Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF walaani shambulio lililoua makumi ya vijana nchini Afghanistan

Wasichana wakisoma vitabu vyao vya kiada katika Kituo cha Elimu cha Dasht-e-Barchi huko Kabul, Afghanistan. (Maktaba)
© UNICEF/Shehzad Noorani
Wasichana wakisoma vitabu vyao vya kiada katika Kituo cha Elimu cha Dasht-e-Barchi huko Kabul, Afghanistan. (Maktaba)

UNICEF walaani shambulio lililoua makumi ya vijana nchini Afghanistan

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya watoto UNICEF limeeleza kusikitishwa kwake na shambulio lililotokea mapema hii leo nchini Afghanistan na kusababisha vifo vya makumi ya wasichana na wavulana pamoja na kujeruhi wengine wengi.

 

Taarifa ya UNICEF kutoka Kabul nchini Afghanistan imesema shambulio hilo limetokea Magharibi mwa Afghanistan katika eneo la Kaaj lililoko wilayani Dasht-e-Barchi ambapo waathiriwa walikuwa wakifanya mazoezi ya mtihani wa kuingia chuo kikuu.

UNICEF imetuma rambirambi zake kwa familia zilizoathiriwa na tukio hilo na kuwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Taarifa hiyo pia imeeleza “Vurugu ndani au karibu na maeneo ya taasisi za elimu hazikubaliki. Maeneo hayo lazima yawe maeneo yenye amani ambapo watoto wataweza kusoma, kuwa na marafiki zao na kujisikia wapo salama wakati wakiendelea kujijengea ujuzi kwa ajili ya maisha yao ya baadae.”

UNICEF imehitimisha taarifa yake kwa kusisitiza na kukumbusha kuwa watoto na vijana sio, na hawapaswi kamwe kulengwa na ghasia.

“Kwa mara nyingine tena UNICEF inazikumbusha pande zote nchini Afghanistan kuzingatia na kuheshimu haki za binadamu na kuhakikisha kuna usalama na ulinzi kwa watoto wote na vijana wote”