Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalam wa haki za bindamu wataka hatua kukabiliana na changamoto za uhuru wa kujieleza

David Kaye, mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uendelezaji na ulinzi wa haki za kujieleza na kutoa maoni wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini New Yrok, Marekani tarehe 25 Oktoba 2018
UN /Rick Bajornas
David Kaye, mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uendelezaji na ulinzi wa haki za kujieleza na kutoa maoni wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini New Yrok, Marekani tarehe 25 Oktoba 2018

Wataalam wa haki za bindamu wataka hatua kukabiliana na changamoto za uhuru wa kujieleza

Haki za binadamu

Ikiwa ni miaka ishirini tangu kupitishwa kwa pamoja azimio la haki za binadamu kuhusu uhuru wa kujieleza, mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu maoni na kujieleza, David Kaye pamoja na wataalam wa kikanda wametoa wito kukabiliana na changamoto dhidi ya uhuru wa kujieleza kwa muongo mmoja ujao.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa Jumatano Julai 10, wataalam hao wameelezea kuhusu ukatili unaoendelea na kudhalilishwa kwa waandishi habari, kutishiwa kwa vyombo vya habari na kubinywa kwa uhuru na udhibiti wa kisheria wa kujieleza kwenye mtandao, pamoja na ufuatiliaji usio halali na uwezo wa ufuatiliaji mtandaoni kama changamoto kubwa katika uhuru wa kujieleza.

Wataalam hao kupitia taarifa yao wametoa wito kuwekewa mazingira sahihi kwa waandishi wa habari na wengine wanaoshambuliwa kwa ajili ya kufurahia uhuru wao wa kujieleza nje na ndani ya mtandao.

Wamesisitiza kwamba uhuru wa kujieleza unahitajika kwa ajili ya kutengeneza mazingira ya uhuru, uwazi na ujumuishwaji na hivyo wameyahimiza mataifa kutambua haki ya kupata intaneti kama haki ya kibindamu na kiungo muhimu katika kufurahia uhuru wa kujieleza.

Wito wa wataalam hao pia umesihi kampuni binafsi kuzingatia muongozo wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za biashara na za kibinadamu. Aidha wametoa wito kwa ajili ya ufuatiliaji huru na wadau jumuishi, uwazi na mbinu za kuhakikisha uwajibishaji ambazo zinaweza kufuatilia sheria za faragha ambazo zinaweza kuathiri mtu kufurahia uhuru wa kujieleza.

Taarifa hiyo ya pamoja imetolewa na David Kaye pamoja na shirika la usalama na ushirikiano la Ulaya, OSCE wawakilishi wa uhuru wa vyombo vya habari, shirika la majimbo ya Marekani (OAS) mtaalama huru kuhusu uhuru wa kujieleza na kamisheni ya Afrika kuhusu haki za kibinadamu na mtaalma huru kuhusu uhuru wa kujieleza na ufikiaji wa taarifa.