COP27 ni kumbusho kwamba suluhu ya mabadiliko ya tabianchi iko mikononi mwetu:Guterres

Leah Namugerwa, mwanaharakati wa tabianchi kutoka Uganda akiwa COP27
UNIC Tokyo/Momoko Sato
Leah Namugerwa, mwanaharakati wa tabianchi kutoka Uganda akiwa COP27

COP27 ni kumbusho kwamba suluhu ya mabadiliko ya tabianchi iko mikononi mwetu:Guterres

Tabianchi na mazingira

Mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP27 ukiingia siku ya pili hii leo huko Sharm el-Sheikh nchini Misri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewakumbusha viongozi wa dunia na wote wanaohudhuria mkutano huo kwamba suluhu ya changamoto ya mabadikio ya tabianchi iko mikononi mwao na wakati wa kuchukua hatua ni sasa kwani hakuna tena muda wa kusubiri.

Akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha viongozi wa ngazi ya juu cha utekelezaji kwenye mkutano huo Antonio Guterres amesema katika siku chache zijao idadi ya watu duniani itafikia bilioni 8 idadi ambayo inainaupa maana zaidi mkutano huu wa COP27 hasa katika kuchukua hatua zinazohitajika kuepuka zahma ya mabadiliko ya tabianchi 

“Mkutano huu wa mabadiliko ya tabianchi ni kumbusho kwamba jawabu liko mikononi mwetu na saa zinayoyoma tuko katika vita vya kufa na kupona na tunashindwa vita hiyo, gesi ya viwanda inazidi kuongezeka, kiwango cha joto duniani kimefurutu ada na kinaendelea kuongezeka , dunia inaelekea mwisho ambao utafanya mgogoro wa tabianchi usiweze kurekebishwa. Tuko kwenye barabara kuu ya kuelekea kuzimu kwa mabadiliko ya tabianchi huku mguu wetu ukiwa bado kwenye kiongeza kasi.” 

Ameonya kwamba mabadiliko ya tabianchi yako kwenye ratiba tofauti, na kiwango tofauti na wa kulaumiwa ni sisi wenyewe  kwani shughuli za binadamu ndio chanzo kikuu cha janga la mabadiliko ya tabianchi, hivyo hatua za binadamu lazima ziwe suluhu, hatua za kujenga upya matamanio na hatua za kujenga imani hususani kati ya Kaskazini na Kusini. 

Amesisitiza kwamba sayansi iko bayana ili kuhakikisha nyuzi joto duniani inasalia nyuzi 1.5 ni lazima kufikia lengo la kukomesha kabisa uzalishaji hewa ukaa ifikapo 2050. 

Katibu Mkuu wa UN António Guterres wakati wa ufunguzi wa COP27 huko Sharm el-Sheikh nchini Misri
UNIC Tokyo/Momoko Sato
Katibu Mkuu wa UN António Guterres wakati wa ufunguzi wa COP27 huko Sharm el-Sheikh nchini Misri

Dunia ina chaguo kushikamana au kuangamia

Hata hivyo hivi sasa amesema lengo hilo liko kwenye njiapanda Na ili kuepuka hali hiyo mbaya, nchi zote za G20 lazima ziharakishe mabadiliko yao sasa katika muongo huu. Nchi zilizoendelea lazima zishike usukani na nchi mbili zenye uchumi mkubwa zaidi Marekani na Uchina zina wajibu mahususi wa kuunganisha juhudi ili kufanikisha lengo hili. Hili ndilo tumaini letu pekee la kufikia malengo yetu ya mabadiliko ya tabianchi. Ubinadamu una chaguo kushirikiana au kuangamia. Ni mshikamano kuhusu mabadiliko ya tabianchi au sote tuangamie.” 

Katibu Mkuu amesema athari za mabadiliko ya tabianchi tunazo sasa na hasara na uharibu zinazousababisha hauwezi tena kupuuzwa, kwa mantiki hiyo amesisitiza kwamba  “Katika kushughulikia hasara na uharibifu, mkutano huu wa COP27 lazima ukubaliane juu ya ramani ya mwelekeo ilio bayana, iliyo na wakati unaoakisi ukubwa na uharaka wa changamoto hii. Ramani hiyo lazima itoe mipango madhubuti ya kitaasisi ya ufadhili. Habari njema ni kwamba tunajua la kufanya na tuna nyenzo za kifedha na kiteknolojia ili kukamilisha kazi hiyo. Ni wakati wa mataifa kushikamana kwa ajili ya utekelezaji. Ni wakati wa mshikamano wa kimataifa kila kona.” 

