Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali zachagizwa kuwekeza katika michezo kuimarisha afya:WHO 

Michezo ya olimpiki kuanza rasmi Julai 23, 2021.
© 2021 - IOC/Yuichi Yamazaki
Michezo ya olimpiki kuanza rasmi Julai 23, 2021.

Serikali zachagizwa kuwekeza katika michezo kuimarisha afya:WHO 

Afya

WHO imezindua ripoti mpya inayotoa wito kwa serikali, mamlaka za michezo na wadau wa michezo kwenye jamii kuongeza uwekezaji katika matukio makubwa ya na kuchochea hamasa kutokana na michezo hiyo kama njia mojawapo ya kuimarisha afya kwenye jamii. 

Uzinduzi huo umefanyika leo huko Geneva, Uswisi wakati wa mkutano wa ngazi ya juu kuhusu ugunduzi kwenye michezo, WISH.  

Ripoti hiyo , “Kucheza muda mrefu; Mfumo wa kukuza mazoezi ya kimwili kupitia matukio makubwa ya michezo”, inapendekeza njia za kuimarisha urithi wa matukio makubwa ya michezo ili ziweze kuchangia kwa ufanisi zaidi katika kuongeza mazoezi ya kimwili, na kuboresha afya ya watu. 

"Matukio makubwa ya michezo ni fursa muhimu za kukuza afya na manufaa ya kijamii ya mazoezi ya kimwili na michezo, na kuhakikisha urithi wa afya wa kudumu kwa vizazi. Lakini matukio ya michezo mara nyingi hukosa fursa za kuleta mabadiliko endelevu. Ripoti ya “Playing the Long Game” inasisitiza jinsi kujifunza kutoka kwenye matukio ya zamani na mipango mizuri kunaweza kuweka misingi ya afya na urithi endelevu wa michezo." amesema Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO

Ameongeza kuwa “Mazoezi ya mara kwa mara ya kimwili, ikiwa ni pamoja na kucheza michezo, imethibitishwa kusaidia kuzuia na kutibu magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) kama vile ugonjwa wa moyo, kiharusi, kisukari na saratani ya matiti na utumbo. Pia husaidia kuzuia kupunguza shinikizo la damu, uzito kupita kiasi na unene na inaweza kuboresha afya ya akili na ustawi. Kuongezeka kwa ushiriki wa michezo na mazoezi ya mwili kunaweza kuokoa maisha, kuboresha afya na kusaidia mifumo ya afya na jamii zenye nguvu zaidi, thabiti zaidi.” 

 

Mazoezi husaidia kuzuia magonjwa yasiyo ya kuambukiza 

Leo, mtu 1 kati ya watu wazima 4 na vijana 4 kati ya vijana 5 wanabweteka, na kusababisha ugonjwa wa utipwatipwa sana na magonjwa mengine makubwa yasiyo ya kuambukiza.  

Wataalamu kutoka WHO wanaonya kuhusu hili huku wakipendekeza michezo ya viuongo kama gymnastics, kukimbia, kuogelea na kucheza michezo mingine. Wataalamu hao wa WHO wana matumaini makubwa kwa matukio makubwa ya michezo, ambayo, kwa maoni yao, yanapaswa kuzalisha maslahi ya umma katika michezo. 

Wataalamu wanaamini kwamba hali hiyo inaweza kubadilishwa na matukio makubwa zaidi ya michezo ya kimataifa kama mashindano ya Olimpiki, soka au michuano ya michezo ya kwenye barafu, mashindano ya kitaaluma ya tenisi, na kadhalika. 

Matukio haya huvutia mamilioni ya watazamaji na uwekezaji mkubwa. Wanaweza kusaidia kueneza taarifa kuhusu faida za michezo na shughuli za kimwili.  

Hata hivyo, kulingana na WHO, kwa sasa hakuna mikakati ya kimataifa katika suala hili, hakuna viashiria vya kawaida vya kutathmini athari za matukio makubwa zaidi ya michezo kwa idadi ya watu. 

"Miji mingi inayoandaa hafla kuu za michezo ina mipango kabambe ya kutumia hafla hizi kuongeza mazoezi ya mwili na kuboresha afya ya umma. Lakini bado hatuwezi kupima athari kwani hakuna takwimu ya athari hizio," amesema Didi Thompson, mkurugenzi wa utafiti na maudhui wa mkutano wa dunia wa ubunifu wa afya (WISH).