengine ya Afrika, wanawake ndio idadi kubwa ya wahamiaji kwenye Pembe ya Afrika

Kuongeza msaada

Ombi hili la la dola milioni 113.7 linalenga kupatia ufumbuzi mahitaji yanayoongezeka.

Mbali na kuanzisha kliniki za afya zinazohamishika na zisizohamishika, UNFPA itapeleka wakunga waliopatiwa mafunzo kwenye vituo vilivyo katika maeneo yenye mahitaji makubwa zaidi.

Nchini Somalia, wakunga watakuwa rasilimali muhimu katika kutoa huduma jumuishi za afya ya uzazi na ulinzi, shirika hilo lilisema.

Mipango mingine ni pamoja na kuongeza ufikiaji wa jamii kwa ajili ya utoaji wa huduma za afya ya uzazi, pamoja na kuimarisha mifumo ya rufaa ili kuhakikisha wajawazito wanaopatwa na matatizo wanaweza kupata huduma ya dharura ya uzazi.

Maeneo salama kwa walionusurika

UNFPA pia inamipango ya kupanua maeneo salama, malazi, kituo kimoja kwa ajili ya kushughulikia masuala mbalimbali pamoja na mawasiliano ya simu ili wanawake na wasichana walionusurika na unyanyasaji wa kijinsia wapate huduma za matibabu na usaidizi wa kisaikolojia na kijamii.

Watoa huduma za afya pia watapatiwa mafunzo ya kutoa huduma jumuishi za afya ya uzazi na ulinzi, ikijumuisha usimamizi wa kimatibabu wa waliobakwa.

Mipango zaidi inahusisha kusambaza dawa na vifaa vya afya ya uzazi vinavyookoa maisha na vituo vya afya na hospitali, na kutoa vifaa vya kimsingi vya usafi, ikiwa ni pamoja na pedi za usafi, kwa wale wanaohitaji.