Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lengo la kihistoria la ndege zisizozalisha hewa ukaa  lakubaliwa katika mkutano wa ICAO

Ndege nada 747 ya shrika la ndege la Uingereza ikijiandaa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa O'Hare
Unsplash/Patrick Campanale
Ndege nada 747 ya shrika la ndege la Uingereza ikijiandaa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa O'Hare

Lengo la kihistoria la ndege zisizozalisha hewa ukaa  lakubaliwa katika mkutano wa ICAO

Tabianchi na mazingira

Nchi wanachama wa shirika la kimataifa la usafiri wa anga (ICAO) Ijumaa wamepitisha lengo la muda mrefu la kutozalisha kabisa hewa ukaa ifikapo mwaka 2050, kufuatia wiki mbili za za mkutano wa kikao cha kidiplomasia cha 41 cha Baraza kuu la shirika hilo.

Lengo la usafiri wa anga, usiozalisha kabisa hewa ukaa unaofuata ahadi kama hizo kutoka kwa makundi ya tasnia hiyo, "litachangia ubunifu unaojali mazingira na kasi ya utekelezaji, ambayo lazima iharakishwe katika miongo ijayo ili kufikia safari za ndege zisizozalisha hewa chafuzi," amesisitiza Rais wa Baraza la ICAO Bwana Salvatore Sciacchitano.

Ameongeza kuwa ili kufikia lengo hili, hatua kadhaa za kupunguza uzalishaji wa CO2 zitahitajika kutekelezwa, kama vile kuharakishwa kwa teknolojia mpya na bunifu za ndege, kurahisisha uendeshaji wa safari za ndege, na kuongezeka kwa uzalishaji na usambazaji wa nishati endelevu ya anga.

Suala la ufadhili unaowezekana na msaada wa uwekezaji kwa hatua hizi limesisitizwa na nchi zilizowakilishwa katika Baraza hilo na kulikuwa na wito wa mkutano wa tatu wa ICAO kuhusu usafiri wa anga na mafuta mbadala uitishwe mwaka wa 2023.

Wakati uzalishaji wa hewa ukaa unaotokana na uendeshaji wa anga unajumuishwa katika ahadi za kimazingira zilizotolewa na takriban nchi zote katika mkataba wa Paris  ambao ni mkataba wa kimataifa unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, uliopitishwa mwaka 2015.

Uzalishaji unaotokana na safari za ndege za kimataifa unashughulikiwa kwa pamoja chini ya mkataba wa Chicago, ambao ulianzisha sheria za anga mwaka 1947, na mikataba inayohusiana.

Tangu 1944, ICAO imesaidia nchi kushirikiana na kushiriki anga zao kwa manufaa yao ya pande zote. 

Tangu lilipoanzishwa,shirika hilo limeunga mkono uundaji wa mtandao unaotegemewa wa usafiri wa anga duniani, ambao unaunganisha familia, tamaduni, na biashara kote ulimwenguni, huku ukikuza ukuaji endelevu na ustawi wa kijamii na kiuchumi popote ndege zinaporuka.

Mataifa ndiyo yanayofanya maamuzi katika hafla za Baraza Kuu la ICAO, lakini majadiliano na matokeo ya kimataifa, kama vile lengo la kutozalisha kabisa hewa ukaa ifikapo 2050, yanatokana na michango muhimu kutoka kwa sekta na mashirika ya kiraia, ambayo hushiriki kama waangalizi rasmi.