UNWTO yatangaza orodha ya vijiji 32 Bora vya Utalii duniani
UNWTO yatangaza orodha ya vijiji 32 Bora vya Utalii duniani
Kutoka Austria hadi Vietnam, maeneo 32 kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni yametajwa kuwa 'Vijiji Bora vya Utalii kwa mwaka 2022' na Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UNWTO).
Tuzo hiyo inatambua maeneo ya vijijini ambayo yanakumbatia utalii kama kichocheo cha maendeleo na fursa mpya za ajira na mapato, huku kikihifadhi na kukuza maadili na bidhaa za kijamii.
Katibu Mkuu wa UNWTO Zurab Pololikashvili amesema “Kwa jamii za vijijini kila mahali, utalii unaweza kuwa jambo la kuleta mabadiliko ya kweli katika kutoa ajira, kusaidia biashara za ndani na kudumisha uhai wa mila. Vijiji Bora vya Utalii na UNWTO vinaonyesha uwezo wa sekta ya kuendeleza mseto wa kiuchumi na kuunda fursa kwa wote nje ya miji mikubwa.”
Mpango huu wa utambuzi wa vijiji wa UNWTO unatambua vijiji kwa kujitolea kwao katika uvumbuzi na uendelevu katika nyanja zake zote za kiuchumi, kijamii na kimazingira pamoja na kuzingatia kuendeleza utalii kwa kuzingatia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Kwa mwaka huu wa 2022, jumla ya vijiji 32 kutoka nchi 18 katika kanda tano za ulimwengu vilipewa tuzo hiyo. Vijiji hivi vilifanyiwa tathmini na Bodi huru ya ushauri kwa kuzingatia vigezo vinavyojumuisha maeneo tisa ambavyo ni:
- Utamaduni na Maliasili
- Ukuzaji na Uhifadhi wa Rasilimali za Utamaduni
- Uendelevu wa Kiuchumi
- Uendelevu wa Kijamii
- Uendelevu wa Mazingira
- Maendeleo ya Utalii yaliyounganishwa na mnyororo wa thamani
- Utawala ulioweka kipaumbele kwenye Utalii
- Miundombinu iliyounganishwa
- Afya, Usalama na Ulinzi.
Katika toleo la mwaka huu jumla ya vijiji 136 vilipendekezwa kutoka nchi 57 wanachama wa UNWTO. Kila nchi mwanachama inaweza kuteua vijiji vitatu. Kutoka katika orodha hiyo 32 vilitambuliwa kama Vijiji Bora vya Utalii na UNWTO. Vijiji hivyo ni
- Zell am See, Austria
- Wagrain, Austria
- Puqueldón, Chile
- Dazhai, China
- Jingzhu, China
- Choachí, Colombia
- Aguarico, Ecuador
- Angochagua, Ecuador
- Choke Mountains Ecovillage, Ethiopia
- Mestia, Georgia
- Kfar Kama, Israel
- Sauris-Zahre, Italia
- Isola del Giglio, Italia
- Umm Qais, Jordan
- Creel, Mexico
- El Fuerte, Mexico
- Ksar Elkhorbat, Morocco
- Moulay Bouzerktoune, Morocco
- Lamas, Peru
- Raqchi, Peru
- Castelo Novo, Ureno
- Pyeongsa-ri, Korea Kusini
- Rasinari, Romania
- AlUla Old Town, Saudi Arabia
- Bohinj, Slovenia
- Rupit, Hispania
- Alquézar, Hispania
- Guadalupe, Hispania
- Murten, Uswisi
- Andermatt, Uswisi
- Birgi, Türkiye
- Thái Hải, Vietnam
Mbali na kutangazwa kwa vijijini 32 bora, vijiji vingine 20 vitaingia kwenye program ya maboresho.
Vijiji vyote 52 pia vitakuwa sehemu ya mtandao Bora wa Kimataifa wa Vijiji vya Utalii wa UNWTO ulioundwa mwaka 2021 ambao umelenga kukusanya vijiji 115 kutoka mabara matano.
Mtandao huo unamanufaa kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo ana kwa ana na kw anjia ya mtandao, vijiji hivyo vitaweza kushirikishana uzoefu wa yale yanayofanya kazi vizuri katika maeneo mbalimbali pamoja na utambuzi wa chapa ya kimataifa na uhamasishaji.
Vijiji hivyo 20 ni
- Trevelin, Argentina
- Krupa na Vrbasu, Bosnia-Herzegovina
- Fontainhas, Cabo Verde
- Ninhue, Chile
- San Vicente de Chucuri, Colombia
- Barichara, Colombia
- Kalopanagiotis, Cyprus
- Pissouri, Cyprus
- Adaba, Ethiopia
- Khonoma, India
- Neot Semadar, Israel
- Otricoli, Italy
- Il Ngwesi, Kenya
- Grand Baie, Mauritius
- Bella Vista, Paraguay
- Istebna, Poland
- Ferraria de São João, Portugal
- Castara, Trinidad and Tobago
- Anıtlı, Türkiye
- Cumalıkızık, Türkiye
Utalii kama kichocheo cha maendeleo vijijini na ushirikishwaji
Mpango wa Vijiji Bora vya Utalii ni mradi mkuu wa Mpango wa Maendeleo ya Utalii wa UNWTO kwa Maendeleo Vijijini.
Mpango huu unalenga kuhakikisha utalii unachangia katika kupunguza ukosefu wa usawa wa kikanda katika mapato na maendeleo, kupambana katika kupungua idadi ya watu wanao ondoka vijijini, kuendeleza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na vijana, kuendeleza ubunifu na digitali, kuboresha mawasiliano, miundombinu, upatikanaji wa fedha na uwekezaji, ubunifu katika maendeleo ya bidhaa na thamani, kuongeza mnyororo wa thamani, kukuza mazoea endelevu ya matumizi bora ya rasilimali na kupunguza uzalishaji na upotevu na kuimarisha elimu na ujuzi.
Mpango huu unalenga kukuza utawala bora wenye ushirikiano wa ngazi mbalimbali na unaowashirikisha wadau mbalimbali kwa ajili ya kuwawezesha wanajamii.