Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaendelea kufuatilia kinachoendelea Iran

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres

UN yaendelea kufuatilia kinachoendelea Iran

Haki za binadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anafuatilia kwa karibu maandamano yanayoendelea nchini Iran ambayo chanzo chake ni kifo cha msichana Mahsa Amini aliyekufa mikononi mwa polisi baada ya kukamatwa tarehe 13 Septemba kwa madai ya kuvaa hijabu kinyume na inavyotakiwa nchini humo.

Taarifa iliyotolewa jijini New York, Marekani Jumanne usiku na msemaji wa Umoja wa Mataifa inasema Katibu Mkuu anafuatilia hali inayoendelea wakati huu ambapo wakati wa mkutano kati yake na Rais Ebrahim Raisi wa Iran kando mwa mikutano ya Umoja wa Mataifa tarehe 22 mwezi huu wa Septemba jijini New York, alimsisitizia Bwana Raisi juu ya umuhimu wa kuheshimu uhuru wa wananchi kujieleza, haki yao ya kukusanyika kwa amani na uhuru wa kujiunga kwenye vikundi.

“Tunaendelea kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu ripoti za vifo wakiwemo wanawake na watoto, vifo vinavyotokana na maandamano hayo,” imesema taarifa hiyo.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa vikosi vya usalama kujizuia kutumia nguvu kupita kiasi na ametoa wito kwa kila mtu kujizuia ili kuepusha ghasia zaidi.

Halikadhalika taarifa hiyo imemnukuu Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa akisisitiza umuhimu wa uchunguzi huru na wa haraka kuhusu kifo hicho cha Bi. Amini, na kwamba uchunguzi huo ufanywe na mamlaka yenye uwezo.

Maelfu ya watu wamejitokeza kushiriki maandamano dhidi ya serikali kwa siku 11 mfulilizo zilizopita kufuatia kifo cha Mahsa kilichotokea siku tatu baada ya kukamatwa na polisi tarehe 13 mwezi huu  na kuswekwa korokoroni.

TAGS: Mahsa Amini, Iran, Antonio Guterres, Haki za Binadamu