Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madhara ya tabianchi yanachanja mbuga, hatua kwa tabianchi zinadorora- UN

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Tabianchi.
UN /Cia Pak
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Tabianchi.

Madhara ya tabianchi yanachanja mbuga, hatua kwa tabianchi zinadorora- UN

Tabianchi na mazingira

Wawakilishi wa serikali wakianza kukamilisha ajenda kwa ajili ya mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP27 utakaofanyika mwezi ujao huko Misri, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewaambia waandishi wa habari jijini New York, Marekani kuwa kazi iliyo mbele ni kubwa na nzito wakati huu ambapo madhara ya tabianchi yanashuhudia kote duniani.

Katibu Mkuu amesema theluthi moja ya eneo la Pakistani imetwama kwenye maji, Ulaya inashuhudia viwango vya juu vya joto kuwahi kutokea katika miaka 500, Ufilipino imetwangwa na mafuriko, Cuba nzima haina umeme “na hapa Marekani kimbunga Ian kimepiga na kutoa kumbusho kuwa hakuna nchi au uchumi wowote duniani una kinga dhidi ya janga la tabianchi.”

Guterres amesema “madhara ya tabianchi yakichanja mbuga, hatua dhidi ya tabianchi zimekwama.”

Mahesabu hayako sawa

Mikutano ya maandalizi ya COP27 ni pamoja na ule ulioanza leo huko Kinshasa mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambapo Katibu Mkuu ametumia mkutano wake na waandishi wa habari kueleza kuwa ahadi za kundi la nchi 20, G20 kwa bado hazitoshi.

“Hatua zinazochukuliwa na hizi nchi zenye viwanda zaidi duniani na zile zinazoibukia kiuchumi hazileti majawabu yanayotakiwa,” amesema Guterres akitanabaisha kuwa ahadi za sasa na sera zinafungia mlanog lengo letu la kuhakikisha ongezeko la joto duniani halizidi nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi.

Katibu Mkuu ameonya, “tuko katika zama za kufa na kupona kwa ajili ya usalama wetu wa leo na uwepo wetu wa kesho,” akisema huu si wakati wa kunyoosheana vidole, au kusubiria jambo fulani litokee na badala yake inahitajika maridhiano na ulegezaji misimamo wa hali ya juu kati ya nchi Tajiri na zile zinazoibuka kiuchumi.

Amesema sasa hivi dunia haiwezi kusubiri ten ana kwamba kiwango cha utoaji hewa chafuzi kiko juu na kinaongezeka.

Amesisitiza umuhimu wa taasisi za kifedha kurekebisha miundo yao ya kibiashara ili kukabili mabadiliko ya tabianchi.

Tunarudi nyuma

Wakati huo huo, wakati sayari dunia inazidi kukumbwa na joto, Ukraine inazidi kukwamisha harakati dhidi ya tabianchi huku watendaji kwenye sekta ya biashara wakiendelea kukwamishwa na mifumo ya udhibiti iliyopitwa na wakati, urasimu na ruzuku hatarishi zinazotuma ujumbe usio sahihi, amesema Guterres.

Katibu Mkuu amesema maendeleo sahihi lazima yapatikane ili kushughulikia uharibifu uliokwishatokea ambao hata nchi zenye zinashindwa kukabiliana nao, sambamba na ufadhili ili kusaidia hatua dhidi ya tabianchi.

“Maamuzi lazima yafanyike sasa kwenye suala la hasara na uharibifu, na kushindwa kuchukua hatua kutasababisha imani kutoweka zaidi na uharibifu zaidi kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.”

Guterres amesema huo ni waijbu wa kimaadili ambao haupaswi kupuuzwa/

Kipimo cha Majaribio

Kwa Katibu Mkuu Guterres, COP27  ni jaribio la kwanza na kipimo cha iwapo serikali zinachukua hatua kukabili madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa nchi zilizo hatarini zaidi.

“Mkutano huo tangulizi wa COP27 huko Kinshasa utaonesha ni kwa vipi suala hili nyeti litashughulikiwa huko Sharm el-Shaikh nchini Misri mwezi ujao. Dunia inapaswa kupata ufafanuzi wa kina kutoka kwa nchi Tajiri jinsi zitakavyotoa ahadi ya dola bilioni 100 kusaidia hatua kwa tabianchi kwa nchi zinazoendelea.”

Amesisitiza kuwa katika kila harakati kwa tabianchi, jawabu pekee ni mshikamano na hatua za msingi za uamuzi.

Ongeza hatua kwa tabianchi na usaidizi

Huko Kinshasa, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed amewaonya mawaziri wa mazingira na wengineo kuwa dirisha la fursa ya kuepuka madhara makubwa linafunga.

Amesisitiza kuwa msaada mkubwa kwa shughuli za uhimili wa tabianchi kwa nchi zinazoendelea lazima uwe kipaumbele cha dunia hasa katika ufadhili wa miradi ya kujenga uhimili na kukabiliana.

Bi. Mohammed amerejelea mkutano wa mwaka jana wa COP26 huko Glasgow, Uingereza ambako nchi zilizoendelea ziliahidi kusaidia bilioni 40 kila mwaka hadi mwaka 2025.

Naibu Katibu Mkuu huyo wa UN ametoa wito wa mkakati wa wazi wa jinsi ya kufanikisha ufadhili wa fedha hizo kuanzia mwaka huu.

Ameongeza kuwa kiwango hicho cha dola bilioni 40, ni sehemu ndogo tu ya dola bilioni 300 zinazohitajika kila mwaka na nchi zinazoendelea kwa ajili ya miradi ya kukabili mabadiliko ya tabianchi ifikapo mwaka 2030.

Kila nyakati inahesabika

Bi. Mohammed amesisitiza kuwa dunia sasa inahitaji matumaini.

“Tunahitaji maendeleo… hii inaonesha kuwa viongozi wanaelewa kwa kina kiwango cha udharura tunaokabiliana nao na thamani ya COP, kama sehemu ambako viongozi wa dunia wanakutana kutatua matatizo na kuwajibika.”

Kila wakati unahesabika, amesisitiza akisema ni wakati wa kuonesha kuwa “tunasonga katika mwelekeo sahihi na matokeo yanayoonesha kuwa hatua zetu za pamoja ni kushughulikia janga la tabianchi kwa sababu watu na watoto hapa leo na sayari ni muhimu.