Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfumo wa kwenye apu ya simu wasaidia kufuatilia dawa bandia

Tarehe 4 mwezi Machi mwaka 2021, mtumishi wa kituo cha dawa akirekodi kidijitali taarifa kuhusu usambazaji wa chanjo kwenye wilaya kwa kutumia bakodi na apu ya simu.
© UNICEF/Habib Kanobana
Tarehe 4 mwezi Machi mwaka 2021, mtumishi wa kituo cha dawa akirekodi kidijitali taarifa kuhusu usambazaji wa chanjo kwenye wilaya kwa kutumia bakodi na apu ya simu.

Mfumo wa kwenye apu ya simu wasaidia kufuatilia dawa bandia

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na wadau wake wametangaza hatua ya kihistoria katika kukabili dawa bandia wakati huu ambapo Rwanda na Nigeria zimekuwa nchi za kwanza barani Afrika kuthibitisha ubora wa chanjo kwa kutumia teknolojia ya GS1 kupitia apu ya simu.

Shirika hilo kupitia wavuti wake inasema habari hizo zinakuja wakati wa uzinduzi wa TRVST ambao ni ubia mpya wa mfumo wa kufuatilia na kuthibitisha bidhaa za kiafya na ufuatiliaji huo unafanyika katika mnyororo mzima wa usambazaji wa chanjo.

Ubia huo unatekelezwa kwa ushirikiano uitwao VTI ambao ni baina ya UNICEF, ubia wa chanjo duniani, (GAVI), Mfuko wa Bill na Melinda Gates, USAID, mamlaka za udhibiti za kitaifa Nigeria na Rwanda, Vital Wave na Benki ya Dunia.

“Lengo la VTI ni kuongeza uratibu wa dunia na hatua dhidi ya bidhaa bandia za matibabu, hasa katika nchi za kipato cha chini na cha kati,” inasema chapisho hilo la UNICEF.

Mgonjwa akimeza dawa ya Malaria nchiin Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. Mfumo wa TRVST unatarajiwa kusambaa na kusaidia kuthibitisha ubora, viwango na ufanisi wa dawa na chanjo.
UNICEF/UN0Gwenn Dubourthoumieu
Mgonjwa akimeza dawa ya Malaria nchiin Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. Mfumo wa TRVST unatarajiwa kusambaa na kusaidia kuthibitisha ubora, viwango na ufanisi wa dawa na chanjo.

Gharama ya dawa bandia duniani

Yakadiriwa kuwa watoto 169,000 wenye umri wa chini ya miaka 5 hufariki dunia kutokana na kunywa dawa bandia ili kutibu vichomi au Pneumonia, ilhali wengine  116,000 walikufa kwa kunywa dawa bandia wakati wanaugua Malaria.

Usambazaij wa chanjo dhidi ya coronavirus">COVID-19 ulivyoshika kasi duniani kote, vivyo hivyo uzalishaji wa chanjo bandia na za kiwango cha chini pamoja na dawa nyinginezo.

Kabla ya kutangazwa kwa janga la COVID-19, bidhaa 1 ya tiba kati ya 10 katika nchi za kipato cha chini na kati ziliripotiwa kuwa kiwango cha chini au bandia, na hivyo kusababisha madhara kwa wagonjwa na kushindwa kutiba magonjwa ambayo mgonjwa alibainika kuugua.

Bidhaa hizi, sit u zilichangia katika usugu wa vijiumbe maradhi, bali pia zilisababisha watu kukosa imani na dawa, watoa huduma za afya na mifumo ya afya.

“Ziligharimu dola bilioni 200 kila mwaka na dola bilioni 30 katika nchi za vipato vya chini na kati,” limesema chapisho hilo.

Ubia wa kimataifa kuongeza usalama wa mgonjwa

Kwa kutambua changamoto hizo, UNICEF na wadau wa VTI wamekuwa wakishirikiana kupanua wigo wa mpango wa kuthibitisha ubora wa chanjo na dawa.

Wanafanya hivyo kwa kujenga mfumo huo wa ufuatiliaji na uthibitishaji wa dawa au  TRVST. Mpango huo ni matokeo ya kazi ya miaka miwili, ulioleta wadau kutoka mamlaka za udhibiti za kitaifa katika nchi za kipato cha chini na kati, watengenezaji wa chanjo, sekta binafsi na wadau wa maendeleo.

