Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR: Viongozi wa dunia msisahau waliokimbia makazi yao katika COP27

Wakimbizi wa ndani katika eneo la Bozoum baada ya kukimbia ghasia kutoka vikundi vilivyojihami nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.
© UNICEF/Tchameni Zigoto Tchay
Wakimbizi wa ndani katika eneo la Bozoum baada ya kukimbia ghasia kutoka vikundi vilivyojihami nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

UNHCR: Viongozi wa dunia msisahau waliokimbia makazi yao katika COP27

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamishna mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Filippo Grandi amewataka viongozi wa kimataifa kupunguza madhara makubwa zaidi ya kibinadamu ya athari za mabadiliko ya tabianchi na kuepusha hali mbaya ya baadaye kwa mamilioni ya watu waliokimbia makazi yao.

Taarifa iliyotolewa na shirika hilo hii leo kutoka Geneva Uswisi imemnukuu Kamishna Grandi akisema kuwa “COP27 lazima iziandae nchi na wanajamii kuwa mstari wa mbele wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na hali mbaya ya hewa ili kupunguza athari zake. Hatuwezi kuwaacha mamilioni ya watu waliokimbia makazi yao na wenyeji wao kukabiliana na matokeo ya mabadiliko ya tabianchi pekeyao.”

Mishtuko inayosababishwa na tabianchi ikijumlishwa na mizozo ya mabigano, uhaba mkubwa wa chakula, kupanda kwa bei ya bidhaa, na athari zinazoendelea za janga la COVID-19 vimeathiri watu kote ulimwenguni, lakini wale ambao wanahusika kidogo na kusababisha na shida ya mabadiliko ya tabianchi na ambao hawawezi kuzoea mishtuko yake ndio wanaoathirika zaidi.

COP27 iwasikilize na kuwasaidia waathirika wa mabadiliko ya tabianchi

UNHCR imesema zaidi ya asilimia 70 ya wakimbizi duniani na watu waliokimbia makazi yao wanatoka katika nchi zilizoathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi zikiwemo Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, Syria na Yemen. Wananchi wa nchi hizi wana mchango mkubwa katika majadiliano kuhusu mzozo wa mabadiliko ya tabianchi lakini mara nyingi hutengwa.

Hatua za ujasiri pekee na uimarishaji mkubwa wa ufadhili wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kukabiliana na hali hiyo zinaweza kupunguza matokeo ya sasa na ya baadaye ya uhitaji wa kibinadamu ya mzozo wa hali mbaya ya hewa kwa watu waliohamishwa na jamii zinazowakaribisha.

Uwekezaji lazima uwe shirikishi, ujumuishe na utafute suluhu kwa walio hatarini zaidi. Viongozi wa ulimwengu lazima wategemee hatua ya mabadiliko, ya kudumu, na jumuishi ambayo inahusisha wanajamii husika, serikali, na washirika ambao tayari wanapambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Katika baadhi ya mazingira, marekebisho hayatatosha na ufadhili wa ziada utahitajika kwa hasara na uharibifu usioweza kuepukika, mfano mzuri ambao unalazimishwa watu kuyakimbia makazi yao. Wasiwasi na masuluhisho ya watu waliohamishwa makazi yao lazima yapewe nafasi sio tu katika majadiliano kama katika COP 27, lakini pia lazima yapate usaidizi zaidi.” Amesema Grandi.

Nchi zinaathirika na wananchi wanakimbia makazi yao

 Wakimbizi wa Sudan kutoka jimbo la Blue Nile, wanaoishi katika kambi ya Doro katika jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini
Photo UNHCR/V. Tan
Wakimbizi wa Sudan kutoka jimbo la Blue Nile, wanaoishi katika kambi ya Doro katika jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini

Mkutano huu wa 27 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC, COP27 unafanyika wakati ambapo dunia inashuhudia majanga ya hali ya hewa kuanzia kwenye mafuriko ya kihistoria nchini Pakistan hadi ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea kwa miongo kadhaa katika Pembe ya Afrika.

Nchini Somalia, karibu watu milioni moja wamekimbia makazi yao kutokana na ukame na tishio la njaa. Vimbunga vikali nchini Msumbiji vimeathiri makumi ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao hapo awali kutokana na ghasia.

Sudan Kusini na Sudan zinapambana na mafuriko ambayo yameweka rekodi kwa mwaka wa nne mfululizo. Zaidi ya watu milioni 3.4 waliokimbia makazi yao na wenyeji wao wanakabiliwa na matokeo ya mafuriko mabaya ya hivi majuzi huko Nigeria, Chad, Cameroon, na nchi za Sahel ya Kati za Niger, Burkina Faso na Mali - eneo ambalo tayari linakabiliwa na moja ya migogoro mbaya zaidi ya watu kuhama makazi.

Katika Kaskazini ya Mbali nchini Cameroon, vurugu kati ya jumuiya zimezuka kati ya wafugaji, wavuvi na wakulima kutokana na kupungua kwa rasilimali za maji huku Ziwa Chad na vijito vyake vikikauka kutokana na ukame. Zaidi ya watu 100 waliuawa au kujeruhiwa mwishoni mwa mwaka jana, na makumi ya maelfu walikimbia makazi yao.

Wakati huohuo, ukame katika “Ukanda MKavu” wa Amerika ya Kati umewalazimu wakulima kukimbilia miji ya karibu ambako wako hatarini kwa machafuko yanayofanywa na magenge ya mitaani. Na katika maeneo mengine ya eneo kama vile Honduras, mabadiliko ya tabianchi ni sababu moja zaidi inayosababisha watu kukimbia makazi yao huku vimbunga vikiwa na nguvu zaidi na vikitokea mara kwa mara.

UNHCR yatuma wawakilishi  COP27

Wakibeba jukumu kubwa la kusaidia wakimbizi duniani UNHCR itawakilishwa katika COP27 na Andrew Harper, Mshauri Maalumu wa UNHCR kuhusu Hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na Balozi wa hiyari wa UNHCR Emtithal (Emi) Mahmoud, ambaye ni mshairi bingwa wa dunia na mkimbizi wa zamani wa Sudan ambaye familia yake inaendelea kuathirika pakubwa na mgogoro wa badiliko ya tabianchi.

Wote hawa wanashiriki katika COP27 kuelezea jinsi mzozo wa tabianchi unavyosababisha watu kuhama na kufanya maisha kuwa magumu kwa wakimbizi na watu ambao tayari wameondolewa majumbani mwao.

Pia watakuwa wakiwakumbusha viongozi wa kimataifa kwamba hatua za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinahitajika sasa, kwakuwa wale wanaosababisha kidogo athari hizo ndio wanaoteseka zaidi.