Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

 Sekta ya ujenzi yaenda kombo katika kutozalisha kabisa hewa ukaa ifikapo 2050:UNEP Ripoti

Wanaume wakiwa kazini katika ujenzi wa barabara mpya Albania
World Bank/Albes Fusha
Wanaume wakiwa kazini katika ujenzi wa barabara mpya Albania

 Sekta ya ujenzi yaenda kombo katika kutozalisha kabisa hewa ukaa ifikapo 2050:UNEP Ripoti

Tabianchi na mazingira

Kushamiri kwa sekta ujenzi kimataifa kumesukuma uzalishaji wa hewa ukaa au CO2 wa sekta hiyo hadi kiwango cha juu cha gigatani 10, ikimaanisha kuwa sasa sekta hilo imekwenda kombo haijafanikiwa kufikia ahadi za utokomezaji wa hewa ukaa ifikapo mwaka 2050, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira (UNEP). 

Katika taarifa iliyotolewa leo na shirika hilo Inger Andersen, mkurugenzi Mtendaji wa UNEP amesema."Miaka ya maonyo kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi sasa yametimia. Ikiwa hatutapunguza kwa haraka uzalishaji wa gesi chafuzi kulingana na Mkataba wa Paris, tutakuwa katika matatizo makubwa." 

Sekta inayotumia nishati kubwa 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa leo na UNEP, zaidi ya asilimia 34 ya mahitaji ya nishati duniani mwaka 2021 yalitoka katika sekta hiyo, pamoja na karibu asilimia 37 ya nishati na uzalishaji unaohusiana na mchakato wa hewa ukaa. 

Takwimu zilizotolewa na ripoti hiyo ya UNEP kabla ya mkutano wa mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa COP27 nchini Misri, pia zimegundua kuwa uzalishaji wa hewa ukaa mwaka 2021 ulikuwa juu kwa asilimia tano kuliko mwaka 2020 na asilimia mbili zaidi ya kilele cha kabla ya janga la COVID 19 mwaka 2019. 

Hii ilikuwa licha ya ongezeko la asilimia 16 la uwekezaji kwa ajili ya ujenzi mpya wenye ufanisi wa nishati, wa hadi dola bilioni 237, ambazo UNEP ilieleza kuwa zimezidiwa na ongezeko la nafasi ya sakafu inayojengwa. 

Mwaka 2021, mahitaji yakupasha joto nyumba, mfumo wa viyoyozi, taa na vifaa katika majengo yaliongezeka kwa karibu asilimia nne kutoka mwaka 2020 na asilimia tatu kutoka 2019, limesema shirika la UNEP  likionyesha kuwa pengo kati ya utendaji wa mabadiliko ya tabianchi wa sekta hiyo na hitaji la kupunguza hewa ukaa ifikapo 2050 linaongezeka.  

Benki ya dunia nafanyakazi kwa karibu na baadhi ya miji mikubwa ya China ili kusaidia kupunguza msongamano wa magari barabarani na utoaji wa hewa chafuzi
World Bank
Benki ya dunia nafanyakazi kwa karibu na baadhi ya miji mikubwa ya China ili kusaidia kupunguza msongamano wa magari barabarani na utoaji wa hewa chafuzi

Kupanda kwa bara la Afrika 

Kwa mtazamo wa kikanda wa ripoti hiyo UNEP imebainisha kuwa Afrika inatazamiwa kuwa na matumizi ya rasilimali ghafi, maradufu ifikapo mwaka 2060, huku ikikadiriwa kuwa asilimia 70 ya majengo kwa mwaka 2040 bado yako kwenye ubao wa kuchorea. 

Hii ni kwa mujibu wa makadirio kwamba idadi ya watu barani Afrika inatazamiwa kufikia bilioni 2.4 ifikapo mwaka 2050, asilimia 80 wakiishi mijini, na sababu kwa nini bara hilo linaweza kutumia vyanzo vyake vya nishati mbadala ili kujenga majengo yake kwa uendelevu, imesema UNEP  

"Chuma au nondo, kokoto na saruji tayari ni wachangiaji wakuu katika uzalishaji wa gesi chafuzi limeeleza shirika hilo na kuongeza kuwa vifaa vya ujenzi tayari vinachangia karibu asilimia 9% ya uzalishaji wa hewa ukaa unaotokana na nishati katika bara hilo.” 

Matatizo ya Ulaya 

Kwa Ulaya, UNEP imebainisha kuwa sekta ya majengo inachangia asilimia 40 ya mahitaji yote ya nishati ya Ulaya, na kwamba asilimia 80 ya hiyo inatokana na nishati ya mafuta.  

"Hii inafanya sekta hiyo kuwa eneo la linalohitaji hatua za haraka, uwekezaji, na sera za kukuza usalama wa nishati wa muda mfupi na muda mrefu," amesema Bi Andersen. 

Ili kupunguza uzalishaji wa hewa chafu kwa ujumla, shirika hilo la Umoja wa Mataifa ulimeeleza kuwa sekta ya ujenzi inaweza kusaidia kwa: 

• Kuboresha utendaji wa nishati ya majengo; 

• Kupunguza kiwango cha hewa ukaa cha nyenzo za ujenzi; 

• Kuzidisha ahadi za sera pamoja na hatua, hasa kwa kuzingatia kupanda kwa gharama za mafuta yanayohusishwa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na vivutio vya wazi vya uwekezaji wa ufanisi wa nishati. 

Mitindo muhimu ya kimataifa iliyotambuliwa na UNEP imeonyesha kuwa ongezeko la vyumba vya ujenzi kati ya 2015 na 2021 ilikuwa sawa na jumla ya eneo la ardhi lililofunikwa katika majengo nchini Ujerumani, Ufaransa, Italia na Uholanzi.