Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umuganda ni chachu muhimu ya kukabili mabadiliko ya tabianchi Rwanda: UN Rwanda

Baadhi ya wakazi wa kitongoji cha Masoro kilichoko mji mkuu wa Rwanda, Kigali ambao walishiriki Umuganda.
UN/ Flora Nducha
Baadhi ya wakazi wa kitongoji cha Masoro kilichoko mji mkuu wa Rwanda, Kigali ambao walishiriki Umuganda.

Umuganda ni chachu muhimu ya kukabili mabadiliko ya tabianchi Rwanda: UN Rwanda

Tabianchi na mazingira

Umuganda ni mkakati wa kujenga jamii nchini Rwanda ambao dhana ya ni nzuri sana kwani kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa tano asubuhi, biashara zote, maduka, barabara hufungwa, huku raia kote nchini wanakusanyika kwenye vitongoji vyao na kusaidia katika mradi teule wa jamii kwa wiki hiyo. 

 

Umuganda ni nini hasa 

Maana rahisi ya Umuganda ni “Kushikamana kwa azma ya pamoja ili kuleta tija katika jamii.  

Mkakati huo wa Umuganda ulioanzishwa rasmi mwaka 1962 muda mfupi baada ya uhuri ili kuzisaidia jamii kushikamana, kusaidia na kujijenga na unahisisha shughuli mbalimbali za kijamii iwe ujenzi wa shule, barabara, kumsaidia mwanajamii kulima au kujenga nyumba, upandaji wa miti kulinda mazingira na shughuli nyingine nyingi za kijamii. 

Awali kushiriki Umuganda ilikuwa si lazima lakini sasa ni lazima n ani amri ya serikali katika nchi nzima ambapo kila kaya inapaswa kujitokeza kwa muda huo was aa 3 kuchangia katika maendeleo ya jamii yake na kushindwa kufanya hivyo ni kosa linasababisha kulipa faini. 

Wakazi wa eneo la Masoro kwenye mji mkuu wa Rwanda Kigali wakikusanyika tayari kushiriki kwenye Umuganda, shughuli ya kijamii ya upandaji miti.
UN/ Flora Nducha
Wakazi wa eneo la Masoro kwenye mji mkuu wa Rwanda Kigali wakikusanyika tayari kushiriki kwenye Umuganda, shughuli ya kijamii ya upandaji miti.

Lengo kuu la Umuganda 

Wakati baadhi ya miradi ua Umuganda inalenga zaidi maendeleo ya miundombinu kama vile ujenzi wa shule na makazi kwa wale wanaohitaji, asilimia kubwa ya juhudi za Umuganda zinajikita katika ulinzi na uhifadhi wa mazingira na usafishaji wa maeneo ya umma.  

Kwa mantiki hiyo mradi huo unaweza kujumuisha kusaidia katika ujenzi wa barabara, kusafisha mitaa, kukata nyasi, kukata vichaka kando ya barabara, kupanda miti, kukusanya na kuzoa takataka na kukarabati majengo ya umma ili kuweka mazingira safi. 

Mwishoni mwa wiki ofisi ya Umoja wa Mataifa Rwanda na serikali walishiriki zoezi la upandaji miti kama mradi waliouchagua kwa wiki hii lengo likiwa kuichagiza jamii kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi kwa kulinda na kuhifadhi mazingira. 

Watu mbalimbali walishiriki wakiwemo wawakilishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, viongozi wa serikali na kikubwa zaidi ni idadi kubwa ya wanajamii wa rika mbalimbali waliojitokeza ambao wamesema “Umuganda ni hatua muhimu ya kuichagiza na kuihamasisha jamii na watu wa rika zote umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mazingira, kushirikiana na kujifunza hulka ya kuthamini masuala ambayo ni ya muhimu katika maisha kama kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa ajili ya kuhakikisha tunalinda kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.” 

Pia wametoa wito kwa nchi Jirani na dunia kwa ujumla kuiga mfano wa Rwanda wa mradi wa Umuganda ambao umeleta tija kubwa kwa taifa hilo la Afrika Mashariki tangu ulipoanzishwa miaka 60 iliyopita. 

Upandaji miti wakati wa Umuganda huko Masoro kwenye mji mkuu wa Rwanda, Kigali.
UN/ Flora Nducha
Upandaji miti wakati wa Umuganda huko Masoro kwenye mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

Umuganda na mabadiliko ya tabianchi 

Akizungumzia mchango wa Umuganda katika juhudi za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi Waziri wa mazingira wa Rwanda Jeanne d’Arc Mujawamaria amesema “Umuhimu wa Umuganda kupambana na mabadiliko ya tabianchi ni kupanda miti kwenye milima yote, kupanda miti majumbani kwetu na kupanda miti karibu na barabara na kupanda miti karibu na vyanzo vya maji, kokote tunakoona kunatakiwa kuwa na miti.” 

Ametoa wito kwa wananchi wa Rwanda na dunia kwa ujumla kulinda mazingira kwa faida ya kizazi hiki na kijacho “Wananchi wa Rwanda na wa dunia kulinda mazingira ni muhimu sana kwa sababu mabadiliko ya tabianchi ni tatizo kwa watu wote, kwa Wanyama na kwa nchi zetu, kwa hivyo tunatakiwa kulinda mazingira” 

Aliyeuwakilisha Umoja wa Mataifa Rwanda katika shughuli Maxwell Gomera amesisitiza kuendelea kulinda mazingira kupitia Umuganda kwani ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa kuhusu uchafuzi wa mazingira ambacho ni kichocheo kikubwa cha mabadiliko ya tabianchi inaonyesha kuna pengo kubwa la juhudi za kukabiliana na uchafuzi wa hew ana mazingira UNEP shirika la Umoja wa Mataofa la mpango wa mazingira limebainisha kwamba lengo za uzibaji pengo la kupunguza uchafuzi wa hali ya hewa linaweza kufikiwa tu endapo nchi zote zitajizatiti na kuchukua hatua za pamoja kama tulizozishuhudia leo za Umuganda.” 

Rwanda ni moja ya nchi ambazo zimedhamiria katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na has kwa kuhakikisha inaweka mazingira bora kupitia upandaji miti kila mahali ikiamini kwamba faida zake sio kwa kizazi hiki pekee bali pia kwa vizazi vijavyo.