Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yasaidia familia zinazokabiliwa na ukame na utapiamlo nchini Ethiopia

Mvulana akiongoza punda kuelekea nyumbani katika eneo lililoathiriwa na ukame kusini mashariki mwa Ethiopia.
© UNICEF/Mulugeta Ayene
Mvulana akiongoza punda kuelekea nyumbani katika eneo lililoathiriwa na ukame kusini mashariki mwa Ethiopia.

UNICEF yasaidia familia zinazokabiliwa na ukame na utapiamlo nchini Ethiopia

Tabianchi na mazingira

Ukame mkali katika maeneo ya nyanda za chini huko Ethiopia uliosababishwa na mvua kutonyesha katika misimu mitatu mfululizo umekausha visima vya maji, kuua mifugo na kusababisha zaidi ya wananchi 2000 kuyakimbia makazi yao.

Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF ikionesha kambi ya wakimbizi wa ndani ya Awralyas, kwenye jimbo la Somali nchini Ethiopia, eneo ambalo ni makazi ya takriban watu 2000 wanaume, wanawake na watoto walioathirika na ukame.  

Upepo mkali unavuma na kupeperusha vumbi! Makundi ya watu yamekusanyika yakiangalia mizoga ya mifugo yao iliyokufa kutokana na kukosa chakula na maji kwa muda mrefu, mizoga ya ng’ombe imesambaa kila mahala katika eneo hili la Ethiopia

Bashir Sheik Mohammed ni mtaalamu wa lishe wa UNICEF na anasema mbali na ukame huu kusababisha watoto 155,000 kutoka maeneo ya Somali na Oromia kuacha shule ili waweze kusaidia wazazi wao kusaka maji, watoto wengi na wajawazito wanakabiliwa na utapiamlo, “UNICEF inasaidia vituo vya muda vya afya ikiwa ni njia mojawapo ya kuzuia, kugundua mapema na kutibu watoto wanaokabiliwa na utapiamlo mkali. Hii ni sehemu ya mkakati ambao tunauthamini katika kupunguza vifo visivyo vya lazima miongoni mwa watoto, na hii ni sehemu muhimu katika harakati za kuokoa maisha , kuweka mazingira safi, kutibu utapiamlo na matibabu mengine ya magonjwa ya kawaida na ikiwa ni pamoja na kutoa chanjo.” 

Kauli ya Bashiri inathibitishwa na Iman Magan aliyepata huduma hiyo, “naitwa Iman Magan, ninatoka Wilaya ya Debele. Niliondoka Gelile-el mapema leo asubuhi. Kule kuna ukame mkali. Kuna kiu kubwa, uchovu, na shida nyingine nyingi. Hali ni ngumu. Mtoto wangu anateseka, na tunakabiliwa na changamoto. Nilikuja kutafuta dawa kwa ajili ya mtoto wangu. Alichunguzwa na kukutwa na utapiamlo. Alipewa dawa na vyakula vyenye lishe. Nimepata huduma bora.” 

Hadi sasa katika maeneo yaliyoathiriwa na ukame katika mikoa ya Oromia na Somali nchini Ethiopia, kuna takriban watu  milioni 4.4 wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa maji kati yao hao ni watoto 850,000 wanaougua utapiamlo. 

UNICEF inaomba dola milioni 351 kwa ajili ya matibabu ya utapiamlo na pia mahitaji mengine ya kibinadamu nchini Ethiopia