Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki za binadamu ni moyo wa juhudi za kukabiliana athari za tabianchi: Türk

Mtoto akiwa amesimama karibu na pampu ya maji iliyozingirwa na maji ya mafuriko huko Gatumba nchini Burundi.
© UNICEF/Karel Prinsloo
Mtoto akiwa amesimama karibu na pampu ya maji iliyozingirwa na maji ya mafuriko huko Gatumba nchini Burundi.

Haki za binadamu ni moyo wa juhudi za kukabiliana athari za tabianchi: Türk

Haki za binadamu

Kuelekea mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Tabianchi, COP27 huko Sharm el-Sheikh nchini Misri, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu Volker Türk amesema anatarajia matokeo ya mkutano huyo yatazingatia haki ya kila mtu ya kuishi ambaypo kwa sasa ipo hatarini kutokana na uwepo wa hatua zisizotosheleza za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Taarifa iliyotolewa hii leo huko Geneva, Uswisi na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu kwa vyombo vya habari,  imesema katika  barua hiyo ya awazi Bwana Turk anaonya kuwa haki za binadamu ni lazima ziwepo kwenye mazungumzo kwakuwa ndio moyo wa juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Matokeo ya mkutano huo ni muhimu kwa watu wanapaswa kufurahia haki za binadamu kote ulimwenguni, sio tu katika miaka ijayo lakini hata sasa. Watu wanapoteza makazi yao, riziki zao na maisha yao. Kwa kuzingatia mwelekeo wa sasa wa ongezeko la joto, sehemu nyingi ulimwenguni hazitakuwa zinafaa watu kuishi katika kipindi hiki hiki cha Maisha ya watoto wetu, na matokeo yasiyoweza kufikiria," amesema Türk.

Kamishna huyo wa haki za binadamu ameeleza kuwa ukosefu wa haki unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi ni janga akitolea mfano mafuriko nchini Pakistan, ambayo hivi karibuni yaliathiri zaidi ya watu milioni 30.

“Itachukua miaka mingi kujenga upya na hata kuanza kuelewa matokeo ya msiba huu mmoja.” Türk aliendelea alisema na kuongeza kuwa “Misiba kama hiyo inakusudiwa kuwa jinamizi la mara kwa mara kwa watu ulimwenguni kote ikiwa hatutachukua hatua kubwa, zinazotegemea haki ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kupunguza athari zake, na kushughulikia mateso ambayo tayari yamesababisha.”