Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahudumu wa afya Ethiopia warejesha tabasamu kwa watoto- UNICEF

Sedelia Abdullahi ni mhudumu wa afya wa mstari wa mbele huko mashinani nchini Ethiopia na kila siku huchunguza na kutibu watoto wenye utapiamlo kwenye kituo cha afya cha kambi ya wakimbizi ya Bambassi nchini Ethiopia kilichojengwa na UNICEF kwa ufadhili …
UNICEF Ethiopia
Sedelia Abdullahi ni mhudumu wa afya wa mstari wa mbele huko mashinani nchini Ethiopia na kila siku huchunguza na kutibu watoto wenye utapiamlo kwenye kituo cha afya cha kambi ya wakimbizi ya Bambassi nchini Ethiopia kilichojengwa na UNICEF kwa ufadhili wa Muungano wa Ulaya.

Wahudumu wa afya Ethiopia warejesha tabasamu kwa watoto- UNICEF

Afya

Nchini Ethiopia, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniain, UNICEF kupitia msaada kutoka Muungano wa Ulaya umewezesha mamia ya wahudumu wa afya walio mstari wa mbele kila uchao kuweza kutembelea wakimbizi wa ndani waliofurushwa makwao kutokana na mzozo kwenye jimbo la Benishangul-Gumuz lililoko kaskazini-magharibi mwa taifa hilo, likipakana na Sudan ili kuwapatia huduma za lishe bora wakati huu ambapo watoto wanakabiliwa na utapiamlo.

Miongoni mwa wahudumu hao ni Sedelia Abdulahi ambaye katika video ya UNICEF anaonekana akitembea katikati ya vibanda ambavyo ni wakazi wa wakimbizi wa ndani hapa kambini Bambassi nchini Ethiopia.

Yeye ni shujaa wa watumishi walio mstari wa mbele na anasema hapa kuna takribani wakimbizi wa ndani elfu 12 wanaoishi hapa. Watu wamekimbia mapigano kwenye makazi yao. Na kama uonavyo wamekimbia bila kubeba kitu chochote na wako kwenye hali ngumu, hasa wanawake na watoto ambao hali zao ni mbaya.”

Asemacho ni dhahiri, vibanda ni vichakavu, halikadhalika mavazi na hata kando kwenye mafiga moshi unafuka kwa mlo ambao hauna virutubisho vya lishe.

Tweet URL

Akiendelea Bi. Abdullahi akiwa kwenye kituo cha afya, pamoja na mama na mtoto anasema nikiwa mtumishi wa mashinani, lengo langu ni kubaini watoto wenye utapiamlo na kuwapatia huduma kila siku.

Baada ya kipimo anampatia mama kipakiti chenye mlo wenye virutubisho na mama anamlisha mtoto wake.

Wakati wa ziara ya nyumba kwa nyumba alikutana na mtoto Asanti mwenye umri wa miaka miwili na kumpatia matibabu ya utapiamlo, na sasa mama yake aitwaye Assefu Kabede anasema, “alipoanza kuugua alianza na kuhara, kisha mwili ukavimba, akawa anawashwa na kulia mno. Lakini sasa nashukuru Mungu anaendelea vizuri”

Kauli hii ni ya kutia moyo kwa Bi. Abdullahi ambaye anasema kuona watoto wanatabasamu na kucheza baada ya kupona magonjwa mbali mbali ni malipo tosha na inafurahisha.

Ethiopia ni miongoni mwa mataifa duniani ambako wananchi wake hawana uhakika wa kupata chakula kutokana na mizozo na ukame uliosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.