Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki ya Uhuru wa kujieleza Somalia mashakani, wanahabari na watetezi wa haki matatani- Ripoti

Isha Dyfan akizungumza na wanahabari mwishoni mwa ziara yake SOmalia mapema mwaka huu.
UN Photo / Fardosa Hussein
Isha Dyfan akizungumza na wanahabari mwishoni mwa ziara yake SOmalia mapema mwaka huu.

Haki ya Uhuru wa kujieleza Somalia mashakani, wanahabari na watetezi wa haki matatani- Ripoti

Haki za binadamu

Isha Dyfan, Mtaalam Huru wa hali ya haki za binadamu nchini Somalia, hii leo jijini Geneva, Usiwisi akiwasilisha ripoti ya hali ya haki za binadamu nchini Somalia, amelieleza Baraza la Haki za Binadamu  la Umoja wa Mataifa kuwa ripoti za matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu nchini Somalia zinatia wasiwasi mkubwa.

Ripoti hii inahusu kipindi cha kuanzia tarehe 1 Julai 2021 hadi tarehe 30 Juni 2022. Inalenga zaidi kuhusu kutathmini hali ya haki za binadamu nchini dhidi ya vigezo vya maendeleo katika kuboresha hali ya haki za binadamu.

Wanahabari na watetezi wa haki za binadamu wako matatani

Akifafanua kuhusu vitisho hivyo, amesema vikosi vya usalama vinatoa vitisho, vinanyanyasa, vinakamata kiholela na kusweka rumande waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu bila kusahau kufunguliwa mashtaka sambamba na kuendelea kutumika kwa sheria ya mwaka 1964 ya makosa ya jinai ambayo inalinda vitendo vya ukiukwaji  haki za binadamu vinavyotekelezwa na vikosi vya usalama.

Ametolea mfano ripoti ya vyombo vya habari yam waka 2021 ambamo chama cha wanahabari Somalia NUSOJ kiliripoti matukio mawili ya mauaji ya waandishi wa Habari mjini Mogadishu na Galkayo na matukio mengine 63 ikiwemo mashambulio ya kimwili, manyanyaso, kukamatwa kinyume cha sheria na uonevu kwa njia ya mtandao.

“Ripoti hiyo pia ilinakili matukio 13 ya mashambulio ya kikatili ambamo kwayo manne yalihusisha wanahabari wa kike. Nalaani vitendo hivi na vinginevyo vinavyodhibiti uhuru wa kujieleza,” amesema Bi. Dyfan.

Bi Dyfan (wa tatu kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na maafisa kutoka serikali ya jimbo la Kusini-Magharibi nchini Somalia wakati wa ziara yake huko Baidoa mwezi Machi mwaka huu wa 2022.
UN ./Mohamednor Abdikadir
Bi Dyfan (wa tatu kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na maafisa kutoka serikali ya jimbo la Kusini-Magharibi nchini Somalia wakati wa ziara yake huko Baidoa mwezi Machi mwaka huu wa 2022.

Kipi kifanyike uhuru wa kujieleza uweko Somalia?

Mtaalamu huyo amesema ili uhuru wa kujieleza uliowekwa bayana kwenye Katiba ya Muda ya Somalia ya mwaka 2012, ni lazima serikali ichukue hatua za dharura kupitisha sheria ya vyombo vya habari kwa mujibu wa Katiba ya Muda ya serikali  ya shirikisho na viwango vya kimataifa na kikanda vya haki za binadamu. Halikadhalika kurekebisha sheria zinazoharamisha kazi za waandishi wa habari na vyombo vya habari, na kuhakikisha uwajibikaji.

Hata hivyo amekaribisha hatua ya tarehe 18 mwezi uliopita wa Septemba ya kukamatwa kwa askari wawili waliotuhumiwa kushambulia na kujeruhi mwanahabari tarehe 21 mwezi Agosti mwaka 2022 wakati wakiandika habari kuhusu kutekwa kwa Hotel ya Hyatt mjini  Mogadishi.

“Nahamasisha serikali kuchukua hatua haraka kwenye ahadi yake ya kuimarisha haki na kuzuia vitendo kama hivyo siku za usoni,” amesema Bi. Dyfan.

Ukame na haki za binadamu

Kuhusu hali ya ukame na haki za binadamu, Mtaalamu huyo amesema ukosefu wa mvua umesababisha sio tu ukame usio na kifani katika takribani asilimia 90 ya wilaya za Somalia bali pia imezua mzozo wa kibinadamu kwa zaidi ya watu milioni saba ambao wanakumbwa na uhaba wa chakula. Watoto wanakabiliwa na utapiamlo mkali, na kuongezeka kwa mapigano juu ya rasilimali chache zaidi.

Bi. Dyfan amesema mapigano hayo yanasababisha kuhama kwa watu wengi na kuongezeka kwa unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto.

Aidha Bi. Dyfan ameeleza kuwa kuna hitaji la dharura la kuhakikisha ufadhili wa kutosha na endelevu ambao unazidi misaada ya haraka ya kuokoa maisha na kibinadamu kuelekea shughuli endelevu ili kuzuia shida hii ya mara kwa mara.

Wachangiaji nao wakatoa maoni yao, Somalia iungwe mkono zaidi

Katika mjadala kuhusu nchi hiyo ya pembe ya Afrika, Somalia, baadhi ya wazungumzaji wamesema kwamba ingawa matukio machache mazuri yametokea, wasiwasi unabakia kuhusu amani, usalama na changamoto za kibinadamu ambazo zinaendelea nchini Somalia.

Baadhi ya wazungumzaji wamesema kunapaswa kuwa na uungwaji mkono wa dhati kwa Serikali katika kukabiliana na dharura ya ukame, na jumuiya ya kimataifa inapaswa kuongeza maradufu juhudi zake za kusaidia njia ya kurejesha amani nchini Somalia, katika wakati wa migogoro inayoongezeka duniani.

Msemaji mmoja amesema, Baraza lisipitishe maazimio mengine zaidi kuhusu Somalia na badala yake Mtaalam Huru atekeleze mamlaka yake ndani ya masharti ya kanuni za maadili.

Wachangiaji wa mada

Waliozungumza katika mjadala kuhusu Somalia ni Muungano wa Ulaya, Saudi Arabia kwa niaba ya kundi la nchi, Qatar, Sudan Kusini, Senegal, Misri, Ireland, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, Ufaransa, Ethiopia, Australia, Venezuela, Urusi, China, Marekani, Sri Lanka, Uingereza, Sierra Leone, Burundi, Yemen, Sudan, Eritrea, Botswana, Luxembourg, Bahrain, Saudi Arabia, Iceland kwa niaba ya kundi la nchi, na Mauritania.