Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mustakbali wetu umeporwa ni wakati wa kushughulikia hasara na gharama:Vijana COP27

Shule anayosoma Protiva mjini Sylhet imefungwa sababu ya mafuriko makubwa Kaskazini mwa Bangladesh na nyumba yake pia imefurika
© UNICEF/Parvez Ahmad Rony
Shule anayosoma Protiva mjini Sylhet imefungwa sababu ya mafuriko makubwa Kaskazini mwa Bangladesh na nyumba yake pia imefurika

Mustakbali wetu umeporwa ni wakati wa kushughulikia hasara na gharama:Vijana COP27

Tabianchi na mazingira

Wakiwa wamebeba mabango, vibao vyenye ujumbe, spika, na hasa kwa wakitoa ujumbe wenye kugusa moyo unaoungwa mkono na ukweli wa kisayansi na kiuchumi, vijana leo wametawala kumbi za COP27 wakiwataka viongozi wajadili jinsi ya kushughulikia suala la hasara na uharibifu utokanao na mabadiliko ya tabianchi.

"Kuna majanga ya mabadiliko ya tabianchi na uharibifu, na nchi yangu inaishia kukopa fedha kutoka kwa shirika la fedha la Kimataifa na Benki ya Dunia ili kukabiliana na athari . Nchi zetu haziwezi kujiendeleza kwa sababu ya gharama za mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi," amesema mwanaharakati kijana wa Afrika katika moja ya maandamano mengi yaliyofanyika leo katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Tonino Lamborghini.

“Mustakabali wetu unaporwa kutoka kwetu! Huu ni udhalimu!” Vijana-COP27.

Hasara na uharibifu ni gharama ambazo zinazikumba nchi ambazo zimechangia kwa kiasi kidogo zaidi katika mabadiliko ya tabianchi lakini zinabeba mzigo mkubwa wa athari zake, kama vile kupanda kwa kina cha bahari na matukio ya hali mbaya ya hewa yanayozidi kutokea mara kwa mara.

Wanaharakati vijana wameandamana wakidai viongozi kushughulikia hasara yao na jukumu la uharibifu.

Wanaharakati vijana wakiandamana kudai viongozi kushughulikia hasara na uharibifu kwa uwajibikaji
UN News/Laura Quinones
Wanaharakati vijana wakiandamana kudai viongozi kushughulikia hasara na uharibifu kwa uwajibikaji

Hivi sasa, nchi zinazoendelea kama vile Pakistan, Bangladesh na idadi kubwa ya mataifa ya Afrika, yanalazimika kulipa gharama kubwa sana ili kujikwamua kutokana na majanga ya tabianchi, na vijana wanaamini kuwa ni wakati wa wachafuzi wa mazingira kulipa madeni yao ya kiikolojia.

"Hili ni suala ambalo limewekwa kando COP baada ya COP. Ukweli kwamba tuko katika nchi ya Kiafrika mwaka huu ni muhimu sana. Ni ukweli wa kisayansi kwamba nchi zilizo na rasilimali chache zaidi za kiuchumi na zisizo na jukumu lolote la utoaji wa hewa chafuzi ndizo zinazoishia kuteseka zaidi. Ni kuhusu fidia na haki ya kijamii," Bruno Rodriguez, mwanaharakati wa vijana kutoka Argentina ameiambia UN News.

Wito kutoka kwa vijana uko bayana “wanataka kuanzishwa kwa kituo cha kifedha cha hasara na uharibifu ambacho kinaweza kutoa fedha za ziada na zinazoweza kupatikana kwa urahisi ili kusaidia mataifa yanayoendelea kujenga mnepo na kuzuia athari zisizoweza kurekebishwa za mabadiliko ya maisha kwa vijana."

“Hatutaki mikopo, hatutaki madeni zaidi. Lipa sasa kwa hasara na uharibifu,” ulikuwa ujumbe wa mwanaharakati kutoka Ufilipino.

Jumuiya ya wanasayansi inaafiki

Mvulana akiwa ameketi kwenye kifusi cha nyumba yao ambayo imebomolewa na kimbunga Iota huko Bilwi, Nicaragua
© UNICEF/Inti Ocon/AFP-Services
Mvulana akiwa ameketi kwenye kifusi cha nyumba yao ambayo imebomolewa na kimbunga Iota huko Bilwi, Nicaragua

Ripoti ya kila mwaka ya 10 ya kisayansi kuhusu mabadiliko ya tabianchi ambayo, kama jina lake linavyoonyesha, inatoa muhtasari mfupi wa matokeo muhimu zaidi juu ya utafiti unaohusiana na mabadiliko ya tabianchi ili kufahamisha mazungumzo ya COP, pia imeonyesha umuhimu wa kushughulikia hasara na uharibifu, na kuiita "muhimu wa haraka wa sayari".

Wakati wa kutolewa kwa ripoti hiyo leo ambayo imeambatana na 'Siku ya vijana na sayansi katika mkutano wa COP27, wanasayansi wamesisitiza kuwa hasara na uharibifu tayari unatokea na utaongezeka kwa kiasi kikubwa kulingana na mifano ya sasa ya makadirio.

