Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yataka mahitaji ya kibinadamu, haki na uhuru vipewe kipaumbele Afghanistan

Wanahabari Nchini Afghanistan katika siku ya Uhuru wa vyombo na wanahabari mwezi Machi mwaka uliopita
UNAMA/Fardin Waezi
Wanahabari Nchini Afghanistan katika siku ya Uhuru wa vyombo na wanahabari mwezi Machi mwaka uliopita

UN yataka mahitaji ya kibinadamu, haki na uhuru vipewe kipaumbele Afghanistan

Haki za binadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa leo yamepaza sauti yakitaka mahitaji ya kibinadamu, haki, usalama na uhuru wa vyombo vya Habari vipewe kipaumbele nchini Afghanistan. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limeonya kwamba mahitaji ya kibinadamu nchini Afghanistan asilani yasisahaulike.  

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wa shirika hilo shabia Mantoo mjini Geneva Uswis hii leo UNHCR inatiwa wasiwasi mkubwa na hali ya kibinadamu kwa maelfu ya raia ndani ya Afghanistan na imetaka msaada utolewe ili wote wanaouhitaji wasisahaulike.

Hali nchi nzima bado ni tete ingawa mapigano yamepungua kiasi tangu Taliban kuchukua mamlaka Jumapili iliyopita. Hata hivyo shirika hilo limesema athari za mzozo huo bado haziko bayana huku raia wengi wakihofia mustakbali wao. 

 Uhuru na usalama wa waandishi wa Habari 

Kwa upande wake shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO leo limetoa wito wa kutaka uhuru wa kujieleza na usalama wa waandishi wa Habari lazima uheshimiwe na kuhakikishwa nchini Afghanistan kwa kuzingatia .

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay ametoa wito huo leo ijumaa na kusisitiza kwamba "Ufikiaji wa habari za kuaminika na mjadala wa wazi kwa umma, kupitia vyombo huru vya Habari ni muhimu kwa Waafghan ili waweze kuishi katika jamii yenye amani inayostahili. Katika kipindi hiki muhimu, hakuna mtu anayepaswa kuogopa kusema anachofikiria, na usalama wa waandishi wote, haswa wanawake, lazima uhakikishwe.” 

Kundi la wanahabari na watoa msaada wakijikuta katika shambulizi la kujitolea kufa mjini Kabul tarehe 30 April 2018
Reuters/Omar Sobhani
Kundi la wanahabari na watoa msaada wakijikuta katika shambulizi la kujitolea kufa mjini Kabul tarehe 30 April 2018

 Sekta ya Habari yenye nguvu

UNESCO inasema bado imejitolea kuendelea kusaidia uhuru wa kujieleza na kupata habari kwa Waafghan wote kwa kila njia inayowezekana. 

Kwa miongo kadhaa iliyopita, UNESCO imechangia kushamiri kwa sekta mahiri na ya taaluma  pana ya vyombo vya Habari nchini Afghanistan, "ambayo inaendelea kuonyesha kujitolea kwa kiasi kikubwa kunufaisha umma, hata wakati wa vurugu na vitisho". 
Kwa mwaka huu pekee, angalau waandishi wa habari saba, pamoja na wanawake wanne, waliuawa wakiwa kazini, kulingana na takwimu za UNESCO. 

Shirika hilo  la Umoja wa Mataifa linatumai kuwa maendeleo muhimu hayatafutwa na kwamba waandishi wa habari wanawake wanaweza kuendelea na kazi yao muhimu.

“Hususan waandishi wa habari wanawake ni lazima waweze kuendelea na kazi yao muhimu bila vitisho au mashambulizi.” Ameongeza Bi. Azoulay. 

Katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita, kazi ya UNESCO imekuwa ni kusaidia kuunda mifumo mpya ya sheria, kuchangia ukuzaji wa vyombo vya Habari vya jamii, kuboresha elimu ya uandishi wa habari, kukuza usawa wa kijinsia kwenye vyombo vya habari, na pia kuimarisha elimu ya utangazaji.

Hivi karibuni, shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeunga mkono mitandao ya kukagua ukweli na vyombo vya habari ili waweze kutoa ripoti kuhusu changamoto hiyo kwa sababu ya janga la COVID-19 kwa njia ya kitaalam. 
TAGS: UNHCR, Afghanistan, UNESCO vyombo vya Habari, haki za binadami