Kifo cha Mahsa: UN yaingiwa hofu ya matumizi ya nguvu kupita kiasi Iran

Waandamanaji wakiwa wamekusanyika huko Stockholm nchini Sweden baada ya Mahsa Amini, msichana mwenye umri wa miaka 22  kufa akiwa kituo cha polisi nchini Iran.
Unsplash/Artin Bakhan
Waandamanaji wakiwa wamekusanyika huko Stockholm nchini Sweden baada ya Mahsa Amini, msichana mwenye umri wa miaka 22 kufa akiwa kituo cha polisi nchini Iran.

Kifo cha Mahsa: UN yaingiwa hofu ya matumizi ya nguvu kupita kiasi Iran

Haki za binadamu

Hali ikizidi kuwa tete nchini Iran, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, OHCHR imesema ina wasiwasi mkubwa kutokana na vikosi vya usalama nchini Iran humo kuendelea kutumia hatua kali za kudhibiti waandamanaji, huku njia za mawasiliano zikidhibitiwa na kuathiri mawasiliano kwa njia ya simu za mezani na kiganjani halikadhalika mitandao ya kijamii.

Msemaji wa Ofisi hiyo Ravina Shamdasani amewaambia waandishi wa Habari mjini Geneva, Uswisi hii leo kuwa maelfu ya watu wamejitokeza kushiriki maandamano dhidi ya serikali kwa siku 11 mfulilizo zilizopita kufuatia kifo cha msichana Mahsa Amini mikononi mwa polisi, huku vikosi vya usalama vikitumia wakati mwingine risasi kudhibiti maandamano hayo.

“Raia wengi wa Iran wameuawa, wamejeruhiwa au kuswekwa rumande wakati maaandamano hayo yaliyoibuka baada ya msichana huyo mwenye umri wa miaka 22 kukamatwa tarehe 13 mwezi huu wa Septemba kwa madai ya kutovaa Hijab kwa kanuni zinazotakiwa na serikali ya Iran, msichana ambaye hatimaye alifia korokoroni,” amesema Bi. Shamdasani.

Mawasiliano  yamedhibitiwa Iran

Msemaji huyo amefafanua kuwa kutokana na udhibiti wa mawasiliano, ni vigumu kubaini idadi kamili ya vifo, majeruhi na walioswekwar umande.

“Tarehe 24 mwezi huu wa Septemba, chombo cha Habari cha serikali ya Iran kiliripoti kuwa waliouawa ni 41. Mashirika ya kiraia yanayofuatilia matukio hayo yameripoti idadi kubwa Zaidi ya vifo, wakiwemo wanawake na Watoto, na mamia wamejeruhiwa katika majimbo angalau 11,” amesema afisa huyo wa OHCHR.

Tunahofia viongozi Iran wanakashifu waandamanaji

Amesema hofu yao kubwa hivi sasa ni maoni ya baadhi ya viongozi ya kukashifu na kutukana baadhi ya waandamanaji, na matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayofanywa na vikosi vya usalama dhidi ya waandamanaji.

“Bunduki katu hazipaswi kutumia kutawanya mikusanyiko. Katika suala la mikusanyiko, wanapaswa kutumia risasi pale tu kuna tishio la uhaki au majeruhi.”

Ripoti zinadokeza kuwa mamia ya watu wamekamatwa, wakiwemo watetezi wa haki za binadamu, wanasheria, wanaharakati wa mashirika ya kiraia na takribani waandishi wa Habari 18.

Idadi sahihi ya waliokufa au waliojeruhiwa bado kizungumkuti

Serikali ya Iran bado haijatangaza idadi ya waliokamatwa ingawa katika jimbo la Gilan peke yake, Mkuu wa Polisi amesema katika siku tatu zilizopita watu 736  wamekamatwa, wakiwemo wanawake 60.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu imetoa wito kwa mamlaka za Iran kuhakikisha haki za waliokamatwa zinazingatiwa na mchakato sahihi unatumika kuachilia huru wale wote waliokamatwa kiholela.