Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuna wasiwasi na hali ya Iran kufuatia kifo cha Mahsa- OHCHR

Taswira kutoka angani ya mji mkuu wa Iran, Tehran
© Unsplash/Mahyar Motebassem
Taswira kutoka angani ya mji mkuu wa Iran, Tehran

Tuna wasiwasi na hali ya Iran kufuatia kifo cha Mahsa- OHCHR

Haki za binadamu

Kaimu Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Nada Al-Nashif ameeleza wasiwasi wake kufuatia kifo huko nchini Iran kilichomfika msichana mmoja akiwa korokoroni baada ya kuswekwa ndani na polisi kwa madai ya kutovaa hijab inavyotakiwa.

Mahsa Amini alikamatwa wiki moja iliyopita na ‘polisi watunza maadili Iran’.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 22 ambaye jina lake la kikurdi ni Jhina alipoteza fahamu punde tu baada ya kuzirai akiwa kituo cha polisi cha Vozara mjini Tehran na kisha kufariki dunia siku tatu baadaye kutokana na mshtuko wa moyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, USwisi, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za binadamu, Ravina Shamdadani amesema kuna hofu kubwa juu ya nguvu kupita kiasi zinazotumiwa na vikosi vya usalama kufuati akifo cha Bi. Amini.

Maelfu waandamana

Amesema maelfu ya watu wameandamana mitaani kwenye miji mbalimbali nchini Iran, kuanzia Tehrna, Isfahan, Karaj, Mashhad, Rasht, Saqqes na Sanandaj, wakipinga kifo cha Bi. Amini.

“Majeshi ya usalama yameripotiwa kukabili waandamanaji kwa kutumia silaha za moto na mabomu ya  kutoa machozi,” amesema Bi. Shamdasani akizungumza na wanahabari.

Angalau watu wawili wameripotiwa kuuawa na wengine wengi wamejeruhiwa na wengine wamekamatwa.

Bi.Shamdasani pia amegusia sheria iliyopitishwa nchini Iran inayoruhusu polisi kutuma ujumbe mfupi kwa wanawake wakiwa kwenye magari wakiwajulisha kwamba hawapaswi kuvua hijabu wakati wanaendesha gari.

Sheria kuhusu Hijabu haipaswi kuweko

“Suala la msingi ni kwamba sheria hizi hazipaswi kuweko, wanawake hawapaswi kuadhibiwa kwa kile wanachovaa,” amesema afisa huyo.

Amesema wanawake ammbao wanapingwa kanuni za lazima za hijabu hawapaswi kunyanyaswa, hawapaswi kughasiwa na kwamba lazima kufanyike uchunguzi wa haki.

Uchunguzi wa haraka na huru unatakiwa

Bi. Nashif amesema kifo cha msichana huyo mwenye umri wa miaka 22 ni cha kutisha na madai ya kwamba aliteswa lazima yachunguzwe haraka, kwa huru na mamlaka iliyo huru ili kuhakikisha familia yake inatendewa haki.

Kaimu Kamishna huyo amelaani pia matumizi kupita kiasi ya nguvu dhidi ya waandamanaji na kutaka serikali ya Iran ambayo ni mwanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za kiraia na kisiasa kuheshimu  haki za wale wanaotekeleza uhuru na haki yao ya kujieleza na kukutana.

Bi. Al-Nashif pia amerejelea kauli za mara kwa mara za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres juu ya kuendelea kwa ukandamizaji wa haki za watetezi wa haki za wanawake ambao wanapinga kuvaa hijabu.