Pia ametoa wito wa kuhakikisha duniani kote kunakuwa na mifumo ya tahadhari ya mapema ya majanga katika miaka mitano ijayo na serikali kuongerza kodi katika uzalishaji wa mafuta kisukuku kwani amesema jambo moja lililo wazi ni kwamba wale watakaokata tamaa watapoteza katika vita hivi na kupoteza vita hivi sio chaguo ni lazima kuvishinda. 

Mkimbizi toka Afghanistan akipata hifadhi kwenye hema baada ya kutawanywa na mafuriko ya mvua za monsoon nchini Pakistan
© UNHCR/Usman Ghani
Mkimbizi toka Afghanistan akipata hifadhi kwenye hema baada ya kutawanywa na mafuriko ya mvua za monsoon nchini Pakistan

Ni changamoto ya kiwango na kasi tofauti

Katibu mkuu ameongeza kuwa wakati vita vya Ukraine na mizozo mingine imesababisha umwagaji damu mwingi na ghasia na kuwa na athari kubwa duniani kote, Umoja wa Mataifa hauwezi kukubali kwamba suala hilo halijazingatia mabadiliko ya tabianchi.

"Ni suala linalofafanua kuhusu umri wetu. Ni changamoto kuu ya karne yetu. Haikubaliki, ni ya kuudhi na htuwezi kuipa kisogo tena,” amesisitiza Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu ameeleza kuwa migogoro mingi ya leo inahusishwa na "kuongezeka kwa mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi". Vita vya Ukraine vimefichua hatari kubwa za uraibu wetu wa mafuta. Migogoro ya haraka ya leo haiwezi kuwa kisingizio cha kurudi nyuma au kuachna na ulinzi wa mazingira. Ikiwa kuna chochote, ni sababu ya uharaka zaidi, hatua kali na uwajibikaji Madhubuti ndio vinavyohitajika” amesema.

COP27 lazima iwe na ramani muafaka

Katibu Mkuu amesema athari za mabadiliko ya tabianchi tunazo sasa na hasara na uharibu zinazousababisha hauwezi tena kupuuzwa, kwa mantiki hiyo amesisitiza kwamba “Katika kushughulikia hasara na uharibifu, mkutano huu wa COP27 lazima ukubaliane juu ya ramani ya mwelekeo ilio bayana, iliyo na wakati unaoakisi ukubwa na uharaka wa changamoto hii. Ramani hiyo lazima itoe mipango madhubuti ya kitaasisi ya ufadhili. Habari njema ni kwamba tunajua la kufanya na tuna nyenzo za kifedha na kiteknolojia ili kukamilisha kazi hiyo. Ni wakati wa mataifa kushikamana kwa ajili ya utekelezaji. Ni wakati wa mshikamano wa kimataifa kila kona.” 

Pia ametoa wito wa kuhakikisha duniani kote kunakuwa na mifumo ya tahadhari ya mapema ya majanga katika miaka mitano ijayo na serikali kuongerza kodi katika uzalishaji wa mafuta kisukuku kwani amesema jambo moja lililo wazi ni kwamba wale watakaokata tamaa watapoteza katika vita hivi na kupoteza vita hivi sio chaguo ni lazima kuvishinda. 

Nje ya chumba na mkutano wa COP27 Sharm El-Sheikh.
UNFCCC/Kiara Worth
Nje ya chumba na mkutano wa COP27 Sharm El-Sheikh.

Ufadhili zaidi kukabiliana mabadiliko ya tabianchi 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia ametoa wito wa maendeleo katika kukabiliana na hali hiyo na kujenga uwezo wa kustahimili uharibifu wa mabadiliko ya tabianchi siku zijazo, akibainisha kuwa watu bilioni tatu na nusu wanaishi katika nchi zilizo hatarini zaidi na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hii itamaanisha kuwa nchi zitatoa ahadi iliyotolewa katika COP26 mwaka jana ya dola bilioni 40 za usaidizi wa kukabiliana na hali hiyo ifikapo 2025.

Guterres ameonya kuwa "Tunahitaji ramani ya jinsi lengo hili litkavyotimizwa. Na lazima tutambue kwamba hii ni hatua ya kwanza tu. Mahitaji ya kukabiliana na hali hiyo yanatarajia kukua hadi zaidi ya dola bilioni 300 kwa mwaka ifikapo 2030,”

Pia alieleza haja ya taasisi za fedha za kimataifa na benki kubadili mfumo wa biashara zao na kutekeleza wajibu wao.

Muhtasari wa mkutano wa utekelezaji 

Hisia hizo zilisikika katika chumba kikuu cha mkutano wa kituo cha kimataifa cha mikutano cha Tonino Lamborghini, wakati majadiliano yakifunguliwa katika siku ya kwanza ya kile kinachojulikana kama mkutano wa viongozi wa dunia, lakini ambao mwaka huu umepewa jina la “Mkutano wa utekelezaji wa mabadiliko ya tabianchi COP27 Misri.”

