Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua mpya za Marekani za kudhibiti mipaka zahatarisha haki za binadamu – Türk

Wahamiaji wa Amerika ya Kati katika kituo cha uhamiaji kilichopo mpaka ya Mexico na Texas. (Maktaba)
© UNICEF/Adriana Zehbrauskas
Wahamiaji wa Amerika ya Kati katika kituo cha uhamiaji kilichopo mpaka ya Mexico na Texas. (Maktaba)

Hatua mpya za Marekani za kudhibiti mipaka zahatarisha haki za binadamu – Türk

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Volker Türk, ameonya kuwa mikakati mipya iliyotangazwa na serikali ya Marekani ya kudhibiti au kulinda mipaka yake inadumaza misinig ya kimataifa ya haki za binadamu. 

Taarifa iliyotolewa leo jijini Geneva, Uswisi na ofisi ya kamishna huyo wa haki za  binadamu, OHCRC, imesema haki ya kusaka hifadhi ni haki ya binadamu bila kujali mtu atokako, hadhi  ya uhamiaji au jinsi alivyowasili katika mpaka wa kimataifa. 

Amesema “hatua hizi zinaonekana kuwa kinyume na vizuizi vya kufurusha watu kwa jumla na kanuni ya kutofukuza watu ambayo inayosema wale wanaosaka hifadhi wanaweza wasirejeshwe makwao kwa misingi kuwa wanaamini wanaweza kukumbwa na mateso.” 

Hatua hizo mpya zimetangazwa kufuatia ziara ya Rais Joe Biden nchini Mexico. 

Mabadiliko ni yapi? 

Mabadiliko hayo yanajumuisha ongezeko la matumizi ya kasi ya kuwaondoa wasaka hifadih na matumizi ya kifungu namba 42 kuhusu afya kinachoruhusu kufukuwa na kurejeshwa Mexico kutoka Marekani kwa raia takribani 30,000 wa Venezuela, Haiti, Cuba na Nicaragua kila mwezi. 

Kifungu namba 42 tayari kimekuwa kinatumiwa na maafisa uhamiaji wa Marekani kwa mara milioni 2.5 kwenye mpaka wa kusini wa Marekani kufukuzia watu kuelekea Mexico au makwao bila tathmini ya mtu mmoja mmoja ya mahitaji yao. 

Na wakati huo huo, programu ya msamaha kwa misingi ya kibinadaumu ambayo awali ilielekezwa kwa raia wa Venezuela, sasa itapanuliwa kujumuisha raia kutoka Cuba, Haiti na Nicaragua kuruhusu watu 30,000 kila mwezi kutoka nchi hizo kuingia Marekani kwa kipindi cha miaka miwili kwa kuzingatia vigezo na masharti. 

Naunga mkono lakini mikakati isibinye haki za msingi 

“Ingawa nakaribisha mikakati ya kuweka na kupanua njia salama za uhamiaji kama hizi, lakini mikakati hii haipaswi kutumika huku ikikandamiza haki za msingi za kibinadamu na hitaji la hifadhi kwa misingi ya kila mahitaji ya mtu kuangaliwa na kutathminiwa,” amesema Bwana Türk . 

Ameeleza wasiwasi wake kuwa wale wenye uhitaji zaidi wa kusaka hifadhi na wale walio katika hatari zaidi wanaweza wasikidhi vigezo vikali vya kupata msamaha wa kiutu kama vile kuwa na mfadhili wa kifedha nchini Marekani. 

Bwana Türk  amesisitiza wito wake wa kutaka wakimbizi na wahamiaji wote kuheshimiwa na kulindwa kwenye mipaka ya kimataifa. 

“Tunasikia mambo mengi kuhusu majanga ya uhamiaji lakini kihalisia, walio kwenye janga zaidi ni wahamiaji wenyewe. Badala ya kuwanyima haki zao za msingi ni lazima tusake mbinu za kusimamia vyema uhamiaji kwa njia ya kiutu na salama huku tukiheshimu haki ya kila mtu,” amesema Bwana Türk.