Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Je inawezekana kuwa mtalii endelevu? Njia 12 zinazoathiri safari zako 

Utalii endelevu unaweza kusaidia kupunguza umasikini bila kuathiri mazingira
UNDP Bhutan
Utalii endelevu unaweza kusaidia kupunguza umasikini bila kuathiri mazingira

Je inawezekana kuwa mtalii endelevu? Njia 12 zinazoathiri safari zako 

Tabianchi na mazingira

Baada ya utalii kuporomoka wakati wa janga la COVID-19 sasa, utalii unaanza tena kuibuka.  

Hii ni habari njema kwa wafanyikazi na wafanyabiashara wengi, lakini labda sio kwa sayari hii dunia tunayoishi.  

Haya hapa ni baadhi ya mawazo ambayo yangeruhusu watalii kuepuka kuharibu mazingira wakiwa likizoni au mapumzikoni. 

Utalii haukosi mambo mazuri kwani karibu watu bilioni mbili husafiri kila mwaka kwa madhumuni ya burudani.  

Usafiri huchangia katika kubadilishana uzoefu, kwa usikivu zaidi wa kitamaduni na kuimarisha jamii.  

Pia utalii unanaunda nafasi za ajira, huchochea maendeleo ya kikanda na ni kichocheo kikuu cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi. 

Bado kuna hasara: Maeneo yote maarufu zaidi ni waathirika wa kuongezeka kwa uchafuzi wa mazingira, hatari za mazingira, uharibifu wa urithi na unyonyaji kupita kiasi wa rasilimali.  

Kinachoongezwa kwa hili ni uchafuzi unaosababishwa na kusafiri kwenda na kutoka maeneo haya. 

Ndiyo maana vidokezo hivi vichache vitakusaidia kufurahia safari yako, na kuhakikisha kuwa kivutio chako cha utalii hakitateseka kutokana na uwepo wako. 

1. Acha matumizi ya mara moja ya plastiki 

Mara nyingi hutumika kwa chini ya dakika 15, vitu vya plastiki vya matumizi ya mara moja vinaweza kuchukua zaidi ya miaka 1,000 kuharibika.  

Wengi wetu tunapendelea chaguzi endelevu katika maisha yetu ya kila siku, na tunaweza kuwa na mtazamo sawa tunapokuwa safarini.  

Kwa kuchagua chupa na mifuko inayoweza kutumika tena popote unapoenda, unaweza kusaidia kupunguza janga la taka za plastiki kwenye bahari na makazi mengine. 

2. Uwe na busara kuhusu maji 

Kwa ujumla, watalii hutumia maji mengi zaidi kuliko wakazi wa eneo hilo. Kadiri uhaba wa maji unavyozidi kuongezeka, chaguo na tabia zetu zinaweza kusaidia kudumisha ufikiaji wa kutosha wa maji kwa siku zijazo.  

Kwa kusacha, kwa mfano, kubadilisha mashuka na taulo kila siku wakati wa kukaa hoteli, tunaweza kuokoa mamilioni ya lita za maji kila mwaka. 

Kula vyakula vya wenyeji kutakupa ladha tofauti na kusaidia kuinua kipato cha wenyeji
UNDP Bosnia and Herzegovina/Adnan Bubalo

 

3. Tumia bidhaa za ndani 

Unaponunua bidhaa za ndani, unasaidia kukuza uchumi mahali ulipo, na kupunguza kiwango cha hewa ukaa ambacho kinaweza kutokana na kusafirisha bidhaa kutoka sehemu ya mbali ya uzalishaji.  

Kifungua kinywa chako kinaweza kuleta mabadiliko. Furahia mazao mapya, yanayokuzwa nchini kila unapopata fursa. 

4. Panga mambo kimaadili 

Kuandaa safari kunahusisha kila aina ya vifaa na waendeshaji wa usafiri, pamoja na wingi wa wauzaji.  

Kila kiungo kwenye mnyororo wa thamani kinaweza kuwa na athari chanya au hasi kwa mazingira.  

