Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Türk apendekeza mbinu iliyoratibiwa ili kuwaokoa Warohingya baharini

Watu wa Rohingya waliokwama wakiwa wameketi kwenye boti ya wasafirishaji haramu katika Bahari ya Andaman mnamo 2015.
UNHCR/Christophe Archambault
Watu wa Rohingya waliokwama wakiwa wameketi kwenye boti ya wasafirishaji haramu katika Bahari ya Andaman mnamo 2015.

Türk apendekeza mbinu iliyoratibiwa ili kuwaokoa Warohingya baharini

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Volker Türk leo jijini Geneva, Uswisi ametoa wito wa kuwepo kwa mbinu iliyoratibiwa ya kikanda ili kuwalinda maelfu ya Warohingya waliokata tamaa wanaohatarisha maisha yao kwa kufanya safari hatari za baharini.

"Zaidi ya Warohingya 2,400 wamejaribu kuondoka Bangladesh na Myanmar mwaka 2022 pekee, na nina huzuni kubwa kwamba zaidi ya watu 200 wameripotiwa kufariki dunia wakiwa njiani. Ripoti za hivi karibuni zinaonesha kuwa boti zilizojaa na zisizo salama zinazowabeba Warohingya zimeachwa zikiyumba kwa siku nyingi bila msaada wowote.” amesema Türk.

"Wakati janga la baharini likiendelea, ninaziomba nchi katika eneo hili kuweka utaratibu ulioratibiwa ili kuhakikisha kuwa utafutaji na uokoaji wa kina, kushushwa kwa wakimbizi wa Rohingya kwenye maeneo yao, na ulinzi wao mzuri." Ameongeza akibainisha kuwa baadhi ya Mataifa yalikuwa yameshatoa msaada.

Aidha Kamishna huyo Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa nchi za eneo hilo na kimataifa kusaidia Bangladesh kusaidia wakimbizi zaidi ya milioni moja wa Rohingya ambao wametafuta ulinzi huko tangu 2017 kwa heshima kamili ya utu na haki za binadamu kama raia kamili na sawa wa Myanmar.