Afisa wa kwanza kuzungumza leo mchana, mbele ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, alikuwa Rais wa Misri, Abdel Fattah El-Sisi. Aambaye alisistiza kwamba ili kuondokana na mzozo wa leo wa mabadiliko ya tabianchi na viongozi kutekeleza wa mkataba wa Paris wanahitajika kwenda mbali zaidi ya maneno.

"Watu wa dunia wanatutazama leo na wanataka utekelezaji wa haraka wa hatua madhubuti za kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi na kuimarisha uwezo wao wa kuhimili na kuhakikisha ufadhili unaohitajika kwa nchi zinazoendelea ambazo leo zinateseka zaidi kuliko zingine," alisema.

Bwana. El-Sisi amewataka viongozi kuzingatia vipaumbele vya bara la Afrika, na kuunga mkono kanuni ya "uwajibikaji wa pamoja", ili kuhamasisha imani katika uwezo wao wa kufikia malengo ya mabadiliko ya tabianchi.

Kiongozi huyo wa Misri amesema kuwa kuna matarajio makubwa kwa mkutano huo kutoka kwa mamilioni ya watu duniani kote, na COP27 inapaswa kutoa maamuzi, ikiwa ni pamoja na kujibu maswali yenye miiba.

Wanawake wakiwa wanarejea nyumbani wakipita katika eneo ambao limeathirika vibaya na ukame Gwembe Valley Zambia
© UNICEF/Karin Schermbrucke
Wanawake wakiwa wanarejea nyumbani wakipita katika eneo ambao limeathirika vibaya na ukame Gwembe Valley Zambia

"Ninawahimiza muwe kielelezo ambacho ulimwengu unatumaini. Na kuonyesha uwezo wa kweli wa kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi,” amesisitiza.

Mwishoni mwa hotuba yake, Rais wa Misri, akiongelea machafuko, ametoa wito wa wazi kwa viongozi waliokusanyika kushinikiza kumalizika kwa vita nchini Ukraine, na hivyo kuzua shangwe miongoni mwa waliohudhuria.

"Nchi yangu sio moja ya nchi zenye nguvu zaidi kiuchumi, tuliteseka sana na COVID-19, na tunateseka tena kwa sababu ya vita hivi visivyo vya lazima. Dunia nzima inateseka,” amesema.

Picha zinazungumza zaidi ya maneno elfu moja

Filamu ya dakika 10, iliyotayarishwa na nchi mwenyeji, na kuonyeshwa kwenye skrini kubwa za muundo wa 360° ndani ya chumba cha mkutano ilikuwa moja ya vivutio vya mkutano wa Jumatatu.

Utayarishaji huo ulitumia sauti ya shairi lenye nguvu linaloelezea hatua ambazo ustaarabu wa kale wa Misri ulitumia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Ramani ya dunia ilikuwa na bendera nyekundu kuonyesha maeneo ambayo yamekumbwa na majanga mwaka wa 2022 pekee karibu dunia nzima ilifunikwa.

Kutoka Oman hadi Ufaransa, na kutoka Brazili hadi Sudan, picha zenye nguvu za uharibifu zilionyeshwa pamoja na shuhuda zenye kuvunja moyo kutoka kwa waathiriwa wa mabadiliko ya tabianchi, wakiwemo watoto.

Video hiyo pia imebainisha kuwa bila hatua halisi dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, maeneo vile Alexandria, Osaka, Rio de Janeiro, Maldives, Miami na Venice yanaweza kutoweka.

Gari likiwa limekwama kwenye mafuriko  huko Pulang Pisau katikati mwa Kalimantan Indonesia
© Greenpeace/Pram
Gari likiwa limekwama kwenye mafuriko huko Pulang Pisau katikati mwa Kalimantan Indonesia

"Tafadhali fanya kila uwezalo kuokoa jiji letu," mkazi wa Venetian alisema huku akilia.

Hata hivyo, filmu hiyo ilimalizika kwa matumaini, ikisema kwamba sayari inaendelea kutupa nafasi kwa serikali kufanya mabadiliko, kutoka nishati kisukuku na kuingia kwenye nishati mbadala na kutumia nishati hiyo kimaadili zaidi.

"Mabadiliko ya tabianchi yanatuathiri sisi sote” msimulizi mwanamke alisema, akiwaalika viongozi wa ulimwengu kupunguza changamoto zetu za sasa, kama Wamisri wa kale walivyojifunza, kuupa ustaarabu wao miaka 500 zaidi ya kuishi.

