Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Urejeshaji wa miamba ya matumbawe nchini Colombia waanza kuzaa matunda

Wanabaiolojia Maria Fernanda Maya na Mariana Gnecco kutoka shirika la kiraia la Blue Indigo wakikagua afya ya matumbawe kwenye kisiwa cha San Andrés nchini Colombia
Blue Indigo
Wanabaiolojia Maria Fernanda Maya na Mariana Gnecco kutoka shirika la kiraia la Blue Indigo wakikagua afya ya matumbawe kwenye kisiwa cha San Andrés nchini Colombia

Urejeshaji wa miamba ya matumbawe nchini Colombia waanza kuzaa matunda

Tabianchi na mazingira

Shughuli za utalii, uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi zimechochea kuleta wasiwasi kwa wananchi wa kisiwa cha San Andres nchini Colombia kutokana na matumbawe waliyokuwa wanategemea kuvutia watalii kuanza kuharibika na samaki wa asili kuanza kupotea ambao ni chanzo cha mapato cha wanajamii.

Soundcloud

Shirika la Blue Indigo linaloongozwa na wanawake wanasayansi wa kisiwani humo wamedhamiria kutumia taaluma zao kuwaleta pamoja wanajamii na watalii katika kuhakikisha wanarejesha mifumo asilia ya miamba ya matumbawe huku wakiendeleza utalii endelevu na wananchi kuendelea na uvuvi ili kujipatia kipato.

Kisiwa maarufu kwa wapiga mbizi duniani

San Andrés ni kisiwa kizuri cha kuvutia nchini Colombia, maarufu kutokana na kuwa na mandhari nzuri ya ikolojia ya baharini yenye maji safi na yanayoonsha vizuri ikolojia ya bahari hivyo kuwa kivutio kikubwa kwa wapiga mbizi kutoka kila kona ya dunia. 

Kwa wastani kisiwa hicho chenye jumla ya wakazi 80,000 ambao wanajulikana kuwa wanajamii wa Raizal hupokea watalii zaidi ya milioni moja kila mwaka ambao pamoja na kuwaingizia wananchi na serikali fedha lakini mahitaji makubwa ya watalii yamegeuka zahma kwani kila uchao rasilimali asilia ya matumbawe imezidi kuharibika.

Mariana Genecco mwana biolojia wa Bahari na Mratibu wa masuala ya Kisayansi wa shirika la Blue Indigo amesema “tunachofanya ni kujaribu kurejesha baadhi ya mifumo ya ikolojia ambayo ni muhimu zaidi Duniani. Naona wakati ujao kutakuwa na matatizo. Tunaogelea dhidi ya mkondo wa maji

Kauli yake inaungwa mkono na Camilo Leche mwanajamii mvuvi anayeeleza kuwa hapo awali mambo yalikuwa mazuri “Kulikuwa na matumbawe makubwa, mazuri na kulikuwa na samaki wengi wakipatikana karibu. Na tulikuwa tunaweza kupiga mbizi na kupata kamba.”

Neema imeingia doa

Utalii wa kiwango cha juu, uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi yamesababisha wasiwasi kwa wananchi hawa kutokana na kupungua kwa matumbawe hai.

Mvuvi Camilo amesema Tunajua kwamba ikiwa hakuna matumbawe, hakuna samaki. Na ikiwa hakuna samaki, siwezi tena kuihudumia familia yangu kwa sababu matumbawe ndio yanayowavutia samaki.”

Toka enzi na enzi wanajamii ya raizal waliweza kuishi vyema na kuendeleza kupiga mbizi pamoja uvuvi bila ya kuharibu mazingira na wamekuwa wakitegemea bahari hiyo kwa ajili ya kuendesha maisha yao.

Mwanasayansi Mariana amesema kwa tathmini waliyofanya “Mifumo ya ikolojia imefika mahali ambapo inahitaji msaada. Kwa hivyo ikiwa mashirika pamoja na wananchi ambao ni mashujaa, hawatachukua hatua, matumbawe yataendelea kuharibika mpaka yatashindwa kabisa kufanyi kazi tena.”

Nguvu ya pamoja

Mwanabailojia Maria Fernanda Maya akisafisha kamba iliyoshikilia kitalu cha matumbawe.
Blue Indigo
Mwanabailojia Maria Fernanda Maya akisafisha kamba iliyoshikilia kitalu cha matumbawe.

Wanajamii wa San Andrés kwa pamoja wameamua kurejesha mifumo yao ya ikolokia ambayo Wavuvi, wanabiolojia wa baharí pamoja na wapiga mbizi wameunganisha nguvu ili kurejesha miamba ya matumbawe huku wakitoa elimu kwa jamii ambayo haikuwa ikifahamu athari zinazotokea kama anavyoekeza Camillo “Nilifikiri kwamba, matumbawe hayo yalikuwa yanazeeka na kupata mvi. Sikujua ni kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi na kila kitu kinachotokea duniani.”

Maria Fernanda Maya ni mhifadhi wa Matumbawe na amesema Tunafanya kazi kwakutumia aina mbalimbali za samaki asilia wa eneo hili ambao husaidia miamba kurejea yenyewe katika hali ya awali na zaidi ya yote kurejesha eneo hili kuvutia kiuchumi kwa kuwa na wale samaki muhimu.”

Shughuli hiyo ya utunzaji mazingira imezaa matunda na matumbawe yameanza kurejea pamoja na mandhari ya kuvutia ya eneo hilo.    

Wakati watu wanakuja ili kuona mradi wetu, wao huvutiwa zaidi na kuuliza “Matumbawe yangu tuliyopanda kwenye mwamba, yanaendeleaje?” Kwa hivyo tunaona kwamba kadri unavyowahusisha watu zaidi kushirikia katika tutunzaji wa matumbawe, ndivyo inavyokuwa rahisi kwao kufahamu tatizo.”

Ama hakika shughuli hizi zinazofanywa na Blue Indigo zinatoa maana halisi kwa Muongo wa Umoja wa Mataifa wakurejesha ya mifumo ikolojia.

Jamii ya Raizal inashiirki ipasavyo katika juhudi za kurejesha matumbawe. Pichani wanaume wawili wakijiandaa kutumbukiza baharini vitalu vya matumbawe.
Blue Indigo
Jamii ya Raizal inashiirki ipasavyo katika juhudi za kurejesha matumbawe. Pichani wanaume wawili wakijiandaa kutumbukiza baharini vitalu vya matumbawe.

Mariana Genecco mwanasayansi wa Blue Indigo amesema “Tunachohitaji ni mfumo wa ikolojia unaofanya kazi. Kwa hivyo tunajaribu angalau kuisaidia, ili iweze kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kwa sababu mfumo wa ikolojia utabadilika hilo tunafahamu lazima litokee. Lakini angalau inaweza kubadilika kwa njia ambayo haiendi kufa kabisa.’

Na sasa wavuvi kama Camilo Leche wana matumaini na chanzo chao cha mapato “Ikiwa hakuna matumbawe, nikama karibu hakuna maisha na bila maisha, sisi sote tunapoteza.”