“Bidhaa za dawa za kiwango cha chini au bandia zinazidi kuwa suala la kimataifa, zikiwa ni hatari na tisho kiafya, kiuchumi na kijamii. Zinatishia maisha ya wale ambao tunatakiwa kuwalinda,” amesema Etleva Kalili, Mkurugenzi wa Idara ya Usambazaji ya UNICEF.

Amesema ni kwa kutambua hilo, UNICEF inajivunia kuwa mstari wa mbele kwenye juhudi za kimataifa, sambamba na wadau kuhakikisha viwango vya juu vya udhibiti,  na wagonjwa wanapata dawa na chanjo salama, fanisi na zenye ubora.

Mfumo wa TRVST unategemea taarifa zilizomo kwenye bidhaa husika kuanzia taarifa za kiafya, Jina la dawa kimataifa, namba ya kuzalishwa, kundi la bidhaa, tarehe ya kutengenezwa na tarehe ya kuharibika.

TRVST inaruhusu watumiaji wakiwemo wahudumu wa afya, mamlaka za udhibiti na mawakala wa forodha kutumia apu ya kwenye simu kurambaza bakodi ya kwenye bidhaa na kuthibitisha ubora wake papo hapo.

Iwapo kuna changamoto yoyote kwenye uthibitishaji au kuna shuku yoyote juu ya ubora, hatua hiyo inaibua shaka na hivyo taarifa kutumwa moja kwa moja kwa mtengenezaji na mamlaka za udhibiti.

“Lengo letu ni kuwa na uwezo wa kufuatilia mwanzo hadi mwisho chanjo zote kupitia mfumo huu wa kidijitali katika mfumo wa afya ya umma. TRCST itasaidia kujenga uwezo wa nchi katika usambazaji wa chanjo na dawa nyingine zilizo na viwango na salama,” amesema Thabani Maphosa, Mkurenzi Mwendeshaji wa miradi ya kitaifa GAVI.

Mtoto akipatiwa chanjo dhidi ya polio jimboni Borno, nchini Nigeria
UNICEF/UN036155/Page
Mtoto akipatiwa chanjo dhidi ya polio jimboni Borno, nchini Nigeria

Usambazaji wa mfumo wa TRVST barani Afrika

Mwezi Julai mwaka 2022, mfumo wa TRVST ulizinduliwa Nigeria na Rwanda na mfumo huo kuwa wa kihistoria katika hakikisho la usalama wa mgonjwa dhidi ya dawa bandia na zisizo na viwango.

Kampuni ya Johnson & Johnson ilitoa fungu la kwanza la dawa na kujumuishwa kwenye kanzi dawa, na ilianza na chanjo dhidi ya COVID-19 ili kuhakikisha usalama wa wagonjwa na kushughulikia hatari ya kuweko kwa chanjo bandia au chanjo ambazo zilipelekwa eneo ambalo hazikupaswa kupelekwa.

"Ubora wa bidhaa za matibabu nchini sasa una hakikisho kupitia mfumo huu wa ufuatiliaji na uthibitishaji,” amesema Profesa Mojisola Christianah Adeyeye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya kitaifa nchini Nigeria ya Chakula na Dawa.

Kwa upande wake Rwanda kupitia Dkt. Emile Bienvenu, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya kitaifa ya udhibiti wa vyakula na dawa, “mfumo wa TRVST ni nyongeza muhiu katika mfumo wa kitaifa wa mnyororo wa usambazaji wa dawa na mifumo ya afya katika kuimarisha ushirikishanaji fanisi wa data katika mnyororo mzima, ubora wa data na kupunguza gharama ya takwimu.”

Upanuzi wa siku za usoni wa mfumo wa TRVST

Kwa sasa mfum ohuo unatarajiwa kuimaika na kugusa pia chanjo za kwenye ratiba na bidhaa nyingine za kiafya zikiwemo dawa za Virusi vya Ukimwi, VVU, Kifua Kikuu, Afya ya uzazi, Malaria na dawa nyingine muhimu.