Wito kutoka kwa vijana wa Kiafrika 

Lea Namugerwa, mwanaharakati wa mabadiliko ya tabianchi kutoka Uganda, amewaomba viongozi wa dunia ambao wangepanda jukwaani kuzungumza kama wako katika dharura, kwa sababu ndivyo hali ilivyo.

Ameeleza jinsi maisha yake yalivyobadilika alipoona watu wake wa karibu wakifa kutokana na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua nyingi nchini Uganda alipokuwa na umri wa miaka 14 pekee.

Akiwa na umri wa miaka 15, alizindua shirika lisilo la kiserikali au NGO yake mwenyewe iitwayo ‘Birthday Trees’.

Badala ya sherehe ya kitamaduni ya siku ya kuzaliwa, anawaalika watu kuwa na sherehe ya upandaji miti.

"Nina lengo la kupanda miti milioni moja, lengo lako ni nini?" Amewauliza viongozi wa dunia.

Bi Namugerwa amesema kwa kuwa COP27 imepewa jina la ‘African COP’, mkutano huo unapaswa kuonyesha kuwa bara lake, wakati linazalisha chini ya asilimia 4 ya hewa chafu duniani, linakabiliwa na matokeo mabaya zaidi ya mabadiliko ya tabianchi.

"Naomba COP ya Afrika iwe COP tofauti. Acha COP ya Afrika iwe COP wa vitendo," amepaza sauti, akiwapa changamoto Marais na mawaziri wakuu kufikiria kama wanataka kukumbukwa kama viongozi ambao "hawakufanya lolote walipokuwa madarakani.”

Mwanamke akienda kusaka maji kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Kabasa huko Dolow nchini Somalia
© UNICEF/Ismail Taxta
Mwanamke akienda kusaka maji kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Kabasa huko Dolow nchini Somalia

Utashi wa kisiasa ni chanzo mbadala: Al Gore 

Wakati huo huo, na katika mojawapo ya hotuba zenye nguvu zaidi za kikao hicho, ilikuwa ni ya makamu wa rais wa zamani wa Marekani Al Gore

"Leo, kama kila siku, tunamwaga tani milioni 162 za joto lililotengenezwa na mwanadamu na kusababisha uchafuzi wa joto angani duniani kote. Huongezeka na kujilimbikiza hapo. Kiasi kinachokusanywa hunasa joto la ziada kiwango ambavyo kingetolewa na mabomu 60,000 ya atomiki ya kiwango cha Hiroshima yanayolipuka kila siku katika sayari yetu. Ndio maana tunashuhudia majanga haya," amesisitiza, akionya kuwa hali inazidi kuwa mbaya.

Bwana. Gore amesema kuwa viongozi wana tatizo la uaminifu wanazungumza lakini hawafanyi vitendo ya kutosha.

"Ni chaguo kuendelea na mtindo huu wa uharibifu kuwa mabadiliko ya tabianchi yanafanya kazi sawa na ubaguzi wa rangi huku walio hatarini zaidi wakiteseka zaidi.” Amesema bwana Gore

Ameongeza kuwa "Sio lazima kuchagua laana, tunaweza kuchagua baraka, ikiwa ni pamoja na baraka za nishati mbadala. Tuko katika hatua za awali za mapinduzi ya nishati, tukiwekeza na kuacha kufadhili utamaduni wa kifo, tunaweza kujiokoa,” alisema.

Mwanamazingira huyo mashuhuri aliyeshinda tuzo ya amani ya Nobel pia amesema kuwa Afrika inaweza kuwa kinara wa  nishati mbadala duniani, kwa sababu uwezo wa teknolojia ya jua na upepo wa bara hilo ulikuwa mara 400 zaidi ya jumla ya hifadhi ya mafuta kisukuku iliyobaki.

Amewaalika viongozi wa dunia na taasisi za fedha za kimataifa kufungua njia za kuzalisha nishati mbadala y kuleta mageuzi ikiwa ni pamoja na kupunguza viwango vya riba kwa nchi za Afrika.

"Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema tuko kwenye barabara kuu ya kuelekea kuzimu kwa mabadiliko ya tabianchi, na tunahitaji kuondoa mguu kwenye kiongeza kasi," amesema, akisisitiza kwamba maendeleo yoyote ya nishati ya kisukuku hayaendani na lengo la kufanya joto duniani kusalia chini ya nyuzi joto 1.5.

Hatimaye, ametoa wito kwa viongozi kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta athari chanya na kushughulikia tatizo lao la uaminifu.

"Tunaweza kuleta nia ya kisisa kufanya kile kinachohitajika, utashi wa kisiasa ni rasilimali inayoweza kurejeshwa", amehitimisha.