Ikiwa unapendelea kukabidhi upangaji huu kwa mtu mwingine zaidi yako mwenyewe, hakikisha umechagua mwendeshaji ambaye anatanguliza mbele mazingira, anatumia rasilimali kwa ufanisi na kuheshimu utamaduni wa wenyeji. 

Utalii endelevu unafaida kwa mazingira, uchumi na kwa jamii
© UNWTO

 

5. Tafadhali usiwalishe wanyama 

Kushiriki chakula na wanyamapori, au kuwa karibu nao sana, huongeza hatari ya kueneza magonjwa kama homa, kichomi, mafua na homa ya mapafu ,kutoka kwa wanadamu hadi kwa wanyama.  

Zaidi ya hayo, wanyama wanapozoea kupokea chakula kutoka kwa wanadamu, tabia zao za asili hubadilika na kuwa tegemezi kwa wageni ili waendelee kuishi. Katika baadhi ya matukio, inaweza pia kusababisha mgongano kati ya mwanadamu na mnyama. 

6. Na usiwale pia 

Ulaji wa viumbe wa kigeni au walio katika hatari ya kutoweka huleta mahitaji ambayo husababisha kuongezeka kwa ujangili, usafirishaji haramu na unyonyaji wa wanyama.  

Mbali na kudhuru mnyama kwenye sahani yako, kula bila kuwajibika kunaweza kuchangia kutoweka kwa aina ambazo tayari zimetishiwa na mabadiliko ya tabianchi na upotezaji wa makazi.  

Kumbuka hili unaponunua zawadi na epuka bidhaa zinazotengenezwa na wanyama wa pori walio hatarini kutoweka. 

7. Kufanya safari pamoja 

Usafiri huchangia pakubwa kwa alama ya hewa ukaa itokanayo na utalii. Badala ya kukodi teksi za kibinafsi, tumia usafiri wa umma kama vile treni, mabasi na teksi za pamoja.  

Unaweza pia kuchukua baiskeli, njia rahisi na ya bei nafuu ya kuchunguza maeneo. 

8. Kaa na wenyeji 

Kukaa na mwenyeji au familia ni chaguo rafiki wa asili ambayo inakuwezesha kuimarisha utamaduni na desturi za jamii husika.  

Chaguo hili huleta mapato kwa jamii za karibu huku zikikupa fursa ya kupata uzoefu wa njia tofauti za maisha. 

9.Baini kabla ya kufika 

Kabla ya safari yako, fahamu kuhusu unakokwenda. Hii itakuruhusu kuzama vyema katika mila na desturi za mahali hapo na kuthamini maeneo au desturi ambazo pemngine ungezikosa.  

Ukiwa na maelezo sahihi, unaweza kuchunguza unakoenda kwa busara zaidi na kufurahia matukio na kubaini mambo mapya. 

Wapanda miliwa wawili wakiwa kwenye milima ya Chile
Unsplash/Toomas Tartes

 

10. Tembelea hifadhi za taifa na mihadhara 

Kuchunguza asili na wanyamapori katika mbuga za kitaifa ni njia ya kuingia ndani ya wanyama na mifumo yao ya ikolojia.  

Wakati mwingine bei ya tiketi yako ya kuingia inasaidia aina na juhudi za kuhifadhi mazingira na husaidia kuhifadhi maeneo haya asilia. 

11. Usiache alama 

Unaweza kuhitimisha safari yako kwa kuondoka bila kuacha alama yoyote katika eneo lako la likizo.  

Weka takataka zako kwenye vyombo vilivyotolewa kwa madhumuni haya na usiondoe au kurekebisha chochote kwenye eneo ulipofikia bila idhini.  

Hebu tuhakikishe tunaacha nyayo za busara tu, na haswa sio kwenye mazingira. 

12. Waambie marafiki zako 

Sasa kwa kuwa uko tayari kusafiri kwa kuzingatia mazingira, usisite kueneza neno hilo!.  

Waelimishe watalii wenzako, marafiki na familia kuhusu jinsi utalii endelevu unavyowanufaisha wenyeji kwa kuboresha maisha na ustawi wao, na kutunufaisha sote kwa kulinda mazingira yetu mazuri.