Mhamiaji mmoja, mti mmoja; kampeni yajenga utangamano Niger

6 Agosti 2019

Nchini Niger maadhimisho ya siku ya uhuru yameenda sambamba na upanzi wa miti ukibeba kauli mhamiaji mmoja mti mmoja katika taifa hilo ambalo takribani eka 100,000 za ardhi yenye rutuba hupotea kila mwaka kutokana na ukataji miti hovyo.

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM limesema mkakati huo ukiongozwa na shirika la kiraia la JEMED, umehusisha zaidi ya wahamiaji 100 wanaoishi kwenye vituo vya muda kwenye mji mkuu Niamey, pamoja na wahamiaji wengine wanaoishi kwenye vitongoji vya hali ya chini karibu na eneo hilo.

Kampeni hii ya siku moja ya upandaji miti ilienda sambamba na wahamiaji kupata fursa ya kujadili safari zao za uhamiaji na matumaini yao kwa siku za usoni.

“Huu ni mpango mzuri, si tu kwamba upandaji wa hii miti utaleta tofauti chanya kwa watoto wanaokwenda shule, bali pia ni fursa ya kukutana na watu kutoka mataifa mbalimbali,” amesema Adamao, mkazi wa moja ya vitongoji vya jirani akisema kuwa “inatukumbusha kuwa sisi sote ni ndugu.”

Naye mhamiaji mwingine, Ousmane kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR akizungumzia mpango huo amesema, “mara nyingi watu wanatuona kama wasumbufu na mzigo. Ni vyema kuwa tumepata fursa leo ya kuonyesha kuwa nasi pia tunaweza kusaidia na kuleta tofauti kwenye jamii. Hii miti ni ushahidi, itakuwa mchango wetu pindi tutakapoondoka Niger.”

Kwa upande wake mkuu wa IOM nchini Niger, Barbara Rijks amesema, “hii ni fursa kubwa kwa wahamiaji na jamii kushirikiana kutekeleza lengo moja. Tunafurahi kushirikiana na JEMED katika siku hii ya kuhamasisha kuhusu masuala muhimu kama mazingira na wakati huo huo kujenga uhusiano mzuri baina ya watu mbalimbali kwenye jamii.”

Tangu mwaka 1975 Niger imekuwa ikisherehea siku yake ya uhuru tarehe 3 Agosti kwa kuhamasisha wananchi kupanda miti na kufanya shughuli za kulinda mazingira ambazo ni muhimu ili kukabiliana na ukataji miti holela nchini humo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter