Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Barubaru wanne kati ya watano, wanashindwa kufanya mazoezi kwa hata dakika sitini kwa siku-WHO

Shirika la afya duniani WHO linawachagiza vijana barubaru kufanya mazoezi ya viungo na zaidi kwa ajili ya afya na mustakabali wao
Unsplash/Paul Proshin
Shirika la afya duniani WHO linawachagiza vijana barubaru kufanya mazoezi ya viungo na zaidi kwa ajili ya afya na mustakabali wao

Barubaru wanne kati ya watano, wanashindwa kufanya mazoezi kwa hata dakika sitini kwa siku-WHO

Afya

Umoja wa Mataifa umesema hali ya kutisha ya kukosa kufanya mazoezi miongoni mwa vijana  barubaru kote duniani inaweka hatarini hali yao ya kiafya katika siku zijazo za utu uzima wao.

Katika utafiti wa kwanza wa aina yake kuhusu mwenendo wa kimataifa na wa kikanda kati ya watu wa umri wa miaka 11 na 17, Shirika la afya ulimwenguni WHO kupitia taarifa yake iliyotolewa hii leo mjini Geneva Uswisi, limesema kwamba takribani asilimia 80 ya vijana barubaru wa umri tajwa wanashughulika kwa chini ya dakika 60 kwa siku hali ambayo  kwa hakika ni pendekezo la chini la kila siku.

Wavulana wa Ufilipino na wasichana wa Korea Kusini waongoza kwa kutofanya mazoezi

Kwa mujibu wa utafiti huo, Wafilipino wamekuwa na kiwango cha juu cha kutofanya mazoezi miongoni mwa wavulana kwa kuwa na kiwango cha asilimia 93 wakati nchini Korea Kusini, watafiti wamegundua kuwa asilimia 97 ya wasichana walishindwa kufanya mazoezi ya kiwango cha kutosha.

Kwa upande wa jinsia, kwa wastani, asilimia 85 ya wasichana walishindwa kufanya mazoezi ya kutosha kote duniani  ikilinganishwa na asilimia 78 ya wavulana.

Dkt Leanne Riley ambaye ni mmoja wa watafiti, anasema, “tangu mwaka 2001 hadi mwaka 2016, tulibaini kwamba hakukuwa na maendeleo yoyote huu ya kuwa na saa moja tu katika maisha yao kila siku kuweza kufanya  mazoezi ya mwili ili kupata faida za kiafya kutokana na mazoezi ya viungo. Hayo yanaweza  kufanyika kwa muda kidogo tu tofautitofauti ili mradi kufikisha dakika 60.”

Ili kuimarisha hali hiyo ya barubaru kufanya mazoezi Dkt. Fiona Bull mwandishi mwenza wa ripoti hiyo anasema “Nchi zinapaswa kuweka au kurekebisha sera zake ili kuongeza rasilimali zinazohitajika katika kuongeza mazoezi ya viungo. Sera hizo lazima zijumuishe mifumo yote ya mazoezi ya viungo ikiwa ni pamoja na kupitia elimu ya viungo ambayo inaelimisha, michezo Zaidi na fursa za burudani pia kuweka mazingira salama ili vijana wadogo waweze kutembea ama kuendesha baiskeli peke yao. Hatua za kina zinahitaji kushilikisha sekta na wadau mbalimbali zikiwemo shule, familia, michezo, mipango miji na viongozi wa kijamii.”

Bibi kizee akiendesha baiskaeli nchini Croatia (13 Februari 2013). Mwongozo mpya wa WHO unasisitiza mazoezi ili kujikinga na ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu.
World Bank/Miso Lisanin
Bibi kizee akiendesha baiskaeli nchini Croatia (13 Februari 2013). Mwongozo mpya wa WHO unasisitiza mazoezi ili kujikinga na ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu.

Haihitaji mazoezi mazito ili kupata faida za kiafya

Akisisitiza kuwa mazoezi ya mwili si lazima yawe makali ili kuwa ya faida, Dkt Riley anasema kwamba kukimbia, kutembea, kuendesha baiskeli au hata kujaribu kuchangamka, kunaweza kuleta tofauti chanya.

Taarifa ya WHO inaonya kuwa kushindwa kufanya mazoezi ya kutosha, kunaacha watu katika hatari ya kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza na hata yanayozuilika.