"Ingawa uharibifu na hasara nyingi zinaweza kuhesabiwa kwa njia za kifedha, pia kuna uharibifu hasara zisizo za kiuchumi ambazo zinahitaji kueleweka vizuri na kuhesabiwa," waandishi wa ripoti hiyo wameonya, wakitaka hatua za haraka zilizoratibiwa za sera ya kimataifa kuhusu jambo hili.”

Taarifa, zilizokusanywa na mpango wa utafiti wa mabadiliko ya tabianchi na kuungwa mkono na ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na mabadiliko ya tabianchi (UNFCCC), pia inaangazia kwamba mengi ya matokeo haya hayawezi kuepukwa kwa hatua za kukabiliana na hali hiyo na kwamba kuchukua hatua haraka kupunguza hewa chafuzi ni chaguo bora zaidi.

"Ripoti inasema kwamba uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hauna kikomo, na hilo halitazuia hasara na uharibifu wote ambao tunaweza kuona sasa. Napongeza pande zote kwa kujikita katikahasara katika ajenda ya COP27," amesema mkuu wa UNFCCC. Simon Steel.

Hata hivyo, amesema, kukabiliana na hasara na uharibifu hairuhusu nchi kuachana na masuala muhimu ya uzalishaji wao wa hewa chafuzi.

"Hatua za kujenga mnepo haziwezi kuchukua nafasi ya hatua kabambe za kupunguza uzalishaji", amesisitiza.

Barua zilizoandikwa na watoto na vijana kama zinavyoonekana kwenye banda lao maalum kwenye mkutano wa COP27
UN News/Laura Quinones
Barua zilizoandikwa na watoto na vijana kama zinavyoonekana kwenye banda lao maalum kwenye mkutano wa COP27

Kwa waandishi wa ripoti hiyo, ukweli kwamba makumi ya maelfu ya watu wanakufa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi hivi sasa, unahitaji kuwa kiini cha mazungumzo.

Pia wameangazia kuwa zaidi ya watu bilioni tatu watakaa maeneo hatarishi, maeneo yenye uwezekano mkubwa wa kuathiriwa vibaya na hatari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi ifikapo 2050, mara mbili ya ilivyo leo.

Baadhi ya maarifa mengine katika ripoti hiyo ni pamoja na maonyo kwamba uhamaji utokanao na mabadiliko ya tabianchi, hatari za kiafya, na masuala ya usalama wa kitaifa yanaongezeka kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi.

Vijana washika usukani

Katika siku yao, vijana wakubwa, barubaru na watoto katika mkutano wa COP27 wameshiriki katika kushika hatamu kwenye matukio tofauti na wameonekana na kusikika  karibu kila kona ya kituo cha mkutano.

Wamejieleza si kwa kupinga tu, bali pia kwa muziki, ngoma, mavazi ya rangi na michoro ya ukutani yenye ujumbe kwa viongozi wa dunia.

Wimbo mwingine uliotawala leo ni "wafukuze wachafuzi wa mazingira" huku mashirika matatu yasiyo ya kiserikali yakilaani kwamba katika orodha ya washiriki waliosajiliwa ambayo sasa ni zaidi ya 45,000 kulingana na UNFCCC kuna zaidi ya washawishi 600 wa mafuta, ikiwa ni ongezeko la asilimia 25 ikilinganishwa na mwaka jana.

"Ushawishi wa watetezi wa mafuta ya kisukuku ni mkubwa kuliko nchi na jumuiya zilizo mstari wa mbele. Wajumbe kutoka nchi za Kiafrika na jumuiya za kiasili wamepungukiwa na wawakilishi wa maslahi ya kampuni,” kundi la waandamanaji kutoka shirika la Kick Big Polluters Out walipiga kelele katika jukwaa kuu la mkutano.

Balozi Wael Aboulgmagd, mwakilishi maalum wa Urais wa Misri wa COP27, amesema wakati wa mkutano na waandishi wa habari kwamba ingawa hakuweza kujua kama washiriki hawa walikuwa washawishi au wanachama tu au vyombo fulani, kuna tasnia nyingi zinazochangia uzalishaji, kama vile makampuni ya saruji na mbolea. Lakini hawakuwa wakishiriki katika mazungumzo hayo, amefafanua.

Amesema alitarajia kwamba wakati wa siku ya kujadili utoaji hewa ukaa, ambayo itakuwa Ijumaa, wengi wao wataonyesha jinsi wanavyosonga mbele katika kupunguza uzalishaji wao.

Kuhusu mazungumzo ya jumla, Bwana. Aboulgmagd amesema kwamba sasa kuna rasimu ya kwanza ya maandishi ya uamuzi wa mpango  kazi wa kupunguza hewa ukaa ambao unaonyesha maendeleo mazuri sana, na kwamba Jumamosi asubuhi, wajumbe wataanza kutoa michango kwa hati ya matokeo ya COP27.