Mradi wa UNICEF wasaidia kutokomeza utapiamlo kwenye jimbo la Somali nchini Ethiopia

25 Julai 2019

Nchini Ethiopia, mradi wa aina yake wa kuwezesha familia kujikimu hata zile zilizo katika hali duni, PSNP, umesaidia wakazi wa jimbo la Somali nchini humo kukabiliana na njaa, lishe duni na umaskini. 

Kutana na Kawsar Yusuf Nur, mkazi wa jimbo la Somali nchini Ethiopia na mnufaika wa mradi wa kunusuru kaya maskini, PSNP. Mradi huu hulenga wenye uwezo wa kufanya kazi ambao hulipwa ujira kwa kazi  ya umma, na familia ambazo watoto wao wana utapiamlo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,  UNICEF, serikali ya Sweden na wadau wengine wanasaidia Ethiopia katika uanzishaji wa mradi huu.

Kawsar anasema kabla ya mradi huu, alipokuwa mjamzito hakuwa na chakula,

(Sauti ya Kawsar Yusuf Nur)

Lakini nilipojiunga tu na PSNP, nilipokea mgao, nilipata fedha, kila kitu. Awali tulizoea kula mtama na vyakula vigumu.  Nilikuwa siwezi kununua vyakula laini. Lakini sasa naweza kununua mchele, tambi na uji. Sasa tunaweza kulisha watoto wet una hakuna tena utapiamlo.

Kila mwezi kaya maskini  hupatiwa fedha na kuendeleza vikundi vyao vya kujiwekea akiba. PSNP  inaunganisha wanufaika na huduma za  bure za kijamii, hususan kaya maskini zaidi ambapo kuna kuwepo na wahudumu mahsusi wa kijamii kusimamia.

(Sauti ya Kawsar Yusuf Nur)

Tulinufaika na mradi wa kuendeleza watoto, kwa sababu watoto wetu walianza kwenda shuleni. Wahudumu wa afya wanatutembelea na wakikuta kuna mjamzito au mama anayenyonyesha mtoto, wanasema asifanye kazi ngumu, apumzike na wanatutia moyo. Wanatupatia mafunzo ya kazi.”

Sasa familia zinajihisi salama kwa sababu ya PSNP na hakuna kaya yenye mtoto mwenye utapiamlo.

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud