Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Stadi sahihi kwa vijana ni jawabu la kufanikisha SDGs 2030- Guterres

Viki Bokanda, ingawa ni mvulana mwenye umri wa miaka 15 anajifunza  ushoni kwenye kituo cha mafunzo stadi kwa wasichana  huko Kisangani, Kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
© UNICEF/UN0507530/Frank Dejongh
Viki Bokanda, ingawa ni mvulana mwenye umri wa miaka 15 anajifunza ushoni kwenye kituo cha mafunzo stadi kwa wasichana huko Kisangani, Kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Stadi sahihi kwa vijana ni jawabu la kufanikisha SDGs 2030- Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Leo ni siku ya kimataifa ya stadi kwa vijana yenye lengo la kuangazia umuhimu wa marekebisho ya stadi hizo ili hatimaye siku za usoni vijana waweze kuendana na mahitaij ya kazi zilizoko au zitakuweko.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wa siku hii iliyopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2014, anasema, “vijana wameathiriwa kwa kiasi kikubwa na majanga yanayokumba dunia, kuanzia mabadiliko ya tabianchi,, mizozo na umaskini.”
Amesema janga la COVID-19 ni kama ‘limetia chumvi kwenye kidonda’ kwa sababu ajira miongoni mwa vijana iliporomoka kwa kwa kuwa na idadi ya vijana milioni 39 wasio na ajira mwaka 2020 pekee.

“Hii leo vijana milioni 24 duniani kote wako hatarini kushindwa kurejea shuleni,” amesema Guterres.
Amefafanua kuwa janga pia limeongeza kasi ya marekebisho zaidi ya soko la ajira na hivyo kuongeza ukosefu wa uhakika wa mustakabali sambamba na kupanua pengo la kidijitali.

“Lazima tuhakikishe uzingatiaji wa haki ya vijana ya kuwa na elimu bora na jumuishi, mafunzo na kuendeleza stadi kwa maisha yao yote,” amesema Katibu Mkuu.

Msingi wa mkutano wa Septemba kuhusu elimu

Hata hivyo amesema kwa hali ilivyo sasa hilo ni changamoto kwa kuwa, “hilo linahitaji ‘kufumua kabisa’ mfumo wa stadi za kuendeleza vijana huku tukiwekeza kwenye elimu ya ufundi stadi, masuala ya kuunganishwa kimtandao na stadi za kidijitali.”

Guterres amesema ni kwa msingi huo ndio maana mwezi Septemba mwaka huu anaitisha mkutano wa ngazi ya juu kuhusu Marekebisho ya Mfumo wa Elimu duniani. 

“Mkutano huu utaleta pamoja marais, viongozi wa nchi, vijana na watendaji kwenye sekta ya elimu. Vijana ndio kichocheo cha mabadiliko na lazima washiriki katika upitishaji wa uamuzi utakaoathiri mustakabali wao,” amesisitiza Katibu Mkuu.

Ametamatisha ujumbe wake akisema ya kwama, “tukiongozwa na mkakati wa Umoja wa Mataifa kwa vijana mwaka 2030, nasihi kila mmoja wetu kupatia kipaumbele uendlezaj iwa stadi kwa vijana wakati wa mkutano na hata baada ya mkutano.”

“Kwa pamoja hebu na tujenge nguvu kazi ya usawa, yenye ustawi, tusongeshe malengo ya maendeleo endelevu na tusimwache nyuma mtu yeyote,” ametamatisha Katibu Mkuu.TAGS: Siku za UN, Stadi kwa Vijana, SDGs, Marekebisho ya mfumo wa Elimu.